Shai alivyovunja rekodi ya miaka 63
Muktasari:
- Itakumbukwa kwamba Chamberlain alifunga pointi hizo au zaidi katika michezo 126 miaka 63 iliyopita na hivyo aliendelea kuikumbatia rekodi hiyo kwa zaidi ya nusu karne, ambapo licha ya kupita mastaa kibao wa mchezo huo, lakini hakuna aliyeweza kuifikia.
HABARI kubwa kwa sasa duniani katika medani za kikapu ni juu ya nyota wa Oklahoma City Thunder, Shai Gilgeous-Alexander alivyofanikiwa kuweka rekodi mpya katika Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), baada ya kufikisha mchezo wa 127 mfululizo akifunga pointi 20 au zaidi, akimpita gwiji wa mpira wa kikapu Wilt Chamberlain.
Itakumbukwa kwamba Chamberlain alifunga pointi hizo au zaidi katika michezo 126 miaka 63 iliyopita na hivyo aliendelea kuikumbatia rekodi hiyo kwa zaidi ya nusu karne, ambapo licha ya kupita mastaa kibao wa mchezo huo, lakini hakuna aliyeweza kuifikia.
Mfululizo huo wa mafanikio wa Shai ulianza Novemba 1, 2024, na ulifikia kiwango cha kihistoria wiki hii wakati alipofunga mtupo wa kuruka juu ya eneo la 'key' dhidi ya Baylor Scheierman katika mchezo dhidi ya Boston Celtics.
Awali, mwanzo alianza polepole, lakini rekodi ikaonekana wazi kwamba alikuwa akiisaka kwani kadri muda ulivyosonga ndivyo pia alivyoendelea kufanya mambo mazuri, kwani hakufunga pointi yoyote katika nusu ya kwanza ya robo ya kwanza.
Hata hivyo, kufikia mwisho wa dakika 12 za kwanza tayari alikuwa na pointi 10, jambo lililoonyesha wazi kuwa kuvunja rekodi hiyo kulikuwa karibu kutokea.
Kinachofanya rekodi hiyo iwe ya kuvutia zaidi ni kwamba katika michezo 35 kati ya 127, Shai hakuhitaji hata kucheza robo ya nne kwa sababu Thunder walikuwa wanaongoza kwa tofauti kubwa ya pointi.
Katika mchezo huo, Shai alimaliza na pointi 35, akiiongoza Thunder kushinda 104–102 dhidi ya Celtics katika mchezo uliokuwa wa kusisimua.
Kocha wa Thunder, Mark Daigneault alisema kabla ya mchezo watapambana ili nyota huyo avunje rekodi nyingi.
“Anafanya kazi kubwa na nyuma ya mafanikio hayo anafanya hivyo kwa uthabiti. Ni mtu anayependa ubora katika kazi yake. Ana kiwango cha juu anachojiwekea, lakini pia ana uelewa mkubwa kwa wachezaji wenzake,” alisema kocha huyo.
Rekodi ya Chamberlain ilikuwaje zamani? Kwa upande wa Chamberlain, mfululizo wake uliisha ghafla baada ya kutolewa nje mapema kwa kadi katika mchezo ambao ungekuwa wa 127, hivyo akabaki kuwa na michezo 126 ya ufanisi wa kufunga pointi 20 au zaidi. Baada ya tukio hilo, aliendelea tena na michezo 92 mfululizo akifunga pointi 20 au zaidi, jambo linaloonyesha ubora wa kiwango chake wakati huo.
JORDAN ASHINDWA KUJIZUIA
Katika hatua nyingine, mastaa wengi wa zamani katika historia ya NBA, wamempongeza nyota wa Miami Heat, Bam Adebayo baada ya kuweka historia kwa kufunga pointi 83 katika mchezo mmoja, ambapo miongoni mwao ni gwiji wa kikapu anayechukuliwa kuwa bora wa muda wote, Michael Jordan.
Wadau wa NBA wanaendelea kushangazwa na kile alichofanya Adebayo. Nyota huyo wa Miami Heat alishtua wengi kufuatia kufunga pointi 83 katika ushindi wa 150–129 dhidi ya Washington Wizards kwenye Uwanjan wa Kaseya Center. Pointi hizo 83 ni za pili kwa wingi katika historia ya NBA katika mchezo mmoja.
Kabla ya hapo, mara ya mwisho mchezaji kufikisha zaidi ya pointi 80 ilikuwa 2006 wakati hayati Kobe Bryant alipofunga pointi 81 dhidi ya Toronto Raptors. Rekodi ya juu kabisa bado inashikiliwa na Wilt Chamberlain aliyefunga pointi 100 katika mchezo mmoja 1962.
Katika miaka ya hivi karibuni baadhi ya nyota walikaribia kufikia kiwango hicho kama vile Damian Lillard na Donovan Mitchell waliowahi kutupia pointi 71. Pia Luka Doncic aliwahi kufunga pointi 74 mwaka 2024 alipokuwa Dallas Mavericks. Cha kushangaza zaidi ni kwamba kabla ya mchezo dhidi ya Wizards, rekodi ya juu ya Adebayo katika maisha yake ya NBA ilikuwa pointi 41.
Baada ya mchezo huo wa kihistoria, Adebayo alisema hata Michael Jordan alimtafuta na kumpongeza, na alipoulizwa kuhusu alichosema Jordan, Adebayo alisema: “Aliniambia tu: Hongera. Ujumbe mfupi sana.”
Adebayo aliongeza kuwa, “ukijua tabia ya Mike, huwa si mtu wa kuongea sana.”
Wakati huohuo, gwiji mwingine wa NBA, Magic Johnson alimpongeza Adebayo kupitia mitandao ya kijamii kwa kuvunja rekodi ya pointi 81 ya Bryant na kuwa na mchezo wa pili wenye pointi nyingi katika historia ya NBA.