Kombe la Dunia 2026, sherehe tatu za ufunguzi zitakazoandika historia
Muktasari:
- Mashindano haya yatakuwa ya kwanza kufanyika katika nchi tatu kwa pamoja Marekani, Canada na Mexico na yatashirikisha timu 48 badala ya 32 kama ilivyokuwa awali.
NEW YORK, TORONTO: KOMBE la Dunia la FIFA 2026 linatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa zaidi ya michezo kuwahi kushuhudiwa duniani, sio tu kwa ukubwa wake wa kimashindano bali pia kwa namna litakavyopangiliwa.
Mashindano haya yatakuwa ya kwanza kufanyika katika nchi tatu kwa pamoja Marekani, Canada na Mexico na yatashirikisha timu 48 badala ya 32 kama ilivyokuwa awali.
Hii ina maana kwamba dunia itashuhudia mashindano makubwa zaidi, yenye mechi 104 zitakazopigwa katika miji mbalimbali ya mataifa hayo matatu.
Kinachozua mvuto zaidi katika fainali za mwaka huu 2026 ni uamuzi wa kuwa na sherehe tatu tofauti za ufunguzi, kila moja ikifanyika katika nchi mwenyeji tofauti.
Haya ni mabadiliko makubwa katika historia ya Kombe la Dunia, ambapo kwa miaka yote iliyopita sherehe ya ufunguzi ilikuwa moja tu. Sasa, FIFA inalenga kuonyesha utofauti wa mataifa wenyeji huku ikiunganisha dunia kupitia muziki, utamaduni na soka katika tukio moja la kimataifa.
Kwa mujibu wa shirikisho la soka duniani FIFA, sherehe hizi zitatumia “mstari mmoja wa ubunifu” unaounganisha kila tukio, lakini kila nchi itaruhusiwa kuonesha utambulisho wake wa kipekee kupitia sanaa, muziki na tamaduni zake. Hii ina maana kwamba, ingawa tukio litakuwa moja kiroho na kimashindano, kila sehemu ya dunia itapata ladha yake maalum inayowakilisha taifa husika.
Rais wa FIFA, Gianni Infantino, ameeleza kuwa lengo kuu la mpango huu ni kuifanya dunia kuona soka si tu kama mchezo, bali kama daraja la kuunganisha watu wa tamaduni zote. Amesema kuwa ufunguzi wa Kombe la Dunia 2026 utakuwa “mwanga wa umoja wa dunia” unaoonesha jinsi michezo inavyoleta watu pamoja bila kujali mipaka ya kisiasa, lugha au historia zao.
Mashabiki wa soka duniani kote wanatarajia kwa hamu kubwa tukio hili, hasa kutokana na ukweli kwamba Kombe la Dunia la 2022 lililotangulia lilivutia zaidi ya watazamaji milioni 550 katika mechi ya ufunguzi pekee. Hii inaweka presha kubwa kwa mataifa mwenyeji kuhakikisha kwamba sherehe za 2026 zitakuwa za kiwango cha juu zaidi, zenye ubunifu wa kipekee na burudani za kutosha.
MEXICO NA UFUNGUZI WA HISTORIA
Sherehe ya kwanza ya ufunguzi itafanyika nchini Mexico, katika jiji kubwa na lenye historia ndefu ya soka la kimataifa, Mexico City. Tukio hili litafanyika Juni 11, 2026, likitangulia mchezo wa kwanza wa mashindano (Mexico vs Afrika Kusini). Mexico, ikiwa ni moja ya nchi zenye historia ndefu katika Kombe la Dunia, imepewa heshima ya kufungua pazia la mashindano haya makubwa.
Sherehe ya Mexico inatarajiwa kuwa ya rangi, muziki na sanaa inayotokana na utamaduni wa Kilatino. Moja ya alama muhimu zitakazotumika ni sanaa ya jadi inayojulikana kama “papel picado,” ambayo ni mapambo ya karatasi yaliyokatwa kwa ustadi mkubwa na hutumika katika sherehe mbalimbali za kitamaduni nchini humo. Sanaa hii inawakilisha furaha, maisha na historia ya watu wa Mexico na inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mandhari ya ufunguzi.
Serikali ya Mexico imeahidi kuwa sherehe hii haitakuwa ya kawaida, bali itakuwa tukio la kihistoria litakaloonyesha uwezo wa taifa hilo kuandaa matukio makubwa ya kimataifa.
Rais wa taifa hilo, Claudia Sheinbaum Pardo ameweka wazi kuwa Mexico inataka kutumia fursa hii kuonyesha utajiri wa utamaduni wake kwa dunia nzima huku ikithibitisha tena nafasi yake kama moja ya mataifa makubwa ya soka duniani.
Katika upande wa burudani, Mexico imeandaa safu ya wasanii wakubwa wa muziki wa Kilatino na wa kimataifa. Bendi maarufu ya Maná inatarajiwa kuwa miongoni mwa vichwa vya habari vya sherehe hii, huku msanii Alejandro Fernández akitarajiwa kuleta ladha ya muziki wa mariachi na baladi za kimapenzi.
