Ballon d’Or; Tuzo sifa na siasa za soka
Muktasari:
- Timu za watu wanaowazunguka wagombea zilianza mikakati ya kuwapa nafasi zaidi kwenye mjadala, huku vyombo vya habari vikichochea hamasa kuhusu nani anayestahili kutwaa tuzo hiyo mwaka huu.
PARIS, UFARANSA: OUSMANE Dembele alikuwa bado hajakaa vizuri kwenye kiti chake baada ya kutwaa tuzo ya Ballon d’Or katika ukumbi wa kihistoria wa Theatre du Chatelet, jijini Paris, Septemba mwaka jana, tayari kampeni za kuwania tuzo hiyo ya mwaka 2026 zilikuwa zimeanza kushika kasi.
Timu za watu wanaowazunguka wagombea zilianza mikakati ya kuwapa nafasi zaidi kwenye mjadala, huku vyombo vya habari vikichochea hamasa kuhusu nani anayestahili kutwaa tuzo hiyo mwaka huu.
Mjadala huo umekuwa na uzito wa kipekee kwa sababu mwaka huu ni wa Kombe la Dunia, mashindano yanayoweza kubadili mwelekeo wa ushindani kwa wachezaji wanaowania tuzo hiyo. Kwa baadhi yao, suala halikuwa tu kuiongoza nchi yao kutwaa ubingwa, bali pia jinsi mafanikio hayo yanavyoweza kuongeza nafasi zao za kushinda Ballon d’Or.
Mtaalamu wa soka la Ulaya, Guillem Balague, alisema katika kipindi cha Euro Leagues cha BBC Sport kwamba Ballon d’Or imekuwa ikijadiliwa kila siku.
Alieleza kuwa mjadala huo unaakisi mwenendo wa jamii inayozidi kuweka mkazo kwa mtu mmoja mmoja, badala ya kuelewa mchango wa timu kwa ujumla.
Kwa mtazamo wake, ni rahisi kwa watu kuelewa na kujadili uwezo wa mchezaji mmoja kupiga chenga au kushindwa kufanya hivyo kuliko kutambua namna ambavyo timu nzima inavyofanya kazi kwa pamoja.
Kadiri sherehe za utoaji tuzo zilivyokaribia, ndivyo kampeni za kutafuta uungwaji mkono zilivyozidi kuongezeka.
Mwandishi wa habari za soka la Ufaransa, Julien Laurens, alionya kuwa nguvu za matangazo na mahusiano ya umma zinazotumiwa na baadhi ya klabu na wachezaji haziwezi kupuuzwa.
Makocha na wakurugenzi wa michezo nao waliingia kwenye mjadala, wakisifu wachezaji wao na kuhoji sababu za baadhi yao kukosa nafasi katika orodha ya wagombea 30 walioteuliwa kuwania tuzo hiyo.
Mkurugenzi wa michezo wa Barcelona, Deco, alielezea kutoridhishwa kwake na kutokuwamo kwa Raphinha na Pedri katika orodha hiyo, akieleza kuwa uamuzi huo ulikuwa kashfa kubwa. Hata hivyo, alimpa nafasi kubwa Lamine Yamal ya kutwaa tuzo hiyo, akisisitiza kuwa mtazamo wake haukutokana na kuwa mc hezaji wa Barcelona, bali mapenzi yake kwa soka.
Wachezaji wenyewe nao hawakuwa nyuma katika kutoa maoni yao. Yamal alisema hataki kuomba apewe tuzo hiyo, ingawa mwaka uliopita alikiri kuwa na ndoto ya kutwaa nyingi zaidi. Alisisitiza pia kuwa mshindi hapaswi kuamuliwa kwa kuangalia idadi ya mabao pekee.
Kocha wa Paris Saint-Germain, Luis Enrique, alisema amechoshwa na mjadala wa Ballon d’Or, kauli iliyokuja wakati klabu yake ikiwa na rekodi ya wachezaji 10 katika orodha ya wagombea.
