Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DAKIKA ZA JIOOONI: Mshale wa saa unavyoikimbiza KenGold Championship

JIONI Pict

Muktasari:

  • Hilo ndilo linawakuta KenGold, timu ambayo imepanda daraja msimu huu kushiriki Ligi Kuu Bara na sasa ndiyo ipo karibu zaidi kushuka kutokana na hesabu kuwa ngumu kwao.

KATIKA mchezo wa soka, wanasema kosea mambo yote, lakini hakikisha timu inafanya usajili wa maana kwani ukikosea hapo tu, majuto yake ni makubwa zaidi.

Hilo ndilo linawakuta KenGold, timu ambayo imepanda daraja msimu huu kushiriki Ligi Kuu Bara na sasa ndiyo ipo karibu zaidi kushuka kutokana na hesabu kuwa ngumu kwao.

KenGold ambayo awali ilijukana kwa jina la Gipco FC iliyokuwa na maskani yake mkoani Geita, ilibadilishwa jina baada ya pande mbili kufikia makubaliano ya kibiashara na kuhamishiwa wilayani Chunya, mkoani Mbeya.

Hata hivyo, katika Championship ilidumu misimu minne ikiwa nafasi tano za juu na msimu uliopita ilimaliza kinara wa ligi, huku ikiweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa jumla kwenye michuano hiyo.

Timu hiyo inayomilikiwa na mdau wa michezo na mwekezaji kwenye sekta tofauti ikiwa ni Elimu na Madini, haijawa na matokeo mazuri tangu ianze msimu huu na kuwa kwenye presha ya kushuka daraja.

Kwa sasa kila mshale wa saa unavyosogea, siku za KenGold kwenda Championship nazo zinasogea.

Kwa sasa KenGold ipo mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 16, imebakiwa na mechi nne zenye jumla ya pointi 12, endapo ikishinda zote itamaliza ligi na pointi 28 ambazo angalau zitawaweka juu na kuepuka kushuka daraja.

Hata hivyo, ikiwa tofauti hata kwa kupoteza mchezo mmoja tu kati ya minne iliyobaki, basi matumaini ya kubaki ligi kuu yatakuwa madogo sana.

Ikitokea ikapoteza mechi mbili mfululizo zijazo, basi moja kwa moja itakuwa imeshuka daraja kwani haitaweza tena kufikisha pointi 24 ilizonazo Tanzania Prisons kwa sasa inayoshika bnafasi ya 14.

Ratiba waliyonayo, ndiyo inaifanya KenGold kutabiriwa kuwa timu ya kwanza kushuka daraja kwani kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Tanzania Prisons, kimezidi kuwachimbia shimo.

Mchezo ujao, KenGold itakuwa jijini Tanga kucheza dhidi ya Coastal Union, kisha itarudi nyumbani kukabiliana na Pamba Jiji na Simba, itamaliza msimu ugenini kwa Namungo.

Mechi hizo nne, inacheza dhidi ya timu tatu zinazopambana kuweka mambo sawa zisishuke daraja ambazo ni Coastal Union, Pamba Jiji na Namungo, huku moja ambayo ni Simba inawania ubingwa.

Hiyo inaifanya KenGold ambayo imeshinda mechi tatu pekee kwenye ligi msimu huu kati ya 26 ilizocheza kuwa na maswali mengi ya kujiuliza.

Kati ya timu mbiil ambazo zitashuka daraja moja kwa moja, KenGold inaonekana kuwa na nafasi moja kati ya hizo.

JIO 04

USAJILI TATIZO

Tatizo kubwa la timu hii ilianzia mwanzoni mwa msimu kwenye usajili baada ya kuwapa nafasi wachezaji wengi ambao hawakuwa na uzoefu wa Ligi Kuu ikiamini wanaweza kufanya kitu.

Matumaini ilikuwa ni vijana hao walioaminiwa iwapo watafanya vizuri, timu inufaike nao kibiashara lakini mambo yalionekana kuwa magumu hadi dirisha dogo lilipofunguliwa.

Katika kikosi kilichoanza msimu na timu hiyo ilikuwa ni wachache waliokuwa wamewahi kucheza Ligi Kuu ikiwa ni James Msuva, Helbert Lukindo, Charles Masai na Emanuel Mpuka.

Aidha timu hiyo ilianza msimu chini ya Kocha Fikiri Elias, baadaye aliamua kung’atuka kutokana na mwenendo wa matokeo yasiyoridhisha, ndipo Omary Kapilima akashika mikoba yake.

Dirisha dogo lilipofunguliwa Desemba 15, 2024, mabosi waliamua kuweka fedha mezani na kuongeza baadhi ya mastaa wa ndani na nje na hata hivyo, hali haijawa nzuri ndani ya uwanja.

Baadhi ya wachezaji walioongezwa ili kuleta mabadiliko ni Benard Morison, Ernaes Morison, Zawadi Mauya, Kelvin Yondani, Seleman Bwenzi na Obrey Chirwa.

Pamoja na usajili huo ambao kwa kiasi fulani ulitikisa nje ya uwanja, lakini ishu ya matokeo yamebaki yakiumiza vichwa vya wadau na mashabiki wa timu hiyo.

Kama haitoshi, vigogo wa timu hiyo waliamua kusaka kocha mkuu na kumnasa Vladslav Heric raia wa Serbia ambaye alikutana na kikwazo cha kibali na changamoto ya kozi refresha.

Timu hiyo hadi inamaliza duru la kwanza, ilikuwa ipo mkiani na pointi sita, nafasi hiyo imeendelea kuishikilia huku ikibadilika kwenye kukusanya pointi tu kwani hadi sasa imeongeza 10 na kufanya kuwa nazo 16 ikibakiwa na mechi nne.

