Prime
SIO ZENGWE: Prince Dube anamjua sana mtu wa tatu

Muktasari:
- Mshambuliaji mwenye sifa ya uchoyo hujaribu kupiga shuti langoni kana mpira unaweza kumtoboa mchezaji na kupenya hadi kwenye nyavu.
MOJA ya sifa kubwa ya washambuliaji ni uchoyo au ubinafsi wanapopata mipira mbele ya lango. Awe amelipa mgongo goli, awe pembeni sana ya goli au awe amezingwa na mabeki wa timu pinzani.
Mshambuliaji mwenye sifa ya uchoyo hujaribu kupiga shuti langoni kana mpira unaweza kumtoboa mchezaji na kupenya hadi kwenye nyavu.
Wanapofanikiwa kupitisha mipira kutoka pembeni, mbele ya mabeki au anapogeuka haraka na kupiga shuti na kufanikiwa kufunga bao, mshambuliaji huyo huonekana bora na idadi yake ya mabao huongezeka.
Washambuliaji aun wachezaji wenzake ambao hunyimwa pasi na mshambuliaji mchoyo, husubiri akosee ndipo humwambia; "Mbona nilikuwa na nafasi nzuri tu ya kufunga?" Lakini anapofanikiwa kufunga, huungana naye kushangilia huku mioyo ikisononeka na uchoyo wa mwenzao.

Hii sifa ya uchoyo ni kwa washambuliaji wengi duniani, hata wale nyota kama kina Ronaldo, lakini pengine Mungu amemnyima hiki kitu mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube.
Pamoja na ukweli anaongoza kwa ufungaji, akiwa amefunga mabao 12, bado Dube amefanya kazi kubwa ya kusaidia wenzake kufunga mabao, akijigeuza ukuta wa kugongeshea mpira kwenda kwa wachezaji wengine walio katika nafasi nzuri zaidi ya kufunga.
Pengine sifa hiyo ya kukosa uchoyo inaweza kujionyesha zaidi katika mechi ambayo Yanga iliishinda Simba kwa bao 1-0, bao lililofungwa na Maxi Nzengeli.
Baada ya Yanga kupiga pasi nyingi za kutaka kuifungua ngome ya Simba na kuonekana kama isingewezekana, kiungo Pacome Zouzoua aliamua kupitishia mpira katikati ya ngome. Aliburuza pasi hadi kwa Dube aliyekuwa amelipa mgongo goli.
Wakati mpira ukienda kwa mshambuliaji huyo, Nzengeli alikuwa kama anaukimbiza na Dube alikuwa ameshamwona.

Alichokifanya mshambuliaji huyo Mzimbabwe ni kumwekea mpira Nzengeli katika njia aliyokuwa akipita na Mcongo huyo hakufanya ziada zaidi ya kuusogeza mbele kidogo na kuachia kiki ya mguu wa kushoto kufunga bao hilo pekee.
Alikuwa amemuona mtu wa tatu aliyekuwa anakimbia akitarajia anaweza kupewa mpira wakati wowote. Hiyo ndio sifa kubwa ya Dube katikati ya safu ya ushambuliaji ya Yanga.
Huwa hana shughuli nyingi na mpira wakati anapoupokea akiwa karibu na lango. Kazi yake kubwa huwa ni kuangalia nani anafanya mikimbio kuelekea golini au anayejiweka katika nafasi nzuri ya kufunga.
Katika mechi dhidi ya Stand United, Dube alitoa pasi kadhaa kwa mtu wa tatu, lakini hazikuweza kugeuzwa kuwa mabao. Alitoka uwanjani akiwa hajafunga bao, huku pasi zake za mabao zikiwa zimepotezwa na wenzake, lakini ngome ya Stand ilijua ilifanya kazi gani kubwa. Yanga ilishinda kwa mabao 8-1 baada ya Clatous Chama na Stephane Aziz Ki kutumia pasi hizo za mtu wa tatu kufunga mabao sita baina yao.

Pengine uwezo wa Dube kumuona mtu wa tatu mbele ya lango ndio umeifanya Yanga kufunga mabao mengi kupitia katikati, badala ya ile ya kutumia krosi. Hata mabao yanayotokana na krosi, huwa ni zile ambazo hazitoki pembeni kabisa ya uwanja (half space). Mara nyingi hutokea nje kidogo ya eneo la penalti na katika krosi hizo nyingi, Dube amefunga mabao sita ya kichwa.
Kutokana na mtindo wa timu nyingi kujaza wachezaji wengi nyuma zinapokutana na klabu kubwa, njia nzuri za kupata mabao ni kutumia krosi, mipira ya adhabu na kupenyeza mpira katikati ili kuichana ngome.
Yanga imeamua kutumia njia ya kupitisha mipira kwenye kiini cha ngome na Prince Dube anaonekana kuwa ndiye mtu sahihi kufanikisha mbinu hiyo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kumuona mchezaji wa tatu, pia kutoroka mabeki wa kati wanapokuwa wamejisahau kwa kukodolea macho mpira badala ya kuchunga wachezaji.
Ustadi wake hauko katika kumuona mtu wa tatu pekee, bali pia katika kutoa pasi muhimu za kusababisha kupata bao.

Si ajabu kwa ujanja huo, Dube ndiye mchezaji anayeongoza kwa kuhusika katika mabao mengi, huku pia akitoa pasi za mwisho na kutimiza wajibu wake wa kwanza kama mshambuliaji wa kufunga mabao.
Amehusika katika mabao 29, akiwa amefunga mabao 12 na hivyo kuongoza orodha ya wafungaji pamoja na Jean Ahoua wa Simba. Ametoa pasi nane za mwisho na hivyo kushika nafasi ya pili pamona na Nzangeli na Pacome, wote wakiwa nyuma ya Feisal Salum 'Fei Toto' anayeongoza kwa kutoa pasi 13.
Pamoja na mshambuliaji Kennedy Musonda kuonyesha ufanisi katika umaliziaji kila mara anapopewa nafasi, Kocha Miloud Hamdi anaonekana kumchagua Dube ndiye mshambuliaji wa kwanza.
Na pengine sifa hiyo ya kumjua zaidi mtu wa tatu ndio inayomfanya Hamdi aendelee kumtegemea Mzimbabwe huyo kuongoza mshambulizi ya kikosi chake ambacho kina wachezaji watatu katika orodhab ya wafungaji kumi bora hadi sasa ambao wamefunga mabao kuanzia nane hadi 12.