Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dakika za jioooni: Tanzania Prisons presha tupu

DAKIKa Pict

Muktasari:

  • Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza Tanzania, haijawa na matokeo mazuri ikiwa katika nafasi ya 14 kwa pointi 24, ikibakiwa na mechi nne za kuamua hatma ya ushiriki wa Ligi Kuu msimu ujao.

PRESHA inazidi kupanda na kushuka kwa Tanzania Prisons kutokana na matokeo iliyonayo katika Ligi Kuu Bara, huku ikitahadharishwa kutojirudia yaliyotokea msimu wa 2010/11 na 2021/22.

Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza Tanzania, haijawa na matokeo mazuri ikiwa katika nafasi ya 14 kwa pointi 24, ikibakiwa na mechi nne za kuamua hatma ya ushiriki wa Ligi Kuu msimu ujao.

Katika mechi hizo, itacheza tatu mfululizo nyumbani dhidi ya JKT Tanzania, Coastal Union na Yanga kisha kumaliza ratiba ya msimu dhidi ya Singida Black Stars ugenini.

Maafande hao wenye kumbukumbu ya kushuka daraja msimu wa 2010/11 kisha kurejea 2011/12, kwa sasa wana presha wakiwa katika harakati za kukwepa kushuka daraja.

Kama haitoshi, msimu wa 2021/22 timu hiyo ilijikuta ikiponea chupuchupu kushuka daraja baada ya kumaliza Ligi katika nafasi ya 14 na kuangukia kujiokoa kwa play off.

DAKI 01

Katika mchujo huo ilishinda kwa jumla ya mabao 2-1 dhidi ya JKT Tanzania, huku kipa Edward Mwakyusa akiibuka shujaa kwa kuokoa hatari kadhaa na kupewa ajira kikosini humo ikiwa ni shukrani kutoka kwa mabosi wa Jeshi la Magereza.


MISIMU MITANO

Historia ya mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Muungano 1999, katika Ligi Kuu haishtui sana kwa mwenendo wake licha ya kwamba mechi sita za mwisho zimekuwa zikiipa wakati mgumu kutoboa hadi kusubiri huruma dakika za mwisho.

Katika misimu mitano imekuwa ikimaliza kwa hekaheka, ambapo 2018/19 ilimaliza nafasi ya 12 kwa pointi 46 na 2019/20 nafasi ya 10 kwa alama 49.

Msimu wa 2020/21 timu hiyo ilimaliza katika nafasi ya saba kwa pointi 44, huku 2021/22 ikimaliza nafasi ya 14 kwa pointi 29 na kucheza play off, 2022/23 ikamaliza nafasi ya nane kwa alama 37 na 2023/24 nafasi ya tisa kwa pointi 34.

Kwa sasa ipo nafasi ya 14 kwa pointi 24, ambapo jasho limeonekana kuwatoka wengi wakifikiria kushuka daraja inaweza kuwatoa kwenye heshima iliyonayo kwa wadau na mashabiki jijini Mbeya.

DAKI 02

HESABU ZILIVYO

Maafande hao wanapigia hesabu michezo minne iliyobaki kutopoteza hata mmoja, wakianza na JKT Tanzania Aprili 18 kupigania ushindi ili kujiweka pazuri.

Kwa sasa wadau na mashabiki wa timu hiyo pamoja na uongozi wa juu wameonyesha kuwa na ushirikiano wakiongozwa na Chama cha Soka Mbeya (Mrefa) kuhakikisha anayefika Sokoine anaacha alama tatu.

Ilishuhudiwa kikao kizito usiku wa Aprili 4, 2025 vigogo wa timu hiyo chini ya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza nchini, Kenneth Mwambije wakieleza mwelekeo mpya wa timu hiyo kwa wadau jijini Mbeya.

Katika kikao hicho kilichohusisha viongozi wa dini, mila, mashabiki na wadau mbalimbali waliazimia kila mchezo kwa sasa ni kushinda, ambapo tayari matokeo yameanza kuonekana.

Kabla ya kikao hicho, timu hiyo ilikuwa na michezo sita, miwili tayari imechezwa na kushinda yote dhidi ya Kagera Sugar 1-0 na KenGold 3-1, imetoka nafasi ya 15 kwenye mstari mwekundu wa kushuka daraja hadi 14, eneo la play off.

