Bandari ya Fumba kivutio kipya AFCON 2027
Muktasari:
- Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetenga Sh1 trilioni kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo. Fumba, kisiwani Unguja, ni miongoni mwa maeneo yanayofanyiwa maboresho makubwa, yakihusisha ujenzi wa uwanja wa kisasa na bandari itakayorahisisha usafiri wa wageni.
WAKATI Tanzania, Kenya na Uganda zikiendelea na maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, Zanzibar inaendelea kuimarisha miundombinu yake, huku ujenzi wa bandari katika Mji wa AFCON, Fumba, ukiwa miongoni mwa miradi inayotarajiwa kuongeza mvuto wa eneo hilo.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetenga Sh1 trilioni kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo. Fumba, kisiwani Unguja, ni miongoni mwa maeneo yanayofanyiwa maboresho makubwa, yakihusisha ujenzi wa uwanja wa kisasa na bandari itakayorahisisha usafiri wa wageni.
Bandari hiyo inajengwa kwa lengo la kurahisisha usafiri wa mashabiki watakaotumia boti kufika karibu na Uwanja wa Fumba kushuhudia mechi za AFCON. Mafundi kutoka Kampuni ya Orkum Group ya Uturuki wanaendelea na kazi ya kufukia sehemu ya bahari ili kupanua eneo la bandari na kuwezesha kupokea boti ndogo na kubwa za abiria.
Mwanaspoti ilitembelea eneo hilo kujionea maendeleo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika Mji wa AFCON, huku bandari hiyo ikiwa miongoni mwa miradi inayovutia kutokana na mchango wake unaotarajiwa katika usafiri wa mashabiki.
UWANJA WAFIKIA ASILIMIA 84
Ujenzi wa Uwanja wa Fumba, unaotarajiwa kuchukua watazamaji 36,500, umefikia asilimia 84, huku awamu ya kwanza ya mradi ikipangwa kukamilika Desemba 31, 2026.
Kampuni inayotekeleza mradi huo imeanza kufunga viti vya watazamaji, zoezi linalotarajiwa kukamilika ndani ya miezi miwili. Kuanzia Novemba 2026, pia inapanga kuweka nyasi zinazokidhi viwango vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Mbali na uwanja mkuu, mradi huo unahusisha viwanja vya mazoezi, mabwawa ya kuogelea na eneo la burudani la mashabiki (Fan Zone) lenye uwezo wa kuchukua watu 4,000. Pia, kuna sehemu maalumu kwa ajili ya watu wenye ulemavu na mahitaji mengine maalumu ili nao waweze kushuhudia mechi kwa urahisi.
MWINYI ARIDHISHWA NA MAANDALIZI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu kuelekea AFCON 2027.
Akizungumza na vyombo vya habari Ikulu Zanzibar Oktoba 3, 2026, Dk Mwinyi alisema maandalizi hayahusishi uwanja pekee, bali pia maboresho ya barabara na miundombinu mingine katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.
“Tunaridhika sana na kasi ya ujenzi wa miundombinu yote, si uwanja pekee. Barabara ukitembea hivi sasa unaona kabisa kuna mabadiliko makubwa,” alisema.
Kwa upande wake, mwakilishi wa CAF, Dk Boubakar Sidiki, alisema ziara yao ililenga kutathmini uwezo wa vituo vya afya, huduma za dharura na upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya wachezaji, viongozi na watazamaji wakati wa mashindano.
Alisema CAF imeridhishwa na maandalizi yaliyofanywa na SMZ, yakiwemo upatikanaji wa magari ya wagonjwa, kitengo cha masuala ya michezo, huduma za dharura na mashine ya MRI.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dk Riziki Pembe Juma, alisema Serikali inaendelea kufuatilia maendeleo ya mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati. Alisema kazi zinafanyika saa 24 na hatua iliyofikiwa inatia matumaini.
Dk Riziki alieleza kuwa ujenzi wa sehemu za kufunika viwanja vya mazoezi umeanza, kuanzia eneo la VIP, huku sehemu nyingine zikitarajiwa kufuatia. Alisema upanuzi wa eneo la bahari kwa ajili ya bandari ulitokana na maelekezo ya Serikali ili iweze kupokea boti kubwa na ndogo.
Aliongeza kuwa barabara zinazoelekea uwanjani zimefikia hatua nzuri, huku eneo la karibu na uwanja likiwa limekamilishiwa miundombinu hiyo.
SH1 TRILIONI ZA MAANDALIZI
Bajeti ya Sh1 trilioni kwa ajili ya maandalizi ya AFCON 2027 ilitangazwa Juni 11, 2026 na Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Juma Malik Akil, wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27 katika Baraza la Wawakilishi, Chukwani.
Kati ya fedha hizo, Sh669.754 bilioni zimeelekezwa katika utekelezaji na uwekezaji wa miundombinu na huduma mbalimbali kwa ajili ya mashindano hayo.
Serikali imesema uwekezaji huo unalenga kuboresha usafiri, miundombinu, utalii na huduma za kijamii, huku ukitarajiwa kuacha manufaa ya muda mrefu kwa wananchi.
Mradi wa Mji wa AFCON Fumba unakadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 150, sawa na Sh388.8 bilioni, ukiwa na uwanja wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 36,500 na unaolenga kukidhi viwango vya CAF.