Dembele na Khvicha Kvaratskhelia nao walitumia nafasi mbalimbali kupongeza uwezo wa kila mmoja. Dembele alitania kuwa wanaweza kugawana tuzo hiyo vipande viwili, kabla ya kueleza kuwa Kvaratskhelia alistahili kutokana na msimu wake bora. Kvaratskhelia naye akajibu kuwa Dembele ndiye aliyestahili.
Nchini Georgia, kampeni iliyobatizwa jina la ‘Kvara d’Or’ iliibuka kumwunga mkono Kvaratskhelia, anayependwa sana nchini humo.
Winga huyo alisema huenda mataifa makubwa yakashindwa kuelewa kikamilifu maana ya mchezaji kutoka nchi ndogo kutwaa tuzo ya kiwango hicho.
Tofauti na baadhi ya wagombea waliokuwa waangalifu katika kutoa maoni yao, mshambuliaji wa Real Madrid, Kylian Mbappe, hakuficha imani yake kuhusu uwezo wake wa kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya kwanza.
Mbappe alisema daima hujiona kuwa bora zaidi, ingawa anakubali kuwa kila mtu ana maoni yake. Aliongeza kuwa mwaka huo ungeweza kuwa mzuri kwake kushinda Ballon d’Or, lakini uamuzi wa mwisho unabaki kwa waandishi wa habari wanaopiga kura.
Tangu mwaka 2015, baada ya kuondolewa kwa mfumo uliowapa nafasi makocha na manahodha wa timu za taifa kupiga kura, mshindi wa Ballon d’Or amekuwa akiamuliwa kwa kura za waandishi wa habari.
Orodha ya wagombea 30 huandaliwa na machapisho ya France Football na L’Equipe, kisha mwandishi mmoja wa habari kutoka kila nchi kati ya nchi 100 zinazoongoza katika viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) hushiriki kupiga kura.
Kwa wakati ambao makala hii iliandikwa, muda wa kupiga kura ulikuwa umekwisha na mshindi alikuwa tayari amecha guliwa, ingawa mjadala wa nani alistahili kutwaa tuzo hiyo uliendelea kutawala.
Mtaalamu wa mikakati ya chapa katika michezo, James Kirkham, ambaye amewahi kufanya kazi na klabu na wachezaji wakubwa akiwamo Harry Kane, alifananisha kampeni za Ballon d’Or na uchaguzi.
Alisema kampeni hizo zinahusisha kutafuta wapiga kura, kujenga uungwaji mkono na kuhakikisha wagombea wanapata kura kutoka katika makundi mbalimbali ya nchi.
Hata hivyo, si kila kiongozi wa soka anayekubaliana na mfumo huo wa kampeni. Mjumbe wa bodi ya Bayern Munich anayeshughulikia masuala ya michezo, Max Eberl, aliwaunga mkono Kane na Michael Olise, lakini akasema wachezaji bora zaidi ni wale wasiopaswa kufanya kampeni ili kutambuliwa.
Jean-Pierre Papin, mshindi wa Ballon d’Or mwaka 1991, naye alikosoa namna baadhi ya wachezaji wanavyojipigia debe. Ingawa alisema anampenda Mbappe na kutambua uwezo wake wa kuvunja rekodi, alionya kuwa wakati mwingine mjadala huo hugeuka kuwa wa mchezaji kujizungumzia mwenyewe kupita kiasi.
Mbappe, hata hivyo, alitoa hoja inayogusa historia ya tuzo hiyo, akirejelea utawala wa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, ambao kwa pamoja walitwaa Ballon d’Or mara 13 ndani ya kipindi cha miaka 15, kuanzia 2008 hadi 2023.
Alisema enzi ya Messi na Ronaldo ndiyo iliyounda mtazamo wake kuhusu Ballon d’Or, akiamini kuwa tuzo hiyo inapaswa kutolewa kwa wachezaji wa kipekee, si wale wa kawaida.
