MUSIC FACTS: Mabantu na Hamisa Mobetto tangu kitambo tu!

Muktasari:
- Hata hivyo, safari yao haikuwa rahisi hadi kufika walipo, kwa miaka mingi walilazimika kupita huko na kule wakijitafuta na hatimaye wamejipata kwani muziki wao unawatambulisha vizuri wao ni kina nani na uwezo wao ni upi.
Ndani ya Bongo Fleva kwa sasa miongoni mwa makundi machache yaliyosalia na kuendelea kufanya vizuri ni pamoja na Mabantu ambao muziki wao ni maarufu hasa kwa vijana watafutaji na wapenda bata kwa sana.
Hata hivyo, safari yao haikuwa rahisi hadi kufika walipo, kwa miaka mingi walilazimika kupita huko na kule wakijitafuta na hatimaye wamejipata kwani muziki wao unawatambulisha vizuri wao ni kina nani na uwezo wao ni upi.
1. Kundi la Mabantu linaundwa na wasanii wawili ambao ni ndugu, Muuh ni mtoto wa mama mkubwa na Twaah akiwa mtoto wa mama mdogo lakini hawakuwahi kufahamiana hadi pale muziki ulipowakutanisha kwa mara ya kwanza wakiwa Dar es Salaam.
Jina la Mabantu lilikuja baada ya kuunganisha majina yao, Muuh na Twaah, na neno ‘Bantu’ katika jina lao lina maana ya wao kama wasanii kufanya muziki unaotumiza zaidi lugha ya Kiswahili ambayo asili yake ni Kibantu.
2. Twaah aliondoka kwao Mtwara akiwa na umri wa miaka 12 na kuja Dar es Salaam kufanya muziki, baba yake mzazi alifungwa jela tangu akiwa na umri wa miaka sita, hivyo maisha ya nyumbani hayakuwa mazuri na ndio sababu ya kuondoka.
3. Kufika Dar akajiunga na Mkubwa na Wanawe, hivyo kundi la Mabantu lilianza muziki katika kituo hicho cha Mkubwa Fella na walidumu hapo kwa takribani miaka mitano ingawa kila mmoja aliingia Mkubwa peke yake na kwa wakati wake.
4. Baada ya Aslay kuvutiwa na uimbaji wa Muuh, akapendekeza aingie Mkubwa na Wanawe na ndiye alikuwa msanii wa kwanza kutambulishwa wakati huo akitumia jina la Dogo Muuh. Kwa upande wake Twaah alikuja kutambulishwa kupitia video ya wimbo wa Quick Rocka na Ngwea, My Baby (2013) ambayo Miss XXL After School Bash 2010, Hamisa Mobetto alitokea pia kama vixen.
5. Katika shoo ya kuadhimisha miaka saba ya Tanzania House of Talent (THT) iliyofanyika Dar Live ndipo uwezo wa Twaah ulionekana baada ya kuomba kuonyesha kipaji chake jukwaani, wakati huo alikuwa anachana na sio kuimba.
6. Siku iliyofuata alifika Mkubwa na Wanawe na kukutana na Beka Flavour wa Yamoto Band na Chambuso aliyempa nafasi ya kurekodi, na Muuh ndiye alichaguliwa kuimba kiitikio cha wimbo huo na baada ya muda ndipo wakaja kugundua wao ni ndugu.
7. Kipindi wanatafuta njia ya kutoka baada ya kuachana na Mkubwa na Wanawe, Mabantu waliletewa Marioo na rafiki yao, Kusah na kuambiwa naye ni msanii anayepambana kutoka, baadaye Marioo akamleta Whozu ambaye naye alikuwa anapambana kutoka. Cha kufurahishwa kwa sasa ni kwamba Mabantu, Marioo, Kusah na Whozu wote wameshatoka kimuziki na wameshirikiana sana katika nyimbo zao ambazo baadhi zimefanya vizuri.
8. Wimbo wao, No Love No Stress (2020) ndio uliokuja kuwatambulisha vizuri ila mwanzo uligoma, wakaamua wafanye remix yake na kuwashirikisha Young Lunya na Moni Centrozone, basi remix yake ikaenda sana na ukawa mwanzo wa wao kujulikana zaidi. Na video ya wimbo huo ndio ilikuwa ya kwanza kwa wao kuingia trend katika mtandao wa YouTube kitu ambacho awali hawakuwahi kukifikiria kama kitakuja kutokea hasa kupitia wimbo huo.
9. Young Lunya aliyesainiwa Sony Music ndiye rapa pekee Bongo ambaye Mabantu wamefanya naye kolabo nyingi, Lunya amesikika katika nyimbo zao tatu ambazo ni No Love No Stress Remix (2020), Sponsa (2020) na Nawekera (2020).
Hiyo ni kutokana Young Lunya naye aliwahi kupita Mkubwa na Wanawe, hivyo walikuwa wanafahamiana tangu kitambo ila Lunya ndiye alitangulia kutoka kimuziki chini kundi la OMG waliosainiwa Switch Music Group (SMG).
10. Hawajawahi kutoa albamu bali EP moja, University (2023), na hawajawahi kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) ila wana nyimbo nyingi maarufu huku wakishirikiana na wasanii wakubwa kama Rayvanny, Harmonize, Marioo, Navy Kenzo n.k.
Pia Mabantu wanaofanya vizuri sasa na wimbo wao, Kigamboni (2025), wamewahi kurekodi na wasanii wengine wakubwa kama Diamond Platnumz na Khaligraph Jones wa Kenya lakini nyimbo hizo hadi sasa hazijatoka kwa sababu ambazo zipo nje ya uwezo wao.