Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DAKIKA ZA JIOOONI: Maeneo manne yameiangusha Fountain Gate

DAKIKA Pict

Muktasari:

  • Kutoka kuwa nafasi mbili za juu mwanzoni mwa msimu hadi sasa kupambana isishuke daraja, ni matokeo mabaya zaidi kwao kwani inafahamu ikiteleza kidogo tu kipindi hiki cha lala salama, itajikuta Championship.

UKIIANGALIA Fountain Gate inavyocheza na namna inavyopata matokeo katika mechi za Ligi Kuu Bara, utagundua kuna maeneo sita muhimu ambayo yanaifanya timu hiyo kuwa na shida kubwa.

Kutoka kuwa nafasi mbili za juu mwanzoni mwa msimu hadi sasa kupambana isishuke daraja, ni matokeo mabaya zaidi kwao kwani inafahamu ikiteleza kidogo tu kipindi hiki cha lala salama, itajikuta Championship.

Pengine nafasi ya kumi waliyopo sasa kabla ya Namungo haijacheza inaweza kukushangaza kwa nini timu hiyo iwe kwenye hatari ya kushuka daraja, lakini tazama pointi zake, utapata majibu.

Kwa sasa Fountain Gate ina pointi 28 baada ya kucheza mechi 26, imebakiwa na mechi nne kufahamu hatma yao huku Jumatatu hii ikiikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa.

Benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha Robert Matano na msaidizi wake, Amri Said, wana kazi kubwa ya kufanya kuinusuru. Pointi zao 28, zinawaweka rehani kwani tofauti yao na walio chini si kubwa.

DAKI 01

Ili isiwe kati ya timu mbili zitakazoshuka daraja moja kwa moja, Fountain Gate inabidi ifikishe pointi 32 sawa na kushinda mechi moja kati ya tatu ili Kagera Sugar (iliyo nafasi ya 15 ikikusanya pointi 22 hivi sasa na mechi tatu mkononi) isiwakute ikitokea ikashinda zote.

Hata hivyo, inahitajika kukaza msuli kuikimbia nafasi ya 13 na ya 14 za kucheza play off kuepuka kushuka daraja kwani ukiwa hapo, lolote linaweza kutokea. Hapa kuna uchambuzi wa maeneo yanayoiangusha timu hiyo.


KUFUNGA MABAO

Kwanza Fountain Gate haipo vizuri kwenye kufunga wala kuzuia nyavu zao zisitikiswe. Eneo hilo muhimu kwa timu inayosaka mafanikio, kwao limekuwa ni tatizo kubwa.

Kati ya timu 16, Fountain Gate ni ya pili kwa zilizoruhusu mabao mengi (47) nyuma ya KenGold (48), tofauti yao ni bao moja pekee. Ukiangalia KenGold ipo mkiani kwenye shimo la kushuka daraja, wakati Fountain wanacheza kumi bora.

DAKI 02

Ubutu wa safu ya ushambuliaji na kufungika kirahisi, kuliwafanya mabosi wa timu hiyo kuona kocha Mohamed Muya hawezi kutibu tatizo hilo, wakaachana naye Desemba 2024, kisha nafasi yake ikachukuliwa na Robert Matano ambaye naye mwendo ni uleule.

Timu ambayo iliondokewa na mshambuliaji wake Seleman Mwalimu ‘Gomez’, Januari mwaka huu, lakini hadi leo nyota huyo anabaki kuwa kileleni kwenye orodha ya wanaoongoza kwa mabao kikosini hapo, inaonyesha kuondoka kwake ilikuwa pigo kubwa.

Gomez aliondoka akiwa na mabao sita, huku bao lake la mwisho kufunga ikiwa ni Oktoba 21, 2024 dhidi ya KMC.

Tangu ameondoka na kutua Wydad ya Morocco, hakuna mchezaji aliyemzidi kwa mabao zaidi ya Elie Mokono kuyafikia ambapo hivi sasa wapo sawa.

DAKI 03

Aliyekuwa akicheza naye eneo la mbele ni Edgar William, ameonekana kushuka kiwango kwani mara ya mwisho alifunga ni Desemba 13, 2024 dhidi ya Coastal Union. Amebaki na mabao matano.

Kati ya mabao 29 waliyonayo, 23 yalipatikana duru la kwanza huku duru la pili wamefunga sita tu ambapo Elie Mokono amepachika manne na Amos Kadikilo moja, huku jingine Ladack Chasambi wa Simba akijifunga. Hiyo inaonyesha wazi bado eneo lao la mbele lina tatizo kubwa.

Wengine wenye mabao kikosini hapo ni Salum Kihimbwa (4) ambaye mara ya mwisho alifunga Desemba 25, 2024 dhidi ya Namungo. Nicholas Gyan (2) sawa na Dickson Ambundo, huku Abalkassim Suleiman aliyeondoka dirisha dogo akifunga mawili.

DAKI 04

KUTENGENEZA NAFASI

Eneo la pili lenye matatizo kwa Fountain Gate ni katika kutengeneza nafasi kwani mchezo wa soka huwezi kufunga bao bila ya kutengeneza nafasi. Uchache wao wa mabao ya kufunga, shida inaanzia hapa.

Takwimu zinaonyesha timu hiyo kinara wao wa asisti ni Salum Kihimbwa mwenye tano, anafuatiwa na Amos Kadikilo (3), waliobaki wana moja ambao ni Edgar William, Sadick Said, Seleman Mwalimu, Aron Lulambo, Hashim Kilemile, Frank Nduhije na Anack Mtambi. Jumla kikosi hicho kina asisti 15 katika mechi 26. Ukija kuangalia kinara wa asisti kwa ujumla kwenye ligi msimu huu Feisal Salum (Azam) anazo 13.

DAKI 05

KUJILINDA

Eneo la tatu lenye shida kikosini hapo ni katika kujilinda kwani wameruhusu mabao 47, huku timu hiyo katika mechi 26, ikiambulia clean sheet tatu tu. kipa namba moja wa kikosi hicho John Noble anazo mbili na Fikirini Bakari ambaye kwa sasa anacheza Tabora United, ameondoka hapo akiwa nayo moja. Takwimu hizo zinaonyesha wazi namna ambavyo eneo lao la kujilinda halipo vizuri.

Ukiachana na hilo, timu hiyo imeingia kwenye orodha ya waliojifunga msimu huu kupitia Jackson Shiga aliyefanya hivyo Desemba 29, 2024 wakati Fountain Gate ikichapwa 5-0 na Yanga.

Matatizo ya kujilinda yameendelea kuwatesa Fountain Gate kwani timu hiyo hadi sasa imeruhusu kupigiwa penalti 12, huku yenyewe ikipiga nne pekee.


NIDHAMU YA UCHEZAJI

Jambo la mwisho ni nidhamu ya uchezaji haipo vizuri kwao kwani ukiweka kando kujifunga, pia hadi sasa wana kadi nyekundu mbili walizoonyeshwa Abalkassim Suleiman katika mchezo dhidi ya Pamba Jiji katika duru la kwanza, pia John Noble dhidi ya Simba, duru la pili.

Kufuatia hayo yote, kocha Matano amekiri kuna shida hiyo kikosini kwake na amekuwa akiifanyia kazi kila eneo kwa wakati wake.

“Timu yangu ina makosa mengi katika safu ya ulinzi, nina kazi kubwa kuhakikisha nayapunguza, bora timu isifunge lakini pia isiruhusu mabao.

“Kwa upande wetu tumekuwa tukifungwa zaidi ya kufunga, hili ni tatizo kubwa, bado tuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi zilizobaki ili kuinusuru timu.”