Jihan alivyotinga 'top 3' Miss Grand International
Muktasari:
- Jihan sasa amebaki na warembo wawili kutoka nchi ya Vietnam na Ecuador katika mchuano huu yani “Top 3” huku kila mmoja akihitaji kura za kutosha ili kufuzu hatua inayofuata.
MAMBO yanazidi kupamba moto nchini Thailand kwani mrembo anayepeperusha bendera ya Tanzania, Jihan Dimack, ameendelea kufanya vizuri katika mashindano ya Miss Grand International 2026, baada ya kufuzu hatua ya tano ya “Country’s Power of the Year” ikiwa ni tuzo ya nguvu ya nchi ya mwaka.
Jihan sasa amebaki na warembo wawili kutoka nchi ya Vietnam na Ecuador katika mchuano huu yani “Top 3” huku kila mmoja akihitaji kura za kutosha ili kufuzu hatua inayofuata.
Warembo wawili watakaokusanya kura nyingi zaidi wataingia hatua ya mwisho ya washindani wawili, huku mshindi akipewa nafasi ya moja kwa moja ya kuingia 20 bora ya fainali kuu.
Kwa upande wa Tanzania, sasa ni muda wa kuongeza ushirikiano ili kufanikisha Jihan anarudi nyumbani na ushindi, mashabiki wameanza kuongeza nguvu wakifuatilia mwenendo wa Jihan na kuhamasishana kuhakikisha kura hazipotei.
Kura zimefunguliwa Oktoba 5, 2026, na zoezi hilo litafungwa Oktoba 7 saa 3:00 usiku kwa saa za Tanzania na Kura moja inagharimu Sh2,800, sawa na inapigwa kupitia tovuti rasmi ya Miss Grand International.
Safari hii, umaarufu hautoshi kwani Kura ndizo zinaweza kuamua hatma ya Jihan na kila kura inaweza kuwa na maana katika safari yake ya kuelekea 20 bora.
Macho yote sasa yanaelekezwa Oktoba 7, siku ambayo majina ya warembo wawili watakaofuzu hatua ya mwisho yatatangazwa.
Kwa Tanzania, huu si wakati wa kutazama tu Jihan yupo jukwaani kuibeba bendera ya Tanzania, lakini nguvu kubwa iko kwa watanzania na bara la Afrika.