Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‎ Je, soka letu linatekwa na mihemko au sheria?

ZENGWE Pict


KWA misimu takriban mitatu mfululizo, wachambuzi, waandishi na viongozi wa klabu za soka wamekuwa wakibebesha waamuzi mzigo wa matokeo yote mabovu ya uwanjani, wakidai kuwa makosa ya kibinadamu ndiyo yaliyokuwa yakiamua matokeo ya mchezo na hata kuwatuhumu kuwa wanaenda kuchezesha mechi wakiwa na matokeo yao mfukoni.


Mijadala ya kila siku redioni, kwenye televisheni, magazetini na kwenye mitandao iliyotumia picha za marudio za kampuni iliyopewa haki ya kutangaza moja kwa moja Ligi Kuu, ilionyesha kuwa waamuzi wetu ni wa hovyo na hawana uwezo wa kuchezesha mechi za daraja la juu nchini.


Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, au Kamati ya Saa 72, ilitekwa na mijadala hiyo na haikuwa ajabu kuwa uamuzi ya chombo hicho muhimu yakalingana na majumuisho ya mijadala kuhusu uamuzi mbovu.

Waamuzi, ambao hawakuwa wamewezeshwa na waendeshaji mpira wa miguu kwa kupewa teknolojia ya kuwasaidia kuona matukio vizuri na kufanya uamuzi yanayokaribia na usahihi kamilifu, wakaadhibiwa kwa kufungiwa, kuondolewa kwenye ratiba na hata kushushwa daraja.

ZENG 03

Baadhi tuliingiwa na huruma. Tulijiuliza inakuwaje watu ambao wanatumia teknolojia ya picha za marudio za matukio yaliyoamuliwa uwanjani, wawe na ujasiri wa kuwaadhibu waamuzi ambao hawajapewa teknolojia yoyote?

Na ilifikia wakati tukahoji; inakuwaje teknolojia isiyojitosheleza ya watangazaji wa mechi za Ligi Kuu ikatumika kumkosoa refa na wakati fulani, hata kuamua matukio ambayo yalitokea wakati mchezo haujasimamishwa na pengine refa aliyaona na kwa maoni yake hayakustahili kuadhibiwa.

Mfano matukio kama ya Ibrahim Bacca wa Yanga na Jonathan Sowah wa Singida Big Stars kucheza faulo mbaya ambazo refa hakuzifanyia uamuzi halafu Kamati ya Saa 72 eti ikaenda kuwafungia mechi tano, kitu ambacho ni tofauti na kanuni kuu za mpira wa miguu zinazotaka uamuzi wa refa uwe wa mwisho na kama ni mbovu, basi refa ndio aadhibiwe?

Mamlaka zinazosimamia soka zikatekwa na mijadala hiyo iliyokosa uasili wa mpira wa miguu. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) zikaamua eti kualika waamuzi kutoka nje ya nchi kuchezesha mechi za watani wa jadi, Simba na Yanga kuthibitisha kuwa waamuzi wetu hawawezi kustahimili ukubwa wa mechi hizo.

ZENG 04

TFF, kama chombo cha kitaifa kinachosimamia maendeleo ya mpira wa miguu, hakikutakiwa kushiriki, kuunga mkono wala kutetea uamuzi wa kutumia waamuzi kutoka nje kwa sababu hiyo inamaanisha kuwa kimeshindwa kuzalisha waamuzi wenye hadhi ya kuchezesha mechi za daraja la juu nchini na hivyo hakiwezi kuzalisha waamuzi wa kuchezesha mashindano makubwa Afrika na duniani.

Kwa TPLB, hilo lingemaanisha kuwa linataka mechi zake zichezeshwe na waamuzi wenye kiwango bora bila ya kujali wanatokea wapi kwa kuwa lengo lake ni kuwa na ligi yenye klabu zenye ubora na zinazochezeshwa na waamuzi wenye ubora usio shaka.

