Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hiki kimechangia kifo cha straika Tenerife

DOKTA Pict

Muktasari:

  • Kipa Jesus Owono alipanda hadi karibu na katikati ya uwanja kujaribu kuokoa hatari, ndipo goti lake lilipotua kifuani mwa De Miguel akiwa katika mwendo wa kasi. Wachezaji wote wawili walikuwa katika mwendo wa kasi, hivyo kusababisha mgongano mkubwa ambao ulisababisha majeraha mabaya yaliyosababisha kifo cha De Miguel.

WIKI iliyopita, mnamo Novemba 3, 2026, medani ya soka ilishuhudia tukio baya la ajali iliyotokea nchini Hispania katika Ligi Daraja la Pili, iliyosababisha kifo cha mshambuliaji wa CD Tenerife, Jesus de Miguel, baada ya kugongana na kipa wa klabu ya FC Andorra.

Kipa Jesus Owono alipanda hadi karibu na katikati ya uwanja kujaribu kuokoa hatari, ndipo goti lake lilipotua kifuani mwa De Miguel akiwa katika mwendo wa kasi. Wachezaji wote wawili walikuwa katika mwendo wa kasi, hivyo kusababisha mgongano mkubwa ambao ulisababisha majeraha mabaya yaliyosababisha kifo cha De Miguel.

Mwamuzi alimpa kipa huyo kadi nyekundu ya moja kwa moja, huku mchezaji aliyeumia akilazimika kupewa huduma ya dharura ya ufufuaji wa moyo na mapafu, inayojulikana kama Cardiopulmonary Resuscitation (CPR), kwa dakika kadhaa hapo hapo uwanjani.

Tukio hilo lililazimisha La Liga kutoa heshima maalumu kwa familia ya De Miguel katika kila mechi za ligi zilizochezwa kuanzia Ijumaa, Jumamosi na Jumapili, kwa kusimama na kumkumbuka mwanasoka huyo.

Kama ulipata bahati ya kutazama mechi kali ya Jumapili ya La Liga kati ya Barcelona na Atletico Madrid, mchezo huo ulisimama kwa dakika tatu kumkumbuka De Miguel. Pia, kwenye luninga kulikuwa na msimbo wa QR ambao uliwapa watazamaji nafasi ya kuusoma kwa kutumia simu janja na kuchangia chochote.

DOKT 01

Kwa mujibu wa jopo la madaktari wabobezi wa moyo, mshambuliaji huyo aligongwa na goti la kipa huyo kifuani, hali iliyosababisha moyo kusimama ghafla. Hii ni hali ambayo moyo huacha kufanya kazi ya kusukuma damu na oksijeni mwilini.

Kwa kawaida, moyo una misuli inayopata lishe kupitia damu na huweza kufanya kazi yake kwa misuli hiyo kukunjuka na kusinyaa. Kutokea kwa dosari yoyote au kujeruhiwa kunaweza kuchangia moyo kusimama.

Dalili na viashiria vya hali hiyo ni kuanguka ghafla na kupoteza fahamu, kushindwa kupumua vizuri, kutapatapa na kuweweseka. Kwa kisa cha De Miguel, baada ya kugongwa kifuani alidondoka na kupoteza fahamu.

Moyo kusimama ghafla ni tatizo la dharura linalohitaji hatua za haraka za huduma ya kwanza, ikiwamo ubonyezaji wa kifua kupitia CPR, ili kusaidia kurejesha mapigo ya moyo na utendaji wa mapafu. Huduma hiyo ilitolewa hapo hapo uwanjani kama hatua ya kwanza ya dharura ya kuokoa maisha, lakini kwa bahati mbaya haikuweza kufanikiwa kumwokoa.

DOKT 02

Sababu kuu ya huduma ya kwanza viwanjani ni kuzuia kifo, kuzuia madhara makubwa na kutoa huduma za awali kabla ya mgonjwa kupelekwa kupata matibabu ya kiwango cha juu. Ndiyo maana viwanja vyote vinapaswa kuwa na huduma ya kwanza na gari la wagonjwa.

Leo, jicho la kitabibu litaangazia tatizo la moyo kusimama ghafla, kitaalamu Cardiac Arrest, na namna hali hiyo inavyoweza kusababisha kifo.

Kusimama kwa moyo ni hali ambayo moyo huacha kusukuma damu na oksijeni kwenda kwenye ubongo, viungo na tishu nyingine za mwili. Wakati mwingine mtu anaweza kuzinduka baada ya moyo kusimama endapo matibabu ya kufufua moyo yataanza mara moja.

Hata hivyo, kadiri muda unavyopita bila damu kusukumwa kwenye ubongo, ndivyo uwezekano wa mtu huyo kuzinduka unavyopungua. Pia, endapo atazinduka, uwezekano wa kupata uharibifu wa kudumu wa ubongo huongezeka.

DOKT 03

Uharibifu wa ubongo unaweza kutokea endapo moyo utasimama kwa zaidi ya dakika tano bila mtu kupata huduma ya kwanza ya ufufuaji wa moyo na mapafu, kwa kifupi CPR. Huduma hiyo husaidia kusukuma damu yenye oksijeni kutoka moyoni na mapafuni hadi kwenye ubongo na viungo vingine.

Kwa kawaida, kifo kinaweza kutokea ikiwa moyo utasimama kwa zaidi ya dakika nane bila huduma ya ufufuaji wa moyo na mapafu, yaani CPR. Hivyo basi, huduma hii lazima ianze haraka iwezekanavyo na inapaswa kutolewa na watu wenye ujuzi wa CPR.

Kusimama kwa moyo kunaweza kusababishwa na kitu chochote kinachofanya moyo usidunde sawasawa. Ukiacha sababu ya ajali kama ya De Miguel, sababu moja ya kawaida, hasa kwa watu wazima, ni mdundo usio wa kawaida wa moyo, kitaalamu arrhythmia.

Sababu nyingine inayoweza kusababisha hali hiyo ni kusimama kwa upumuaji, kama vile mtu anapozama majini au anapopata maambukizi makali ya mapafu, kitaalamu pneumonia, au shambulio kali la pumu.

DOKT 04

Mtu mwenye tatizo la moyo kusimama ghafla hupoteza fahamu, huwa tuli, hushindwa kujibu maswali wala kuonesha mwitikio. Mtu huyo anaweza asiwe anapumua kabisa au akawa na pumzi zisizo za kawaida.

Zaidi ya theluthi mbili ya matukio yote ya moyo kusimama ghafla hutokea nyumbani. Kwa hiyo, ni muhimu kwa watu kujifunza kutambua hali hiyo kwa rafiki au mwanafamilia ambaye hajibu anapoitwa na hapumui, au anapumua kwa njia isiyo ya kawaida.

Mtu huyo anaweza kuwa amepatwa na tatizo la moyo kusimama ghafla na anahitaji huduma ya kwanza ya haraka ya CPR pamoja na kuwasiliana na huduma za matibabu ya dharura katika eneo husika.


SABABU YA KIFO INAWEZA KUWA HII

Kupigwa na kitu kizito kifuani kunaweza kusababisha majeraha makubwa ndani ya kifua, ikiwamo kwenye tishu za moyo na mishipa ya damu iliyo karibu na moyo. Pia, kunaweza kusababisha mwili kupata mshtuko, kitaalamu shock.

Kwa kisa cha De Miguel, inawezekana kuwa ndani kwa ndani alipoteza damu nyingi, hali iliyosababisha moyo kusimama ghafla. Vilevile, tukio hilo linaweza kusababisha dosari katika mfumo wa umeme wa moyo na hatimaye moyo kusimama ghafla.