ANTWI: Mghana anayeamini Simba, Yanga zitambeba Black Stars

Muktasari:
- Ni kiungo mkabaji raia wa Ghana, Samuel Antwi anayevaa jezi namba 12 kwenye kikosi hicho. Kiungo huyo alisajiliwa mwanzoni mwa msimu huu kutoka Nsoatreman ya Ligi Kuu Ghana, na alitambulishwa Julai 24, 2024.
LICHA ya kuuanza msimu huu vibaya, lakini sasa unaweza kusema amejipata baada ya kupata uhakika wa namba ili kuzima dimba la kati katika kikosi cha Pamba Jiji ya Mwanza kinachopambana kujinasua kutoshuka Ligi Kuu Bara.
Ni kiungo mkabaji raia wa Ghana, Samuel Antwi anayevaa jezi namba 12 kwenye kikosi hicho. Kiungo huyo alisajiliwa mwanzoni mwa msimu huu kutoka Nsoatreman ya Ligi Kuu Ghana, na alitambulishwa Julai 24, 2024.
Nyota huyo (22), ni miongoni mwa wachezaji wachache wa kikosi hicho tangu ujio wa Kocha Fred Felix ‘Minziro’ Oktoba 17, 2024 wamecheza mechi zote 16 huku akianza katika mechi 12 kwenye dimba la kati.
Antwi ameibuka mchezaji bora wa mechi katika michezo miwili dhidi ya Azam na Ken Gold zote zikipigwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza timu yake ikishinda zote kwa bao 1-0.
Katika mechi tatu za kwanza chini ya Minziro, Antwi alianzia benchi dhidi ya Kagera Sugar (1-0), Tabora United (1-0) na Namungo FC (1-0) kisha akaanza katika mchezo wa nne dhidi ya Fountain Gate na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 ukiwa ni ushindi wa kwanza wa Pamba kwenye ligi msimu huu.
Mchezo huo ulikuwa pia ni wa kwanza kwake kuanza katika kikosi msimu huu tangu aliposajiliwa na tangu hapo amejihakikishia nafasi ya kudumu kikosini.
Chini ya Goran Kopunovic aliyeanza na Pamba Jiji msimu huu katika mechi sita za kwanza za ligi Antwi hakuanza mchezo wowote akiishia benchi dhidi ya Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, Singida Black Stars, Azam na Mashujaa huku akikosekana dhidi ya Yanga na Coastal Union.
Baada ya kuanzia benchi dhidi ya Kagera Sugar, Tabora United na Namungo chini ya Minziro, hatimaye alianza dhidi ya Fountain Gate, Simba, Ken Gold, Moro Kids (Shirikisho), JKT Tanzania, KMC, Tanzania Prisons na Kagera Sugar (kirafiki).
Mzunguko wa pili ameanzia benchi katika mchezo mmoja dhidi ya Dodoma Jiji, na kuanza kati dhidi ya Azam FC (mchezaji bora), Coastal Union, Mashujaa FC, Singida Black Stars, Yanga na Kagera Sugar.
Kiungo huyo amezungumza na Mwananspoti kuhusu kipaji, matamanio ya kuitwa timu ya taifa ya Ghana (Black Stars) na ndoto za kuchezea Simba, Yanga na Azam akiamini ndiyo njia rahisi ya kuuza kipaji chake na hatimaye kufikiriwa kuitwa timu ya taifa.

SIMBA, YANGA NA BLACK STARS
Antwi anasema ni ngumu nchini Ghana kuitwa timu ya taifa (Black Stars) kama hauchezi katika ligi tano kubwa barani Ulaya lakini ana matumaini kuwa soka la Tanzania kwa sasa limekuwa kubwa barani Afrika na litamuwezesha kuonekana na kufikiriwa kwenye kikosi hicho.
“Kwa mfano nchini kwetu ni ngumu kama hauchezi kwenye zile ligi tano kubwa duniani hauwezi kutoboa timu ya taifa na mimi nahitaji kucheza timu ya taifa labda kama nitacheza Yanga, Simba au Azam wanaweza kuniita timu ya taifa,” anasema.
“Lakini inategemea na jinsi gani nitapambana na kufanya vizuri kwahiyo siyo rahisi na ndiyo maana nasema natamani kucheza kwenye hizi timu kubwa mbili Tanzania, na hii kwa kila mchezaji hapa Tanzania.”
Anasema wachezaji wengi wanapokwenda kucheza na Simba, Yanga ama Azam hufanya maandalizi ya ziada na hujitoa zaidi kwani ni mechi ambazo mchezaji unatakiwa uonyeshe ulichonacho bila uoga na kujitangaza.
“Unajua mechi kama hizi tunakuwa na maandalizi maalum tunayoyafanya ni mechi zinazohitaji utulivu na sisi Pamba Jiji nyumbani hatuhitaji kuwa na huruma na mpinzani yeyote kama unaweza kukimbia basi tutakimbia na wewe,” anasema.

