Ushindani wa Paula, Fahyma umehamia huku!
Muktasari:
- Warembo hao ambao wamejizolea umaarufu katika mitandao ya kijamii kutokana na mtindo wao wa maisha, mavazi na urembo, awamu hii wamegeuza ushindi wao kuwa biashara zaidi wakitumia vizuri mtaji wa mashabiki walionao.
WAPENZI wa wanamuziki wa Bongofleva, Marioo na Rayvanny, Paula na Fahyma, bado suala lao halijaisha kwani ushindi wa chini kwa chini baina yao ndio umechukua nafasi kwa sasa, sema tu wamebadilisha uwanja awamu hii.
Warembo hao ambao wamejizolea umaarufu katika mitandao ya kijamii kutokana na mtindo wao wa maisha, mavazi na urembo, awamu hii wamegeuza ushindi wao kuwa biashara zaidi wakitumia vizuri mtaji wa mashabiki walionao.
Kila mmoja amejitosa katikati uwanja wa kutengeneza maudhui (content creation) ambapo Vlog zao kupitia mtandao wa YouTube zimekuwa zikifuatilia na kuibua mijadala, na huku ndio ulipohamia ushindi wao.
Vlog (blog ya video) ni aina ya maudhui ambapo mtu anajirekodi video akiongea, kuonyesha maisha yake, au kufanya shughuli fulani, kisha anaiweka mtandaoni ili watu kutazama kwa lengo la kujifunza na hata kuburudika.
Mtu anaweza kurekodi jinsi siku yake iliyokuwa, safari, kupika, mazoezi au gym, maisha yake binafsi au matukio maalumu kama sherehe ya kumbukizi ya kuzaliwa, yaani birthday party.
Vlog hupatikana katika mitandao kama YouTube, TikTok, Instagram na Facebook, ambayo ina watumiaji wengi duniani.
Wiki hii Fahyma katika Vlog yake mpya ameonyesha mambo mengi ikiwemo alivyosherehekea sikukuu ya Eid pamoja na familia yake, hasa pamoja na mzazi mwenzie Rayvanny pamoja na mtoto wao wa pekee, Jaydan aliyezaliwa Aprili 2017.
Hata hivyo, kuna kipande ambacho kimeibuka maoni mengi kutoka kwa mashabiki, nacho ni kile alichokuwa akionyesha chumba ambacho anaishi pamoja na Rayvanny, na namna wanavyopangilia vitu vyao kama mavazi.
Hili ndio hasa limeonyesha wazi kuna ushindani mkali wa chini kwa chini baina yake na Paula ingawa wote wawili kwa nyakati tofauti wamewahi kukanusha hilo.
Paula, binti wa Kajala Masanja na P-Funk Majani, ndiye hasa aliyeanza kufanya Vlog akishirikiana na mama yake, na baadaye Marioo na Harmonize walikuja kuonekana katika mradi huo ambao mrembo huyo kaweka nguvu zake zote.
Katika moja Vlog ya Paula ambayo iliruka YouTube hapo Februari 8, alifanya kile alichoita “room tour” akionyesha chumba chake cha kulala kilivyo kwa sasa baada ya kufanya ukarabati mkubwa.
Mzazi mwenzie Marioo alimpongeza kwa kutoa mawazo ya kibunifu ambayo yamependesha chumba chao, huku Paula akisema hiyo ilikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu, na pia akimshukuru baba yake kwa kumsaidia baadhi ya vitu.
Kwa muktadha huo, alichofanya Fahyma wiki hii akionyesha chumba chake, tunaweza kusema amelipa deni kwa mshindani wake, hivyo pia tutegemee ushindani mkubwa wa kimaudhui siku zijazo.
Ikumbukwe awali Fahyma alijikita upande wa mitindo hadi kushinda tuzo mbalimbali za kimataifa kama Scream Awards (Nigeria), Starqt Awards (Afrika Kusini) na Swahili Fashion Week Awards (Tanzania ).
Ushindani wa wawili hao umewahi kuwahusisha hata wapenzi wao kupitia muziki wao, na yote yalianza baada ya Paula kuwa na Marioo kufuatia kuachana na Rayvanny ambaye aliamua kurudiana na Fahyma ambaye wamekuwa pamoja kwa zaidi ya miaka 10 sasa.
Mnamo Novemba 2023, Rayvanny aliachia video ya wimbo wake ‘Mwambieni’ akimshirikisha Mac Voice ambaye alikuwa akimsimamia kimuziki kupitia lebo yake ya Next Level Music (NLM) tangu Septemba 2021 alipomtambulisha.
Katika video ya wimbo huo alionekana Fahyma, hatua ambayo ilitafsiriwa na wengi kama kujibu mashambulizi kwa kile walichofanya Marioo na Paula.
Hiyo ilikuwa ni video ya tatu kwa Rayvanny na Fahyma kufanya pamoja ndani ya mwaka huo wa 2023, na kwa ujumla ikiwa ni video sita, na hivyo kumfanya Fahyma kuwa mrembo pekee aliyetokea mara nyingi zaidi katika video za mwanamuziki huyo.
Ikumbukwe hadi sasa Fahyma ameonekana katika video za nyimbo za Rayvanny kama Kwetu (2016), Natafuta Kiki (2016), Siri (2017), Forever (2023), Habibi (2023) na Mwambieni (2023).
Kwa upande mwingine, kitendo cha Rayvanny kumtumia Fahyma katika video zake tatu kwa mwaka 2023, kilikuwa ni sawa na kile alichofanya Marioo na Paula ndani ya mwaka huo huo.
Paula ameonekana katika video saba za Marioo - Lonely (2023), Tomorrow (2023), Sing (2023), Hakuna Matata (2024), My Daughter (2024), Unachekesha (2024) na Tete (2025), na ndiye mrembo aliyetokea mara nyingi zaidi katika video zao mwanamuziki huyo.
Hivyo baada ya Fahyma na Paula kuonekana zaidi katika video zao wapenzi wao hadi kufikia video tatu kwa mwaka kwa kila mmoja, kwa sasa wamebadili upepo wakihamishia ushindani wao upande wa Vlog.