IMEKUWAJE? Arsenal msimu huu haifungi kona
Muktasari:
- Msimu uliopita Arsenal ilitwaa ubingwa wa ligi baada ya miaka 22. Mafanikio hayo yalijengwa kwa ulinzi imara, kikosi chenye uwezo na matumizi ya tofauti ndogo zinazoweza kuamua mechi. Hakuna eneo lililoonyesha hilo zaidi ya mipira iliyokufa.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL ilivunja rekodi ya Ligi Kuu England kwa kufunga mabao mengi kupitia mipira ya kona msimu uliopita. Hata hivyo, baada ya mechi nane za utetezi wa taji lake msimu huu, bado haijafunga bao hata moja kupitia kona.
Ni nini kinaendelea kwa timu iliyokuwa mahiri katika mipira iliyokufa? Hilo ni swali muhimu.
Msimu uliopita Arsenal ilitwaa ubingwa wa ligi baada ya miaka 22. Mafanikio hayo yalijengwa kwa ulinzi imara, kikosi chenye uwezo na matumizi ya tofauti ndogo zinazoweza kuamua mechi. Hakuna eneo lililoonyesha hilo zaidi ya mipira iliyokufa.
Arsenal ilifunga mabao 19 kutokana na kona msimu wa 2025/26, rekodi ya ligi. Asilimia 26.8 ya mabao yake yote yalitokana na kona, kiwango cha juu zaidi kwa timu yoyote iliyowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England.
Waamuzi walipoanza kufuatilia kwa karibu kushikana na kuzuiana wakati wa kona msimu huu, ilitarajiwa Arsenal iendelee kutumia ubora wake.
Lakini baada ya mechi nane, haijafunga bao kupitia kona, wala bao lolote kutokana na mipira iliyokufa isiyokuwa penalti katika mashindano yote. Katika hatua kama hii msimu uliopita, tayari ilikuwa imefunga mabao sita kupitia kona. Je, Arsenal imepoteza makali au kuna sababu nyingine?
ARSENAL IMEPOTEZA MAKALI YA KONA
Baada ya mechi nane, idadi ya mabao pekee haitoshi kuonyesha ufanisi wa Arsenal katika kona. Kipimo cha mabao tarajiwa (xG) kinaweza kutoa picha pana zaidi, kwa kuwa huonyesha uwezekano wa nafasi kuzaa bao.
Msimu uliopita, Arsenal iliongoza ligi kwa mabao tarajiwa 13.8 yaliyotokana na kona. Hiyo ilikuwa wastani wa 0.36 kwa kila mechi, au 0.064 kwa kila kona, sawa na uwezekano wa asilimia 6.4 kwa kila kona kuzaa bao. Kiwango hicho kilikuwa cha pili kwa ubora. Kwa uhalisia, Arsenal ilifanya vizuri zaidi ya matarajio, ikifunga kupitia asilimia 8.8 ya kona zake, kiwango cha juu zaidi ligi.
Msimu huu, Arsenal inazalisha mabao tarajiwa 0.22 pekee kwa kila mechi kupitia kona, sawa na 0.047 kwa kila kona. Kutoka nafasi ya pili kwa hatari ya kila kona msimu uliopita, imeshuka hadi nafasi ya tisa. Tofauti hiyo ina maana ubora wa wastani wa nafasi umepungua kwa asilimia 26.6.
Pia inatengeneza mashuti machache. Msimu uliopita ilikuwa na wastani wa mashuti 2.8 kwa kila mechi kutokana na kona, kiwango cha pili bora ligi. Msimu huu ni 2.1, na kuiacha katika nafasi ya tisa.
Arsenal tayari imetengeneza mabao tarajiwa 1.55 kupitia kona, jumla ya saba kwa ukubwa ligi, ikionyesha ilitarajiwa kufunga angalau bao moja. Liverpool pekee, yenye upungufu wa mabao 2.05 ikilinganishwa na matarajio yake ya kona, imefanya vibaya zaidi kuliko Arsenal, ambayo ina upungufu wa 1.55.
KUNA NINI UPIGAJI KONA?
Kushuka kwa ufanisi hakukutokana na kubadilika kwa mbinu. Msimu wa 2025/26, Arsenal ilipiga krosi kuelekea ndani ya eneo la hatari katika asilimia 86.6 ya kona zake na kutumia pasi fupi katika asilimia 13. Msimu huu, krosi ni asilimia 84.9 na pasi fupi asilimia 15.1. Kwa hiyo, uwiano huo haujabadilika sana.
Arsenal kwa muda mrefu imekuwa ikitumia kona zinazopinda kuelekea ndani ya lango (inswinging corners). Msimu uliopita, asilimia 96.3 ya kona zake zilizopigwa kwa krosi zilikuwa za aina hiyo; msimu huu ni asilimia 100. Hivyo, imeimarisha zaidi mbinu iliyowahi kuipa mafanikio. Ikiwa mkakati haujabadilika, huenda tatizo likawa namna inavyoutekeleza.
