JICHO LA MWEWE: Kwa Chikwende tumetimiza tu maandiko ya ukutani

NILIANDIKA hapa wiki tatu zilizopita namna ambavyo kuna timu kubwa ya Tanzania ingepiga kambi kwa wakala wa staa wa klabu ya FC Platinum ya Zimbabwe, Perfect Chikwende baada ya kuonyesha kandanda safi katika mechi mbili za Simba dhidi ya Platinum.
Ilikuwa wazi kwamba timu moja kati ya Yanga, Simba au Azam ingeingia katika mchakato wa kumnasa. Hatimaye timu mbili ziliingia katika mchakato huo, Simba na Azam. Na hatimaye Simba walifanikiwa kuinasa saini yake.
Ni mwendelezo wa kile ambacho nilitabiri wiki tatu zilizopita. Klabu zetu kubwa huwa zina namna mbili za kufanya uskauti wa mchezaji hasa wa kigeni. Kwanza ni pale mchezaji anapong’ara katika mechi dhidi yao. Pili ni mchezaji anapong’ara akiwa na wapinzani hao hapa nchini.
Miaka ya karibuni hii ndio njia waliyopatikana Luis Miquissone na Saido Ntibanzonkiza ambaye hata hivyo yeye alionekana katika pambano la Burundi dhidi ya Tanzania lililochezwa miezi michache iliyopita hapa nchini. Ukiwauliza viongozi watakwambia walikuwa wanamjua mchezaji mapema kabla ya hapo. ukweli ni kwamba wanakuwa wametunga tu stori.
Tutazame suala la Chikwende na hali halisi. Ni mchezaji mzuri. Simba wanaamini kwamba Chikwende ni bora kuliko Bernard Morrison? Sielewi vema. Ninachojua ni kwamba wakati Simba wanapambana kumnasa Morrison labda hawakujua uwepo wa Chikwende kule Zimbabwe.
Kuna mambo mawili hapa. Simba wangekuwa na nafasi ya kuwekewa wachezaji hawa mezani kuna kundi lingetaka wasimfuatilie Morrison aliyekuwa Yanga na badala yake moja kwa moja wangetaka wamchukue Chikwende.
Lakini hapo hapo tunaweza kuwaza kwamba huenda kuna kundi bado lingemtaka Morrison kwa sababu ya kuwaumiza roho watani zao Yanga ambao walitokea kumpenda vilivyo staa huyo kutoka Ghana aliyewahi kuwafunga bao zuri na la ushindi watani zao.
Ni kweli Simba wasingemsajili Chikwende kama Morrison asingekuwa mgonjwa? Sina uhakika. Wakati mwingine kama una pesa unarundika tu wachezaji. Nadhani kuna watu bado wangetaka Chikwende achukuliwe. Ni Kama hivi ilivyotokea. Siamini kama wangemfungia milango kwa sababu ya Morrison.
Hapo hapo kumbuka kwamba wakati mwingine Chikwende ilikuwa lazima achukuliwe kwa sababu angeweza kwenda kwa watani zao Yanga au wapinzani wao wengine Azam ambapo angeongeza nguvu maradufu.
Usajili wa Chikwende unatuachia maswali kutokana na ukweli kwamba Morrison ni mchezaji lakini hata wakati alipokuwa fiti bado nafasi yake ilikuwa ya kusuasua pale Msimbazi. Na sasa swali linakuja. Simba itaachana na Morrison? Inadaiwa kwamba anaumwa Ugonjwa wa Ngiri ‘Hernia’ na anaweza kufanyiwa operesheni ambayo itamuweka nje kwa miezi sita. Swali ni kama atafanikiwa kurudi kuwa fiti basi kocha wa Simba atalazimika kusumbua kichwa chake. Eneo la katikati na pembeni pale Msimbazi limesheheni kweli kweli. Kwa kuanzia kuna wachezaji wa nguvu ambao ni Rally Bwalya, Clotious Chama, Luis Miquissone, Morrison, Francis Kahata na Chikwende. Hii ni achilia mbali akina Hassan Dilunga, Miraji Athuman na Ibrahim Ajib.
Miraji amewakumbusha Simba kile anachoweza kufanya uwanjani kupitia michuano ya Kombe la Mapinduzi. Nadhani atawapa wakati mgumu kufanya uamuzi kuhusu yeye. Ajib anaweza kuwa anamalizia miezi yake ya mwisho Msimbazi. Dilunga sijui watu wa Simba wanafikiria nini kuhusu yeye.
Hapo kwa kwa Chama, Bwalya, Chikwende, Miquissone na Morrison nadhani kunaifanya Simba ichanganyikiwe kidogo. Wataachana na Morrison hata akirudi baada ya miezi sita? Ni jambo linalowezekana. Sio Wanasimba wote wanafurahia uwepo wake klabuni kutokana na tabia zake za ajabu ajabu alizoanzia Yanga mpaka kwao. Tatizo ni suala la aibu. Kuna soni katika kukiri kwamba ulikuwa uhamisho wa kuwakoga watani zaidi kuliko hali halisi. Wanaweza kuendelea kuwa naye lakini sidhani kama atakuwa na maisha marefu hasa kama Chikwende akihamishia moto wake vema Msimbazi.
Kama kocha, Sven Vandebroeck angeendelea Msimbazi nadhani angepata wakati mgumu zaidi. Nyuma ya mastaa hawa watano huwa anatumia viungo wawili. Jonas Mkude na kiungo mwingine wa ukabaji na usambazaji. Simba tayari wana mtu katika nafasi hiyo. Wamemchukua majuzi kutoka Uganda.
Hii ina maana katika kundi la Chama, Miquissone, Bwalya, Chikwende na Morrison wanahitajika viungo watatu tu hapo na mshambuliaji mmoja mbele. lakini kama mashabiki wakiendelea kung’ang’ania kocha acheze washambuliaji wawili basi hali hapo kwa Chama, Bwalya, Miquissone, Chikwende na Morrison inabidi wacheze viungo wawili.
Imeandikwa na Edo Kumwembe