Fernandes avuna Sh12.5 bilioni kwa picha tu
Muktasari:
- Kiungo huyo wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 31 anaingia katika miezi 12 ya mwisho ya mkataba wake wa sasa, lakini viongozi wa Manchester United wameweka wazi kuwa hawana mpango wa kumruhusu aondoke kwa hali yoyote.
LONDON, ENGLAND: NAHODHA wa Manchester United, Bruno Fernandes, ameingiza kiasi cha pauni 9.2 milioni (zaidi ya Sh12.5 bilioni za Tanzania) kupitia mapato ya haki za matumizi ya picha (image rights), huku klabu hiyo ikijiandaa kumpa mkataba mpya wa kuendelea kubaki Old Trafford.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 31 anaingia katika miezi 12 ya mwisho ya mkataba wake wa sasa, lakini viongozi wa Manchester United wameweka wazi kuwa hawana mpango wa kumruhusu aondoke kwa hali yoyote.
Man United tayari ina kipengele cha kuongeza mkataba wake kwa mwaka mmoja zaidi, lakini sasa inatajwa kutaka kumpa makubaliano mapya ya muda mrefu.
Msimu uliopita Fernandes aliandika historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza wa Manchester United kutwaa tuzo ya Football Writers' Player of the Year tangu Wayne Rooney alipofanya hivyo miaka 16 iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa za kifedha zilizowasilishwa na kampuni yake ya haki za picha, BF8 Sports Ltd, nyota huyo aliingiza pauni 9.2 milioni kutokana na shughuli zake nje ya uwanja.
Nyaraka za msimu wa 2024-25 zinaonyesha kampuni hiyo, aliyoianzisha mwaka 2020 kwa ajili ya kusimamia mapato yake ya kibiashara, sasa ina akiba ya pauni 9.5 milioni, ikiwa ni ongezeko la pauni1.1 milioni ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, sawa na karibu pauni 100,000 za ziada kila mwezi.
Baada ya kulipa gharama zote za uendeshaji, Fernandes alibaki na faida ya pauni 9,180,001.
Mapato hayo yanakuja juu ya mshahara wake wa uwanjani. Fernandes anaripotiwa kulipwa takribani pauni12.5 milioni kwa mwaka na Manchester United, bila kujumuisha bonasi, mapato ya haki za picha na mikataba ya udhamini na kampuni kubwa kama Nike, DHL na EA Sports.
Mbali na hilo, kiungo huyo pia anaripotiwa kumiliki mali kadhaa pamoja na nyumba nchini England na Ureno.
Fernandes anatarajiwa kujiunga na kikosi cha Manchester United kwa maandalizi ya msimu mpya mara baada ya kukamilisha mapumziko yake kufuatia kushiriki Kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa ya Ureno.