Aidha, J Balvin atawakilisha kizazi kipya cha muziki wa ‘reggaeton’ na Latin pop, akiwasha jukwaa kwa miondoko ya kisasa. Wasanii wengine kama Belinda, Danny Ocean, Lila Downs na Los Ángeles Azules watachangia kuongeza ladha ya kipekee ya muziki wa Mexico huku mshiriki kutoka Afrika Kusini, Tyla, akitarajiwa kuleta muunganiko wa muziki wa Afrika na dunia.
Mchanganyiko huu wa wasanii unaonyesha wazi kwamba sherehe hii haiko tu kwa Mexico, bali ni ya dunia nzima.
Mexico pia ina historia kubwa ya kuandaa Kombe la Dunia, ikiwa imewahi kuwa mwenyeji mwaka 1970 na 1986. Katika matukio hayo, dunia ilishuhudia mechi za kihistoria na nyota wakubwa wa soka.
Sasa, miaka zaidi ya miongo mitatu baadaye, taifa hilo linarejea tena katika jukwaa la dunia likiwa na dhamira ya kuandika ukurasa mpya wa historia ya soka.
PATI ITAHAMIA CANADA
Siku moja baada ya sherehe ya Mexico, macho ya dunia yataelekezwa nchini Canada, ambapo sherehe ya pili ya ufunguzi itafanyika katika jiji la Toronto Juni 12, 2026. Tofauti na Mexico, Canada inatarajiwa kuwasilisha sherehe yenye ladha inayolenga kuonyesha utofauti wa watu wake na mshikamano wa kijamii unaojengwa na tamaduni mbalimbali.
Canada inajulikana kama moja ya mataifa yenye mchanganyiko mkubwa wa watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia na hii ndiyo itakuwa kiini cha sherehe yake ya ufunguzi.
Mandhari ya tukio hilo yatatumia wazo la “mosaiki ya taifa,” ambapo kila kipande cha utamaduni kinawakilisha jamii tofauti zinazounda nchi hiyo. Hii ina maana kwamba muziki, sanaa na maonyesho yatakuwa na mchanganyiko wa ladha za kimataifa zinazowakilisha kila kona ya dunia.
Wasanii watakaoshiriki katika sherehe hii ni pamoja na Michael Bublé, Jessie Reyez, Alanis Morissette na Alessia Cara ambao ni miongoni mwa majina makubwa ya muziki wa Canada.
Pia kutakuwa na William Prince, DJ Sanjoy na Vegedream, ambao wataongeza ladha ya kimataifa katika jukwaa hilo.
Zaidi ya hapo, ushiriki wa Nora Fatehi na Elyanna unaonyesha wazi kwamba Canada inataka kuonyesha kuwa sherehe hii si ya ndani tu, bali ni ya kimataifa. Hawa wasanii wanatarajiwa kuleta mchanganyiko wa muziki wa Mashariki ya Kati, Asia na Amerika ya Kaskazini, jambo litakalofanya tukio hilo kuwa la kipekee zaidi.
Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney amesisitiza kuwa taifa hilo liko tayari kuwakaribisha wageni kutoka kila pembe ya dunia, akisema kuwa Kombe la Dunia 2026 ni nafasi ya kuonyesha kuwa Canada ni taifa la amani, upendo na mshikamano wa kimataifa.
Sherehe hii pia inatarajiwa kuwa na ujumbe mkubwa wa kuhimiza usawa na ujumuishaji wa kijamii kupitia michezo.
MAREKANI ITAKUWA FUNGA KAZI
Sherehe ya tatu na ya mwisho ya ufunguzi itafanyika nchini Marekani, katika jiji la Los Angeles, Juni 12, 2026 jioni. Tukio hili linatarajiwa kuwa kubwa zaidi kwa upande wa burudani, likiwa limejikita katika tasnia ya muziki na filamu ambayo Marekani inajulikana nayo duniani kote.
Los Angeles, ikiwa ni kitovu cha burudani duniani, itatumika kama jukwaa la kuonyesha nguvu ya Marekani katika muziki, utamaduni na michezo.
Wasanii wakubwa wa kimataifa watapanda jukwaani, akiwemo Katy Perry, Future, Tyla, LISA kutoka kundi la BLACKPINK, Anitta na Rema. Mchanganyiko huu wa wasanii kutoka mabara tofauti unaonyesha wazi kwamba sherehe hii inalenga dunia nzima, si Marekani pekee.
Sherehe ya Marekani pia inatarajiwa kuwa na ujumbe mkubwa wa umoja na mshikamano, hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo ina jamii mbalimbali za wahamiaji kutoka duniani kote.
Hii inafanya tukio hilo kuwa la kipekee zaidi, kwani litakuwa linaakisi maisha halisi ya Marekani kama taifa lenye utofauti mkubwa wa kitamaduni.
Meya wa Los Angeles, Karen Bass amesisitiza kuwa jiji hilo litahakikisha kila mshabiki anapata nafasi ya kuwa sehemu ya historia hiyo, kupitia matukio ya bure ya kuangalia mechi, mafunzo ya soka kwa vijana na sherehe za kijamii zitakazofanyika maeneo mbalimbali ya jiji.