JIO 05

HAWA ANGALAU

Miongoni mwa nyota wanaoonesha kiwango bora na kuonekana kuwa nguzo kubwa kikosinihapo ni Lukindo, Daud Mishamo na Seleman Bwenzi ambao kwa kiasi kikubwa wamejituma.

Kabla ya dirisha dogo, Lukindo aliyewahi kutesa na Mbao na Biashara United, ndiye alikuwa tegemeo zaidi kikosini japokuwa baadaye aliongezewa nguvu eneo lake kwa kuletwa Bwenzi.

Kwa upande wa Mishamo aliyefunga mabao matano hadi sasa sawa na Bwenzi, ndiye aliipandisha timu hiyo akiwa na maelewano na aliyekuwa mwenzake, William Edgar aliyetimkia Fountain Gate mwanzoni mwa msimu.

Bwenzi, Lukindo na Mishamo wote wamefunga jumla ya mabao 13 kati ya 21 yaliyofungwa na timu nzima, pia wamehusika katika mengine manne, licha ya timu kutokuwa na matokeo mazuri, wakati timu ikienda kushuka, huenda msimu ujao nyota hao wakapata dili timu zingine za ligi kuu.

Kwa sasa Bwenzi ndiye ameachiwa msala kutokana na kiwango bora alichonacho, huku akikumbukwa zaidi kwa bao alilofunga katikati ya uwanja kwenye kipigo cha 6-1 dhidi ya Yanga.

Bwenzi katika michezo kumi aliyocheza amefunga mabao matano akihusika na mengine mawili, huku akiweka rekodi ya kufululiza kufunga mabao kwenye michezo minne mfululizo.

JIO 01

REKODI YA CHAMPIONSHIP

KenGold ambayo ilitabiriwa kufanya makubwa kutokana na matokeo yake ya Championship, hali imekuwa tofauti ikionekana kushindwa kufurukuta kwenye Ligi Kuu.

Ikiwa Championship ilimaliza msimu ikiwa na pointi 70 ikifunga mabao 33, huku ikipoteza mechi nne tu dhidi ya Pamba Jiji 2-1, Mbeya Kwanza 1-0, Transit Camp 1-0 na Mbuni FC 2-1.

Katika mechi 30 ilizocheza, ilishinda 17, sare tisa na kupoteza nne huku ikiwa ndiyo timu iliyoshinda idadi kubwa ya michezo ya nyumbani na ugenini ikilinganishwa na nyingine.

JIO 02

MSIKIE KAPILIMA

Kocha mkuu wa timu hiyo, Omary Kapilima anasema michezo minne iliyobaki ni kufa au kupona katika kupambania nafasi ya kubaki Ligi Kuu, huku akitoa matumaini kuwa hawashuki daraja.

Anasema licha ya matokeo waliyonayo, lakini anafurahishwa na kuridhishwa na kiwango cha wachezaji, akieleza kuwa morali waliyonayo wanaweza kubadili upepo wa matokeo.

“Tunazo mechi za jasho na damu, kipekee nipongeze vijana namna wanavyopambana ukiachana na matokeo ya jumla, tunaenda kufa au kupona hii lala salama,” anasema Kapilima.

Kocha huyo anabainisha yapo makosa wanayofanya hasa eneo la ulinzi kwa kukubali kuruhusu bao kila mchezo, hali ambayo anataka kuimaliza, huku akitaka ushindi kila mechi iliyobaki.

Anaeleza kuwa pamoja na matokeo hayo, anaridhishwa na mwenendo wa vijana wake kwa namna wanavyopambana licha ya kile kinachopatikana na wanaweza kushangaza.

“Vijana hawajapoa, tunaendelea kupambania kilicho mbele yetu na hatuwezi kufa moyo kwakuwa mpira una matokeo yake, walio juu yetu hawajatuacha sana,” anasema kocha huyo.

JIO 03

WADAU WATOFAUTIANA

Wakati Chama cha Soka Mbeya (Mrefa) kikitoa matumaini kuinusuru timu hiyo, baadhi ya wadau na mashabiki wametofautina mtazamo wakieleza KenGold inashuka daraja huku wengine wakidai muda bado.

Mwenyekiti mpya wa chama hicho, Elias Mwanjala anasema baada ya kurejea madarakani mkakati wa kwanza ni kupambania timu hiyo na Tanzania Prisons kubaki Ligi Kuu.

Pia anaitaja Mbeya City ambayo ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Championship kwa pointi 56 kuhakikisha inarejea Ligi Kuu baada ya kushuka misimu miwili nyuma.

“Huko nyuma tulikuwa na timu nne Ligi Kuu, baada ya uongozi uliomaliza muda wake tukashusha hadi kubaki mbili, lazima tupambane hizi mbili zibaki salama na Mbeya City ipande tena,” anasema Mwanjala.

Jumanne John, mdau wa soka Mbeya anasema KenGold hesabu zimeshakufa kwani mechi alizonazo hakuna namna ya kutoboa akieleza kwa sasa ni bora kujipanga upya na Championship.

“Baada ya mechi na Prisons, atamfuata Coastal Union, kisha kumkaribisha Pamba Jiji na Simba, atahitimishia hesabu ugenini dhidi ya Namungo, hapo utaona ugumu wake kutoboa,” anasema John.

Mchambuzi wa soka jijini Mbeya, Linah Mwambene anasema licha ya ugumu walionao KenGold, lakini iwapo itashinda mechi zote inaweza kubadili upepo.

“Wanaweza kuangukia play off ambayo kimsingi haina mwenyewe, itategemea namna wanavyojipanga na hizo mechi kuona wanamalizaje ili kujua hatma yao,” anasema Linah.