Anaongeza kuwa; “Tulipokutana nazo Kirumba tulijaribu kuwaonyesha kwamba na sisi tuna ubora wetu, Mechi kama hizi ndiyo zile ambazo kile ulichonacho unakionyesha kwa hali na mali kwani unapocheza nao lazima uwafanye waone kile ulichonacho.”
MRITHI WA ESSIEN?
Anasema hashangazwi na namna ambavyo mashabiki nchini wameanza kuvutiwa na uwezo wake kwani hata nchini kwao Ghana wengi wanaamini ndiye mrithi wa Michael Essien, kiungo wa zamani wa Chelsea na Real Madrid, kwani ana ubora unaoweza kufikia walau kiwango cha nyota huyo.
“Ghana wananichukulia kama mtu anayeweza kuja kufikia kiwango na mafanikio ya Michael Essien, mimi kama kiungo mkabaji usikivu ndiyo silaha yangu kila wakati nafanyia kazi maelekezo,” anasema Antwi.
Anasema bidii na kujituma mazoezini ni silaha nyingine kwani hataki kuwa wa mwisho na anapenda ushindani uanzie huko.
“Unajua mpira wa miguu ni kuhusu mazoezi kama haufanyi mazoezi hauwezi kucheza soka. Naweza kusema Vinicius Jr ananivutia kwa sababu anaweza kukimbia kila sehemu kama nilivyo mimi anaweza kufanya vitu na ana moyo wa farasi,” anasema.

LIGI YA TANZANIA
Licha ya kuwa nchini kwa miezi 11, Antwi amekoshwa na ubora wa Ligi Kuu Bara akiimwagia sifa na kudai baada ya miaka 10 ijayo itakamata nafasi za juu zaidi. “Ligi ya Tanzania iko juu kwa sasa hata ukitazama takwimu imeelezwa ni ya nne kwa Afrika. Tunapocheza hapa watu wengi hususan nchi jirani na Tanzania zinatazama na hata vyombo vya habari vinaripoti kwa wingi sana,” anasema.
“Kwa sasa naweza kusema Tanzania imeipita Ghana kwani ligi ya Ghana iko kabisa shimoni na Tanzania iko juu kileleni. Na labda tujipe walau kama miaka 10 hivi tunaweza kufika namba moja au mbili kwa sababu kwa sasa wanafanya kazi nzuri.”
PAMBA JIJI
Nyota huyo anaamini mwelekeo Pamba Jiji ni sahihi baada ya usajili wa dirisha dogo na kwamba Kocha Fredy Felix ‘Minziro’ atawafikisha sehemu sahihi kwani inaonekana anaijua Ligi Kuu Bara vizuri.
Anasema katika mzunguko wa kwanza timu ilikuwa inasumbuliwa na ugeni wa ligi ikiwa na wachezaji wengi wapya waliokuwa hawaelewana na kupata muunganiko wa kitimu ili kupambana kuweka heshima, lakini kwa sasa mwelekeo ni mzuri.
“Baada ya mabadiliko ya kocha amekuja na mbinu zake na inaonekana anaijua vizuri ligi hii. Hii inatupa nguvu na kutusukuma tufanye vizuri. Na dirisha dogo akasajili wachezaji wenye uzoefu na wakubwa ikatuongezea nguvu tuliyokuwa nayo mzunguko wa kwanza,” anasema kiungo huyo.

MSIKIE MINZIRO
Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Fredy Felix ‘Minziro’ anasema wakati anajiunga katika timu hiyo alikutana na changamoto ya utimamu wa wachezaji kuwa chini akiwemo Antwi pamoja na majeraha, lakini anampongeza kwa kujituma, kufuata vyema maelekezo na juhudi mazoezini.
“Nilipokuja nilikuta tatizo la fitness (utimamu) wachezaji wanaumia kirahisi na majeraha ya mara kwa mara tulipambana kutaka washindane. Hata ukimtazama huyo Antwi ameimarika anapambana uwanjani na ana kipaji.”