Mwaka 2007, Kaka wa AC Milan ndiye aliyekuwa mshindi wa mwisho kabla ya ushindani wa muda mrefu kati ya Messi na Ronaldo kuanza kutawala tuzo hiyo.
Katika kipindi hicho, dunia ilikuwa tofauti sana na ilivyo sasa. Mitandao ya kijamii kama Facebook na Twitter ndiyo ilikuwa inaanza kupata umaarufu, Nokia ikiwa miongoni mwa kampuni zilizotawala soko la simu, huku watu wakibeba kamera za kidijitali wanapoenda matembezi.
Kufikia mwaka 2023, Messi alikuwa ametwaa Ballon d’Or kwa mara ya nane, huku teknolojia na mitandao ya kijamii vikiwa vimebadili kabisa namna mashabiki wanavyofuatilia soka na wachezaji.
Aliyekuwa mtendaji mkuu na mkurugenzi wa michezo wa AC Milan, Ariedo Braida, alisema kwa sasa kila kitu kinaenda kwa kasi kubwa sana.
Braida, aliyeshuhudia AC Milan ikizalisha washindi saba wa Ballon d’Or, kuanzia Ruud Gullit, Marco van Basten, George Weah, Andriy Shevchenko hadi Kaka, alisema mashabiki wa sasa wanaelekea kuwafuata zaidi wachezaji binafsi kuliko klabu zao.
Alifananisha hali hiyo na siasa, akieleza kuwa zamani shabiki angekuwa wa AC Milan na kwenda uwanjani kuishuhudia timu yake. Sasa, kutokana na matangazo ya moja kwa moja na Ligi ya Mabingwa Ulaya, mashabiki wanaweza kuwaona nyota wakubwa wa timu mbalimbali kwa urahisi.
Alisema mabadiliko hayo yanamfanya awe na hisia za kutamani nyakati za zamani, wakati kusubiri tukio kuliongeza hamu na msisimko ambao kwa sasa umepungua kutokana na kila kitu kupatikana papo hapo.
Utawala wa Messi na Ronaldo, pamoja na mashabiki wao wenye misimamo mikali kwenye mitandao ya kijamii, umeongeza mkazo katika rekodi binafsi za wachezaji. Hali hiyo imeathiri mashabiki, vyombo vya habari na hata wachezaji wanaokua wakiota kufikia mafanikio ya nyota hao.
Kirkham alisema kipindi cha sasa kinaweza kuwa na ushindani wa kuvutia zaidi kwa sababu kwa takribani miaka 15 mjadala wa Ballon d’Or ulitawaliwa na Messi dhidi ya Ronaldo, wakati sasa nafasi ya kutwaa tuzo hiyo imekuwa wazi zaidi kwa wagombea wengi.
Aliongeza kuwa kelele za mitandaoni hazikomi. Kila shabiki ana hamu ya kutoa maoni, kujibu hoja na kuchambua kila tukio, huku maudhui yakisambaa kutoka jukwaa moja kwenda jingine.
Bao zuri, chenga ya kuvutia au kitendo cha kiufundi vinaweza kusambaa kwa kasi, lakini vivyo hivyo maoni ya wachambuzi na mashabiki kuhusu wachezaji.
Kirkham alieleza kuwa kauli moja inayotolewa kwenye matangazo inaweza kukatwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, kujadiliwa na watengeneza maudhui, wachezaji wa zamani na wachambuzi, kisha kurejea kwenye redio na televisheni.
Kwa mtazamo wake, mzunguko huo wa maudhui katika majukwaa mbalimbali hujenga simulizi zinazoweza kumnufaisha au kumdhuru mchezaji.
Alisisitiza kuwa si lazima wanaoshiriki katika mchakato huo wawe na nia mbaya, kwa sababu kila mmoja anaweza kuwa anazalisha maudhui anayoamini kuwa yanawavutia wasikilizaji au watazamaji wake. Hata hivyo, maudhui hayo yanapoungana, huunda nguvu kubwa inayoweza kujenga au kubomoa taswira ya mchezaji.