WACHEZAJI WANAGUSA MIPIRA MARA CHACHE?
Takwimu za mguso wa kwanza zinaonyesha kuwa wapigaji wa kona si lazima wawe tatizo. Msimu uliopita, wachezaji wa Arsenal walikuwa wa kwanza kugusa mpira katika asilimia 28.3 ya kona zilizopigwa kwa krosi, kiwango cha wastani kilichoiweka nafasi ya 12. Msimu huu kiwango kimepanda hadi asilimia 42.9, cha pili kwa ukubwa ligi. Hii ina maana wanafikia mipira ya kona mara nyingi zaidi.
Tatizo huenda likawa kinachotokea baada ya mguso wa kwanza: ni nani anayeugusa na anakuwa katika eneo gani la hatari. Tofauti moja kubwa ni kukosekana kwa William Saliba na Jurrien Timber katika sehemu kubwa ya msimu huu. Timber hasa hakupata sifa za kutosha kwa mchango wake kwenye kona msimu uliopita.
Timber alifunga mabao mawili kutokana na kona mwaka 2025/26, zaidi ya mchezaji mwingine yeyote wa Arsenal. Pia aligusa mpira kwa kichwa mara saba kama mchezaji wa kwanza kufikia kona, nyuma ya Gabriel Magalhaes aliyefanya hivyo mara 10. Kutokuwepo kwake kumebadilisha mgawanyo wa wachezaji wanaogusa mipira ya kwanza.
Kai Havertz ndiye aliyegusa mpira wa kwanza mara nyingi zaidi kwenye kona za kushambulia msimu huu, akiwa na miguso minne. Gabriel, ambaye mara nyingi huonekana akijiandaa karibu na eneo la lango kabla ya kona kupigwa, amefanya hivyo mara moja tu. Hajaonyesha mafanikio makubwa kama msimu uliopita.
Ezri Konsa naye hajulikani kama tishio kubwa la mipira ya kona. Amefunga mabao mawili tu ya kichwa katika maisha yake ya Ligi Kuu England. Tangu aanze kucheza ligi hiyo, mabeki 238 wamefunga mabao mengi zaidi ya vichwa kuliko yeye.
Alifunga bao la kichwa kutokana na kona akiwa na timu ya taifa ya England katika mchezo wa kuwania nafasi ya tatu wa Kombe la Dunia 2026, lakini hilo si jambo la kawaida kwake.
Ben White, aliyechukua nafasi ya Timber, bado hajagusa mpira wowote wa kona kwa kichwa. Hata hivyo, mara nyingi jukumu lake ni kuwazuia wapinzani au kuvuruga ulinzi wao. Sababu nyingine inayoweza kuathiri ufanisi ni maeneo ambayo mipira ya kona inaishia ndani ya eneo la hatari.
MAENEO YAPI INAISHIA MIPIRA?
Ingawa mbinu za jumla hazijabadilika, kuna tofauti ndogo katika maeneo ambayo mipira inaelekezwa. Msimu uliopita Arsenal ilikuwa hatari hasa katikati ya eneo dogo la lango. Ilitumia kona zinazopinda kuelekea ndani kuleta vurugu mbele ya lango na kuwasongamanisha wachezaji karibu na kipa wa wapinzani.
Msimu huu, kona zinazoishia katikati ya eneo dogo la lango zimepungua kwa asilimia 7.7, huku zinazoelekezwa karibu na nguzo ya kwanza zikiongezeka kwa asilimia 7.8.
Wakati mwingine hilo linaweza kutokana na namna mpira unavyopigwa. Arsenal mara nyingi hupiga kona kwa nguvu na mwinuko mdogo, hivyo kosa dogo linaweza kuufanya mpira umfikie mchezaji aliye karibu na nguzo ya kwanza.
Katika matukio mengine, kuelekeza mpira karibu na nguzo ya kwanza kunaonekana kuwa mpango. Arsenal imeongeza mbinu ya mchezaji kukimbilia eneo hilo, kugusa mpira kwa kichwa na kuuelekeza upande mwingine. Kuna mifano minne ya mbinu hiyo, miwili katika mchezo mmoja dhidi ya Nottingham Forest.
Mbinu hiyo ikifanikiwa, mguso mzuri wa kichwa unaweza kuuelekeza mpira katika eneo hatari kabla mabeki hawajajipanga. Lakini mafanikio yake yanategemea utekelezaji.
Arsenal inahitaji miguso miwili: wa kwanza kuelekeza mpira, kisha shuti la mwisho. Hilo ni tofauti na mbinu inayohitaji mguso mmoja tu kuunda nafasi ya kufunga.
Huenda Arsenal inajaribu kurejesha vurugu karibu na lango kwa njia tofauti, kufuatia hatua kali za waamuzi dhidi ya kushikana na kuzuiana.