Hadi sasa maazimio ni kuona mchezo ujao na JKT Tanzania timu hiyo ikishinda sawa na Coastal Union, Yanga na kisha kumalizia hesabu huko Liti mkoani Singida.

DAKI 03

TATIZO LIPO HAPA

Tanzania Prisons imekuwa ikihangaika na matokeo kuanzia mwanzo wa msimu muda mwingine hadi mwisho wa msimu kutokana na masuala ya kiutawala.

Ikumbukwe timu hii ina makazi yake Ruanda jijini Mbeya, lakini sehemu ya maamuzi ya mwisho ni jijini Dodoma, jambo ambalo huipa wakati mgumu inapotokea uhitaji wa msaada wa haraka.

Pamoja na kwamba timu hiyo hupewa watu majukumu ikiwamo Katibu, Mwenyekiti, Mlezi na Meneja, lakini asilimia kubwa huwa hawana uamuzi, zaidi ya kusubiri makao makuu Dodoma.

Hali hiyo huupa ugumu uongozi unaokuwa sambamba na wachezaji haswa wakati wa usajili, ambapo mapendekezo yote hutumwa Dodoma kwa ajili ya utekelezaji na muda mwingine mengine huachwa.

Aidha, mabadiliko ya mara kwa mara kwa uongozi wa benchi la ufundi ikiwa ni makocha na ‘staff’ wake hali inayowapa wakati mgumu kufanya vizuri kutokana na kukosa uhuru wa moja kwa moja.

Kwa takribani miaka mitatu wamebadilishwa makatibu wanne ikiwa ni Ajabu Kifukwe aliyeondoshwa na kurejeshwa kisha kuondoshwa tena, Faisal Hau, Ally Mrisho na sasa John Matei.

Kama haitoshi, Tanzania Prisons huathiriwa na mambo mawili ikiwa ni usajili usio wa ushindani ikilinganishwa na timu nyingine.

Asilimia kubwa ya wachezaji wanaosajiliwa huwa ni wa kiwango cha chini na kati, lakini kubwa zaidi viwango vya dau huwa ni vidogo na wachezaji wengi wenye ubora huamua kutimka.

DAKI 04

WABEBA TIMU

Pamoja na kusuasua kwa matokeo kwa sasa, lakini wapo baadhi ya wachezaji wanaoonyesha kiwango bora kuipambania timu hiyo kujinasua na janga iliyonayo.

Miongoni mwa mastaa wafia timu ni Beno Ngassa mwenye mabao manne na asisti nne huku akiwa na tuzo mbili za mchezaji bora wa mechi.

Nyota huyo ambaye ni ndugu wa damu na staa wa zamani wa Taifa Stars na Yanga, Mrisho Ngassa, amekuwa mhimili mkubwa kikosini kwa makocha wote wanaotua Prisons akiwa na uhakika wa namba.

Pia mkongwe, Jumanne Elfadhil ni sehemu ya wachezaji tegemeo zaidi haswa eneo la beki na baada ya kutemwa kikosini dirisha dogo na kupangiwa kazi nyingine jeshini pengo lake lilikuwa kubwa.

Katika michezo minane aliyokosa, timu ilipoteza sita, ushindi mmoja sawa na sare na kuwa nafasi mbili za mkiani, aliporejea mechi mbili timu imeshinda zote wakiruhusu bao moja.


KOCHA KICHEKO

Kocha mkuu wa timu hiyo, Aman Josiah anasema anaridhishwa na ubora wa nyota wake haswa morali iliyopo ndani ya uwanja akiomba sapoti zaidi kwa wadau na mashabiki.

Anasema licha ya kuwa yeye ni kocha lakini hana uwezo wa moja kwa moja kuinusuru timu kama hatapata nguvu ya nje ya uwanja, huku akishukuru ushirikiano uliopo kwa sasa.

“Vijana wanajituma kila mechi hata zile tulizopoteza si kwa sababu ya uwezo mdogo bali ni maamuzi ya wengine, kiujumla mkakati ni kuona tunabaki Ligi Kuu bila kucheza hata play off,” anasema Josiah.