Lakini ujio wa teknolojia ya Football Video Support (FVS), ambao unatakiwa utusaidie kupiga hatua moja mbele, umekutana na changamoto nyingine.

Teknolojia hiyo imeruhusiwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kutumika kwenye nchi ambazo kiuchumi haziwezi kumudu gharama ya matumizi ya Refa Msaidizi wa Video (V.A.R). Teknolojia ya FVS inatumia picha za marejeo za kampuni iliyopewa haki za kurusha moja kwa moja matangazo ya mechi za ligi ya nchi husika.

ZENG 05

Barani Afrika, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kutumia teknolojia hiyo. Lakini wasiwasi umeanza miongoni mwa watu walewale waliokuwa wanatuhumu waamuzi kuwa ni wabovu na wenye matokeo yao mfukoni ama wanacheza Kamari, kuwa teknolojia hiyo ina mapungufu ya uchache wa kamera.

Kwamba FVS itakuwa bora zaidi kama itatumia kamera nyingi zaidi kumuwezesha mwamuzi kupata picha halisi ya matukio na hivyo kufanya uamuzi sahihi. Hawa wamesahau kuwa kabla ya hapo walikuwa wakiwatuhumu waamuzi wetu kuwa si kitu na ni wabovu kwa kutumia teknolojia hiyohiyo ambayo leo wanaona ina mapungufu.

Walipokuwa wanakaa na kuonyesha picha za marudio za matukio ya mechi kwa kutumia idadi hiyohiyo ya kamera waliwadhalilisha waamuzi kuwa waliwezaje kuamua tofauti na kile walichokuwa wanakiona kwenye picha marudio walizozionyesha?

Inakuwaje leo waone kuwa picha walizokuwa wakizitumia kukosoa waamuzi wetu leo zina mapungufu? Wachache tulikosoa vitendo hivyo kuwa hata hizo picha za marudio wanazotumia hazikuwa na taarifa za kutosha kwa kuwa kamera zilizotumika zilikuwa chache kuweza kupata tukio kikamilifu. Lakini hawakuacha, wakaendelea kuponda uamuzi na wakafurahia pale uamuzi wa Kamati ya Saa 72 yalipolingana na mawazo yao.

ZENG 01

Iweje leo waone teknolojia ya FVS ina matatizo?

Kwa kifupi ukiangalia mwenendo wote huo unaona kuwa pengine kuna watu wanaona kuwa ni lazima waamuzi wakutwe na makosa badala ya kuzingatia masuala mazima ya maendeleo ya mpira wa miguu kwa kuzingatia kiwango cha uchumi tulicho nacho na uwezo wetu.

Ni muhimu tukakubaliana na hata kuikumbatia teknolojia tuliyonayo sasa kulingana na hali yetu ya kiuchumi na mambo mengine. Tunapokosea, kama Kamati ya Saa 72 ilivyokuwa ikijikuta katika kuamua kulingana na mhemko uliopo wakati huo, kujihoji na kujisahihisha.

Ni muhimu kwa mamlaka za soka kuzingatia utamaduni wa mpira wa miguu, miongozo yake, kanuni na sheria katika kuendesha mpira wa miguu ili usifikie wakati kama huu ambao tunaona teknolojia tuliyoamua kuitumia inatofautiana na misimamo yetu ya awali.

Tusipofanya hivyo, teknolojia inayobuniwa duniani kusaidia waamuzi kuwa sahihi, haitakuwa na maana tena kwenye soka letu na badala yake tutabakia kujiamulia mambo kulingana na utashi wa jamii yetu na si misingi ya mpira wa miguu.

Kilicholetwa na teknolojia ya FVS ni lazima kiheshimiwe na kifanyiwe kazi kwa mujibu wa miongozo yake na kazi na wajibu wa vyombo vya habari ibakie kuwa ni kutumia muda mwingi kujaribu kuelimisha wadau jinsi teknolojia husika inavyofanya kazi na kutoa ufafanuzi dhidi ya kasoro zinazojitokeza badala ya kuwa sehemu ya kasoro hizo.