MWONGOZO MPYA WA WAAMUZI EPL
Msimu huu, waamuzi wa Ligi Kuu England wameelekezwa kufuatilia kwa karibu kushikilia, kushikana na kuzuiana wakati wa kona. Lengo ni kuzuia wachezaji kupata faida isiyo halali kwa kuwazuia wapinzani kucheza mpira. Waamuzi wamezingatia maelekezo hayo.
Kutokana na hilo, kona zinazoishia kwa timu inayolinda kupewa faulo zimeongezeka hadi asilimia 4.0, kiwango cha juu zaidi katika misimu saba iliyopita. Kwa jumla, kona zimezaa mabao machache kuliko msimu uliopita.
Hadi sasa, mabao 20 kati ya 203 yaliyofungwa ligi msimu huu yametokana na kona, sawa na asilimia 9.8. Msimu uliopita, mabao 188 kati ya 1,045 yalitokana na kona, sawa na asilimia 18. Kwa hiyo, uwiano wa mabao ya kona umekaribia kupungua kwa nusu.
Huenda mwongozo mpya umechangia kushuka huko. Arsenal imeadhibiwa mara moja pekee msimu huu kwa faulo ya kushambulia wakati wa kona. Timu saba zimefanya makosa hayo mara nyingi zaidi. Hata hivyo, kutoadhibiwa mara nyingi hakumaanishi kwamba mwongozo haujaiathiri Arsenal.
Takwimu zinaonyesha mara ngapi timu imeadhibiwa, lakini haziwezi kuonyesha vitendo ambavyo wachezaji wameamua kutovifanya kwa sababu ya mwongozo.
Kwa kuangalia uchezaji wake, inaonekana Arsenal imepunguza tabia ya kuwasongamanisha kwa nguvu wachezaji karibu na makipa wa wapinzani, jambo lililotambulisha mbinu zake za mipira iliyokufa.
ARSENAL HAITEGEMEI TENA MIPIRA YA KONA
Kutofunga kupitia kona hakujaiathiri sana Arsenal. Imeshinda mechi zake zote za Ligi Kuu England msimu huu isipokuwa moja, ikiwa nyuma ya vinara Manchester City na bado ikitajwa miongoni mwa timu zinazoweza kutetea taji.
Wakati hatari yake kupitia kona imepungua, uwezo wa kushambulia katika mchezo wa kawaida umeimarika. Msimu uliopita, Arsenal ilikuwa na wastani wa mabao tarajiwa 1.06 kwa kila mechi kupitia mchezo wa wazi, yaani mashambulizi yasiyotokana na mipira iliyokufa.
Msimu huu kiwango hicho kimepanda hadi 1.24, ongezeko la takribani asilimia 17. Hilo linaashiria kuwa inatengeneza nafasi bora zaidi katika mchezo wa kawaida kuliko ilivyokuwa wakati wa kampeni yake ya ubingwa.
Pia kuna dalili kwamba mipira iliyokufa imepungua kuwa kipaumbele katika kutafuta njia ya kuvunja ulinzi wa wapinzani. Arsenal bado inapiga krosi kuelekea ndani ya eneo la hatari wakati wa kona, lakini imebadili kabisa matumizi ya mipira mirefu ya kurusha kwa mikono kuelekea eneo la hatari (long throws).
Msimu uliopita, Arsenal ilirusha wastani wa mipira mirefu 1.5 kwa kila mechi kuelekea eneo la hatari la wapinzani. Hilo lilionyesha jinsi ilivyokuwa tayari kutumia karibu kila nafasi ya kuanzisha upya mchezo kama fursa ya kushambulia.
Msimu huu, imejaribu mipira miwili pekee ya aina hiyo katika mechi zake saba za mwanzo za ligi. Hilo ni punguzo kubwa na huenda ni ishara kwamba haiweki nguvu nyingi kama awali katika kutengeneza nafasi kupitia mipira iliyokufa.
Ni wazi kwamba Arsenal imepoteza baadhi ya makali yake kwenye kona. Hata hivyo, kutofunga bao lolote kunaweza kutoa picha isiyo sahihi, kwa sababu imetengeneza nafasi zinazoweza kuhalalisha matarajio ya kufunga angalau bao moja.
Arsenal imeimarisha mashambulizi ya mchezo wa wazi na bado inapata matokeo ya kuwania ubingwa. Kwa timu iliyokosolewa msimu uliopita kwa kutegemea sana kona, huenda hili si badiliko baya.
Kwa kuzingatia ubora wa nafasi inazotengeneza, itakuwa jambo la kushangaza ikiwa itaendelea kukosa mabao kupitia kona kwa muda mrefu.
Ikiwa Arsenal itarejesha makali yake ya mipira iliyokufa kwa kutumia mbinu mpya na kuendeleza uwezo wake wa kushambulia katika mchezo wa kawaida, timu nyingine za ligi zinaweza kujikuta na changamoto kubwa zaidi ya kuikabili.