Prime
Ligi Kuu bado kinawaka, wachezaji Yanga, Simba wakabana

Muktasari:
- Mastaa 12 tayari wamejitokeza kuwania tuzo hiyo, huku kila mmoja akipambana kwa nguvu kuhakikisha anaweka historia binafsi, sambamba na kuisaidia timu yake kufikia malengo.
WAKATI burudani ya Ligi Kuu Bara ikiendelea kwa ushindani mkali kila kona, mapambano yamehamia katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu tuzo inayokwenda kwa mfungaji bora wa msimu.
Mastaa 12 tayari wamejitokeza kuwania tuzo hiyo, huku kila mmoja akipambana kwa nguvu kuhakikisha anaweka historia binafsi, sambamba na kuisaidia timu yake kufikia malengo.
Hadi sasa, kinara wa mabao ni kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Charles Jean Ahoua, ambaye amefikisha mabao 12, akiwa ameonesha kiwango bora katika mechi nyingi alizocheza msimu huu.

Mchezaji huyo raia wa Ivory Coast amekuwa chachu ya mafanikio ya Simba kwa kucheza namba 10, huku akitupia mabao muhimu ambayo yameipa uhai timu hiyo katika harakati zake za kuwania ubingwa.
Mabingwa watetezi Yanga wanawakilishwa vyema kwenye orodha hiyo ya wafungaji kupitia washambuliaji wawili Clement Mzize na Prince Dube ambao kila mmoja amefunga mabao 11.
Elvis Rupia wa Singida Black Stars naye yupo kwenye orodha hiyo akiwa na mabao 10 huku mshambuliaji wa Simba, Steven Mukwala, raia wa Uganda akiwa nayo tisa.
Mukwala ameendelea kuonesha umahiri wake mbele ya lango tangu ajiunge na Simba msimu uliopita na kwa sasa ndiye mshambuliaji anayepewa jukumu la kuongoza safu ya ushambuliaji ya Wekundu wa Msimbazi, akishirikiana na Leonel Ateba aliyefikisha mabao nane, sawa na Pacome Zouzoua wa Yanga.
Nyota wengine wanaofukuzia tuzo hiyo kwa mabao saba kila mmoja ni: Stephane Aziz Ki, Gibril Sillah wa Azam FC, na Offen Chikola wa JKT Tanzania.
Hata hivyo, vita hiyo utamu wake ni katika mechi zilizobaki kwa kila nyota na kikosi chake na wanaweza kufunga zaidi endapo watapata nafasi ya kucheza.

Mechi zilizosalia za Simba ambazo ni dhidi ya Mashujaa FC, JKT Tanzania, Pamba Jiji, KMC, Singida Black Stars, KenGold, Kagera Sugar na ule wa Yanga ambao bado haijajulikana hatma yake, zinampa nafasi Ahoua ya kuendelea kuongoza msimamo huo wa wafungaji kama atapata nafasi ya kufunga licha ya kikosi hicho kuwa na wafungaji wengine na anayemfuatia kwenye kikosi hicho ni Mukwala na hata Ateba mwenye saba.
Mzize na Dube pia wana nafasi kubwa ya kubeba kiatu hicho na ndio wanaoibeba Yanga kwa sasa kwenye ufungaji wakilingana mabao 11. Nyota hao ambao wote ni washambliaji juzi Jumatatu walishindwa kufunga mabao dhidi ya Coastal United katika ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Pacome.
Wawili hao wamepakisha mechi sita za kuamua kama mmoja au wote watabeba kiatu kwa kulingana mabao na wataanza na Azam FC, kisha itacheza na Fountain Gate, Namungo, Prisons, Dodoma na Simba ambao haijajulikana hatma ya mchezo huo.

MZIZE: NAISAIDIA TIMU YANGU KWANZA
Akizungumza na Mwanaspoti, mshambuliaji wa Yanga, Mzize alisema licha ya kuwa katika nafasi nzuri ya kuwania kiatu cha dhahabu, hana presha ya ushindani huo bali analenga kutimiza majukumu yake ya kuipeleka Yanga kwenye ubingwa.
“Vita ni kubwa, kila mchezaji ana nafasi. Lakini kwangu muhimu zaidi ni kuisaidia timu yangu kutetea ubingwa. Nafasi yoyote nitakayopata nitatumia vizuri, suala la ufungaji bora litakuja baadaye,” alisema.
Mzize amebakiza mabao manane tu kufikia rekodi ya mabao 19 aliyoweka Feisal Salum ‘Fei Toto’ msimu uliopita akiwa mchezaji wa ndani, ingawa hakutwaa kiatu cha dhahabu kilichochukuliwa na Aziz Ki aliyefunga mabao 21.

RUPIA: NAAMINI NINA NAFASI
Kwa upande wake, Rupia ambaye amekuwa na msimu wa kupanda na kushuka, alisema amerejea kwenye kiwango bora na ana matumaini ya kuendelea kufunga ili kuisaidia timu yake kumaliza katika nafasi za juu.
“Nilianza msimu vizuri, nilikuwa nafunga kila mechi. Ghafla nikapotea kidogo lakini sikuacha kuamini. Nashukuru kwa sasa narudi tena kwenye kasi. Nafurahi kufunga na naamini nina nafasi ya kufanya vizuri zaidi,” alisema.

MUKWALA: MABAO NI MAJUKUMU YETU
Mshambuliaji wa Simba SC, Mukwala alisema wachezaji wa mbele wanapaswa kuwajibika kwa mabao na si kuogopa presha ya ushindani wa tuzo.
“Kila mshambuliaji anajua kuwa kazi yetu ni kufunga. Tuzo ni matokeo ya kazi hiyo. Nafurahia kuwa kwenye orodha ya wanaowania kiatu cha dhahabu, lakini kubwa zaidi ni kuiwezesha Simba kufanya vizuri,” alisema Mukwala.
Kwa jinsi msimu unavyoelekea ukingoni, vita ya mfungaji bora inaonekana kuwa ya wazi zaidi kuliko misimu ya nyuma, huku nafasi ikiwa wazi kwa mchezaji yeyote miongoni mwa hao 12 kufanikisha ndoto hiyo.
MSIMAMO WA LIGI
Mbali na vita ya mfungaji bora, ligi imeendelea kuwa na ushindani mkubwa hasa katika nafasi nne za juu. Yanga SC inashika nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 64, ikifuatiwa na Simba SC (57), Azam FC (51), na Singida Black Stars (50).
Katika hali hiyo, kila bao linalofungwa na nyota waliopo kwenye mbio za kiatu cha dhahabu pia lina mchango mkubwa kwa nafasi ya timu kwenye msimamo wa ligi.
MECHI ZILIZOBAKI YANGA
vs Azam FC (ugenini)
vs Fountain Gate (ugenini)
vs Namungo (nyumbani)
vs Tanzania Prisons (ugenini)
vs Dodoma Jiji (nyumbani)
vs Simba (ugenini)
AZAM FC
vs Yanga (nyumbani)
vs Kagera Sugar (ugenini)
vs Dodoma Jiji (nyumbani)
vs Tabora United (nyumbani)
vs Fountain Gate (ugenini)
SINGIDA BLACK STARS
vs Coastal Union (ugenini)
vs Tabora United (nyumbani)
vs Simba (ugenini)
vs Dodoma Jiji (ugenini)
vs Tanzania Prisons (nyumbani)