David Beckham uso kwa uso na Michael Jordan
Muktasari:
- Beckham mwenye umri wa miaka 51 alionekana akimkumbatia Jordan, 63, huku wote wakiwa wameongozana na wake zao wakati wa chakula cha mchana katika mazingira ya jua kali la Ibiza.
IBIZA, HISPANIA: GWIJI wa England, David Beckham amekutana na shujaa wake wa mpira wa kikapu, Michael Jordan, wakati wa mapumziko visiwani Ibiza nchini Hispania, katika picha zilizowavutia mashabiki wa michezo duniani.
Beckham mwenye umri wa miaka 51 alionekana akimkumbatia Jordan, 63, huku wote wakiwa wameongozana na wake zao wakati wa chakula cha mchana katika mazingira ya jua kali la Ibiza.
Nyota huyo wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya England alikuwa pamoja na mkewe, mbunifu wa mitindo Victoria Beckham, 52, huku Jordan akiwa na mkewe, mwanamitindo wa Cuba, Yvette Prieto, 48.
Katika moja ya picha zilizosambaa, Beckham mwenye urefu wa takribani futi sita alionekana akitabasamu huku akimtazama juu Jordan mwenye urefu wa futi 6 na inchi 6.
Uhusiano wa Beckham na Jordan una historia ya kipekee. Alipoihama Manchester United na kujiunga na Real Madrid mwaka 2003, Beckham alichagua kuvaa jezi namba 23, namba iliyotukuka kutokana na mafanikio makubwa ya Jordan akiwa na Chicago Bulls.
Beckham aliwahi kukiri kuwa alipatwa na msisimko mkubwa alipokutana na Jordan kwa mara ya kwanza katika mgahawa mmoja.
"Ingawa alikuwa amekaa mezani pamoja na Madonna na watu wengine, macho yangu yote yalikuwa kwake," aliwahi kusema Beckham.
Ameongeza kuwa mkewe Victoria alimchokoza kwa kumgusa mguuni na kumwambia: "Acha kuniaibisha."
Baada ya Madonna kuwapelekea chupa ya champagne mezani kwao, Beckham na Victoria waliamua kwenda kumsalimia Jordan.
Akikumbuka tukio hilo, Beckham amesema: "Michael alisimama, nikamshika mkono, lakini mkono wake ulikuwa mkubwa kiasi kwamba ulifunika karibu mkono wangu wote."
Mkutano huo umeonyesha jinsi hata mastaa wakubwa wa soka wanaweza kuwa mashabiki wa wanamichezo wengine, huku Beckham akiendelea kuonyesha heshima kubwa kwa mmoja wa magwiji wakubwa zaidi katika historia ya mchezo wa mpira wa kikapu.