WAKO POA! Kutoka mchangani hadi kuubonda mwingi Ligi Kuu England

Muktasari:
- Kwenye Ligi Kuu England kwa sasa utakutana na sura za mastaa wanaopiga kazi kikwelikweli ndani ya uwanja, utadhani wameibuka tu kutoka kwenye timu kubwa, lakini kumbe waliwahi kukipiga mchangani. Hawa mastaa wameburuza sana mchangani.
LONDON, ENGLAND: UMEONA zile sevu za David Raya anazofanya pale Arsenal? Au vile anavyofanya Ollie Watkins kuwakimbiza mabeki wa timu pinzani kwenye mechi za Ligi Kuu England akiwa na kikosi chake cha Aston Villa? Wote wako moto, lakini kumbe walicheza mchangani.
Kwenye Ligi Kuu England kwa sasa utakutana na sura za mastaa wanaopiga kazi kikwelikweli ndani ya uwanja, utadhani wameibuka tu kutoka kwenye timu kubwa, lakini kumbe waliwahi kukipiga mchangani. Hawa mastaa wameburuza sana mchangani.

MAKIPA
Nick Pope (Newcastle); Baada ya kusajiliwa Charlton Athletic, Pope alitolewa kwa mkopo kwenda kwenye timu za mchangani Harrow Borough, Welling United, Cambridge United, Aldershot Town, York City na Bury, aliyosaidia kupanda hadi League One.
David Raya (Arsenal); Alipojiunga na Blackburn Rovers mwaka 2012, Mhispaniola alipata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza baada ya miezi minne ya kucheza kwa mkopo kwenye klabu ya Southport, ambapo alitumika kwenye mechi 24.
Dean Henderson (Crystal Palace); Alihitimu kutoka kwenye akademia ya klabu ya Manchester United, kipa huyo alisenda kucheza kwa mkopo Stockport County mwaka 2016.
Alex Palmer (Ipswich); Wakati akiwa West Bromwich Albion, Palmer alitolewa kwa mkopo kwenda kucheza klabu ya mtaani kwao Kidderminster Harriers.
Aaron Ramsdale (Southampton); Mwaka 2015, kipa huyo alienda kucheza kwa mkopo katika klabu ya Worksop Town na alicheza mechi moja baada ya kipa wa kikosi hicho kutumikia adhabu.

MABEKI
Marc Guehi (Crystal Palace); Nahodha wa Crystal Palace alianzia maisha yake ya soka kuichezea Cray Wanderers kipindi hicho akiwa na umri wa miaka sita kabla ya skauti wa Chelsea kumgundua na kwenda kujiunga Chelsea.
James Tarkowski (Everton); Alicheza mechi yake ya kwanza kwenye kikosi cha wakubwa huko Manchester kabla ya kukubali ofa ya kwenda kujiunga na Oldham Athletic akiwa na umri wa miaka 19.
Max Kilman (West Ham); Kilman maisha yake ya mwanzoni kwenye soka alizichezea timu za Welling United, Maidenhead United na Marlow.
Tyrone Mings (Aston Villa); Soka la mchangani ni kitu cha kawaida kwenye familia ya kina Mings - baba yake Adie ni mchezaji wa zamani wa Forest Green. Baada ya miaka minane kwenye akademia ya Southampton, Mings alijiunga na timu ya mchangani ya Yate Town na baadaye alienda Chippenham Town.
Ethan Pinnock (Brentford); Baada ya kuhitimu elimu ya chuo na kupata shahada yake, akiwa anachezea Dulwich Hamlet, Pinnock alijiunga na timu ya mchangani ya Forest Green Rovers. Alisaidia timu hiyo kupata daraja na kucheza Football League kabla ya kuhamia Barnsley na baadaye Brentford.
Dan Burn (Newcastle); Burn alifunga kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Ligi kuipa timu yake taji la kwanza baada ya miaka 70, lakini beki huyo maisha yake ya soka siku za mwanzo, alicheza sana timu za mchangani ikiwamo Blyth Town, Blyth Spartans na Darlington.

VIUNGO
Solly March (Brighton); Kabla ya kujiunga na Brighton, Desemba 2011, March alitumikia timu ya watoto ya Eastbourne Borough kabla ya kujiunga na klabu ya mtaani kwao Lewes. Baada ya miezi mitatu Dripping Pan alisajiliwa Brighton.
Ryan Yates (Nottingham Forest); Aliibukia kutoka kwenye akademia ya Nottingham Forest, Yates alikwenda kupata uzoefu wa kucheza kwa mkopo kwenye timu ya mchangani ya Barrow msimu wa 2016/17.
Jack Taylor (Ipswich); Kiungo huyo alitumia sehemu kubwa ya maisha ya soka la utotoni kwenye klabu ya Chelsea kabla ya kujiunga na Barnet mwaka 2012. Katika kipindi hicho alitolewa kwa mkopo mchangani Hampton & Richmond.
Sam Szmodics (Ipswich); Baada ya kutajwa kuwa Kinda Bora wa Mwaka wa Colchester United katika msimu wa 2014/15, staa huyo wa Ireland alitumikia msimu wa 2015/16 kwa mkopo huko Braintree Town kwenda kupata uzoefu wa kucheza kikosi cha kwanza.

WASHAMBULIAJI
Dominic Calvert-Lewin (Everton); Baada ya kuhitimu katika akademia ya Sheffield United, Calvert-Lewin alikwenda kucheza kwa mkopo Stalybridge Celtic na alifunga mabao mawili mechi yake ya kwanza dhidi ya Hyde United.
Ollie Watkins (Aston Villa); Fowadi huyo wa Aston Villa alijiunga na akademia ya Exeter City kwenye kikosi cha chini ya umri wa miaka 11 kabla ya kutolewa kwa mkopo Weston-super-Mare, ambako alifunga mabao 20 katika mechi 25.
Jamie Vardy (Leicester); Straika wa Leicester City, Vardy alikuwa na umri wa miaka 27 wakati anacheza mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu England baada ya kutumikia miaka tisa ya kucheza mchangani Stocksbridge Park Steels, Halifax Town na Fleetwood Town. Vardy alijiunga na Leicester mwaka 2012 na kuipa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2015/16.
Callum Wilson (Newcastle); Wakati alipokuwa Coventry City kama mchezaji wa akademia yao, Wilson alitolewa kwa mkopo Kettering Town na Tamworth. Baadaye alienda kujiunga na Bournemouth mwaka 2014 na miaka sita baadaye, akatua Newcastle United.
Jarrod Bowen (West Ham); Winga huyo wa West Ham United alicheza mechi yake ya kwanza kwenye kikosi cha wakubwa Machi 2014 kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 17, alipotumikia Hereford United. Alicheza vizuri na Hull City kumsajili. Bowen alijiunga na West Ham, Januari 2020.
Michail Antonio (West Ham); Kinara wa mabao wa West Ham United kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, aliwahi kucheza mchangani kwenye klabu za Tooting & Mitcham United.