Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakali hawa wamesimamisha shilingi kwenye singeli

Muktasari:

  • Lakini, nyuma ya vipaza sauti vya muziki huo kuna majina kibao yanayochipukia na yaliyochipua kitambo sasa ambayo yanafanya vizuri, ambayo kwa ujumla wake yanaacha swali la ni nani mkali kati yao? Twende pamoja!

Kuna wakali kibao katika muziki wa kizazi kipya maarufu Bongofleva. Lakini pia kuna ule wa singeli ambao nao umekuwa na mvuto wake na umegeuka kuwa ajira kwa vijana wenye kipaji cha kuimba, na ni huo ambao baadhi ya wadau wa muziki nchini wamekuwa wakiupigia chapuo uwe ndio utambulisho wa muziki wa Kibongo.

Lakini, nyuma ya vipaza sauti vya muziki huo kuna majina kibao yanayochipukia na yaliyochipua kitambo sasa ambayo yanafanya vizuri, ambayo kwa ujumla wake yanaacha swali la ni nani mkali kati yao? Twende pamoja!


D VOICE MWENYE SAUTI YAKE

KAMA kuna jambo ambalo Abdul Hamisi Mtambo maarufu D Voice amelifanya tangu ajiunge na Lebo ya WCB Wasafi, ni kuonyesha kuwa msanii wa muziki wa singeli anaweza kutoka kufanya muziki wa kawaida mitaani na kuingia kwenye biashara kubwa ya burudani bila kupoteza uwezo wake wa kujaribu mitindo mingine ya muziki.

D Voice amekuwa miongoni mwa majina yanayovuta hisia za mashabiki wa muziki kutokana na uwezo wake wa kubadilika, kushirikiana na wasanii wakubwa na kuimba katika aina mbalimbali za muziki.

Mwanamuziki huyo siyo msanii anayejifungia kwenye singeli pekee, bali ana uwezo wa kufanya Bongofleva, Amapiano na mitindo mingine ya muziki. Vilevile, uwezo wake wa kuimba kwa sauti ya kawaida na kufanya vizuri katika maonyesho ya moja kwa moja umeongeza mjadala kuhusu ukubwa wa kipaji chake.

Hiyo ndiyo tofauti inayomfanya aonekane kama msanii anayeweza kutumia kipaji chake katika maeneo mbalimbali ya biashara ya muziki, kuanzia kurekodi nyimbo, kufanya kolabo, kupanda jukwaani hadi kushirikiana na kampuni mbalimbali katika shughuli za burudani.

Safari yake ndani ya WCB ilianza Novemba 16, 2023, alipotambulishwa rasmi na Diamond Platnumz. Siku iliyofuata, aliachia albamu yake ya Swahili Kid, iliyokuwa na nyimbo 10 na ushirikiano na Diamond, Zuchu, Mbosso na Lava Lava.

Kupitia albamu hiyo, D Voice alionesha kuwa anaweza kuingia katika soko pana zaidi ya singeli. Nyimbo kama BamBam, aliyomshirikisha Zuchu, na Tunapendana, aliyomshirikisha Mbosso, zimekuwa miongoni mwa kazi zilizompa nguvu kubwa kwenye majukwaa ya kidijitali. Mafanikio ya jumla ya D Voice hayapaswi kuchanganywa na takwimu za singeli pekee. Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa na Mwanaspoti Septemba 26, 2026, Kuachana Sh’ngapi ndiyo kazi yake ya Singeli iliyokuwa imefanya vizuri zaidi YouTube, ikiwa na watazamaji takribani milioni 2.4. Wakati huohuo, Tunapendana ilikuwa imefikisha watazamaji milioni 38, lakini ni wimbo wa Bongofleva.

D Voice alijijengea jina kupitia wimbo Kuachana Sh’ngapi wa mwaka 2021, kabla ya kujiunga na WCB. Wimbo huo ulipata umaarufu mkubwa na baadaye kufanyiwa remix iliyowashirikisha Barnaba, Lody Music na Platform.

Kazi nyingine zinazohusishwa na safari yake ya singeli ni Sio Unyama, Chizi Wee na Iyo. Kupitia kazi hizo, ameonesha kuwa bado ana nafasi ya kuendeleza muziki huo hata anapofanya kazi za Bongo Fleva.

Kwa upande wa biashara, uwezo wa kufanya aina tofauti za muziki unampa nafasi ya kufikia makundi mbalimbali ya mashabiki, jambo linaloweza kuongeza fursa za maonyesho na ushirikiano wa kibiashara.


MAKABILA BADO NI MTAMBO WA SINGELI

Hata hivyo, D Voice asifikirie kuwa kuutwaa ufalme wa singeli ni jambo rahisi, kwani Abdallah Ahmed maarufu kama Dulla Makabila, bado ni jina lenye uzito mkubwa katika muziki huo. Dulla amejenga jina kupitia nyimbo zenye simulizi za maisha, mapenzi, mipasho na matukio ya kila siku. Miongoni mwa kazi zake zinazotambulika ni Makabila, Hujaulamba, Dua, Miss Buza, Motoni Kumedamshi, Nimeghairi Kufa, Dakika Moja, Meli Ya Makolo, Madee na Kidonda, aliyomshirikisha Jay Melody.

Wimbo Kidonda umeonesha kuwa Dulla bado ana uwezo wa kuingia katika soko la sasa. Video yake ilifikisha watazamaji zaidi ya 500,000 ndani ya wiki ya kwanza, huku baadaye ikiendelea kuongeza idadi ya watazamaji. Pia amekuwa akiendelea kutoa kazi mpya, ikiwemo Mapenzi Yasakwe, aliyomshirikisha Zaiylissa. Hii inamfanya Dulla azidi kutikisa soko la singeli kama ilivyokuwa zamani, kwa kutoa nyimbo kali zinazowagusa watu wengi, hasa vijana walio katika mahusiano. Nyimbo nyingi anazofanya kwa sasa zinahusu kuumizwa katika mapenzi.


MSOMALI ANAINGIA VITANI

Riphati Jumanne Omary, maarufu kama Msomali Vitamin, naye ni miongoni mwa vijana wanaoendeleza ushindani katika muziki wa Singeli.

Kupitia nyimbo kama Nitampeleka kwa Mama, aliyomshirikisha Xouh, Ma Mkali, akiwa na Gigy Money, pamoja na Kwanini, Nina Ugwadu na Dada Amina, Msomali ameendelea kuonesha uwezo wa kutengeneza nyimbo zinazowagusa mashabiki.

Wimbo wake Nitampeleka kwa Mama umeonekana kuwa miongoni mwa kazi zinazofanya vizuri kwenye majukwaa ya kidijitali. Takwimu za Chartex zilizokusanywa zilionyesha kuwa wimbo huo ulikuwa na zaidi ya watazamaji 550,000 katika kipimo chake cha jumla cha video.


MALUME HAJABAKI NYUMA

Ibrah Malume ni jina jingine linalopaswa kuangaliwa katika ushindani huu. Kupitia kazi zake na ushirikiano na wasanii wengine, anaendelea kutafuta nafasi yake katika muziki wa singeli.

Miongoni mwa kazi zinazohusishwa naye ni Kosa Langu, aliyoshirikiana na Msomali Vitamin na Don Breezy, pamoja na Bunduki, aliyomshirikisha Vanillah. Video ya Bunduki imepata zaidi ya watazamaji 330,000 kwa mujibu wa takwimu za chati za YouTube zilizopatikana. Malume ni msanii ambaye ameanza kazi yake kwa kasi kubwa huku akijiongezea wafuasi wengi katika mitandao yake ya kijamii.