Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ligi Kuu Bara yapasuka vipande vitatu

Muktasari:

  • Mgawanyiko huo unatokea kufuatia asilimia kubwa ya timu kubakiwa na mechi nne, huku hivi sasa zikiwa na wiki moja kujiuliza itakuwaje baada ya ligi kusimama kabla ya kuendelea Aprili 18, mwaka huu.

ZIMEBAKI hatua chache kumfahamu bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu sambamba na zile timu zitakazoshuka daraja. Wakati hayo yakisubiriwa kwa hamu hivi sasa ligi hiyo imegawanyika vipande vitatu.

Mgawanyiko huo unatokea kufuatia asilimia kubwa ya timu kubakiwa na mechi nne, huku hivi sasa zikiwa na wiki moja kujiuliza itakuwaje baada ya ligi kusimama kabla ya kuendelea Aprili 18, mwaka huu.

Ligi hiyo imesimama kupisha michezo ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) ambayo inachezwa kuanzia Jumapili hii hadi Jumanne, Aprili 15, 2025.

Mchezo wa mwisho kabla ya ligi kusimama Yanga iliifunga Azam mabao 2-1. Ushindi huo sio tu uliwashangaza wapinzani wao wa karibu, bali pia umebadilisha taswira ya ligi na kuonyesha hali halisi ya namna ilivyogawanyika vipande vitatu ambavyo ni mbio za ubingwa, vita ya kumaliza nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa na ile ya kuwania kubaki msimu ujao.

Katika hatua hii ambapo mechi zimebaki chache kabla ya pazia kufungwa Mei 25, mwaka huu kama ratiba inavyoonyesha, kila mchezo ni muhimu kuliko wakati mwingine wowote. Matokeo ya kila mzunguko yanabadilisha mwelekeo wa msimamo wa ligi na kuongeza presha kwa kila kikosi, kocha, wachezaji na hata mashabiki.

Ndiyo maana baada ya Yanga kulipa kisasi dhidi ya Azam ambao waliwafanya kitu kibaya duru la kwanza kwa kufungwa 1-0, mwelekeo wa ligi umebadilika kwa kiwango kikubwa, huku kila kipande kikionyesha taswira yake.

Kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi baada ya mechi hiyo alisema kuwa sasa ni vigumu kwao kutwaa ubingwa na hivyo wanaelekeza nguvu kumaliza msimu kwa heshima na kuwania tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa.


VITA YA UBINGWA

Yanga inaongoza Ligi Kuu kwa pointi 67 baada ya mechi ikishinda 22, sare moja na kupoteza mbili dhidi ya Azam na Tabora United - zote katika duru la kwanza. Kikosi hicho cha kocha Miloud Hamdi kimeonyesha kiwango bora msimu huu kikicheza soka la kushambulia, nidhamu, na uzoefu mkubwa wa wachezaji wake nyota kama Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Prince Dube na Clement Mzize.

Simba inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 57 katika mechi 22, tofauti ya pointi 10 dhidi ya Yanga iliyozidi pia michezo mitatu. Simba michezo hiyo mitatu ya kiporo ni dhidi ya Mashujaa, JKT Tanzania na Pamba Jiji ambayo itaicheza Mei 2, 5 na 8 wakati ambapo Yanga haitakuwa na mchezo wowote. Kama Simba itashinda michezo yote itaendelea kubaki nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi moja. Yanga itakuwa na 67 ilhali Simba 66. Baada ya hapo timu hizo zitakuwa zimesaliwa na michezo mitano ukiwemo mmoja utakaozikutanisha baada ya ule wa Machi 8 kuahirishwa na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), huku ikielezwa utapangiwa tarehe nyingine. Kwa Simba, mechi tano zitakazobaki baada ya kumaliza viporo ni dhidi ya KMC, Singida Black Stars, KenGold, Kagera Sugar na Yanga. Upande wa Yanga itakabiliana na Fountain Gate, Namungo, Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Simba. Hii ina maana kuwa kama kila timu itashinda mechi zake zote za kawaida, basi mbio za ubingwa huenda zikaamuliwa na Dabi ya Kariakoo ambayo bado haijafahamika itachezwa lini. Ni muhimu kukumbuka kuwa mechi hiyo ya duru la pili kati ya Simba na Yanga haijapangiwa tarehe. Kwa hali ilivyo huenda mechi ikawa fainali halisi ya kuamua bingwa wa Ligi Kuu. Kama Simba itakuwa na pointi 78 na Yanga 79, basi mshindi wa mechi hiyo atatangazwa bingwa, lakini sare itakuwa faida kwa Yanga.


NAFASI YA KIMATAIFA

Wakati Yanga na Simba zikihaha kuwania taji, vita nyingine kali inaendelea nyuma yao kupigania nafasi ya pili na tatu. Azam FC na Singida Black Stars bado wana nafasi ya kupenya katika nafasi ya pili kama Simba itateleza.

Azam yenye pointi 51 baada ya mechi 26, inakishika nafasi ya tatu. Singida Black Stars ni ya nne na pointi 50. Kwa Simba yenye pointi 57, kama itashindwa kufikisha pointi 63, maana yake ni kwamba Azam au Singida Black Stars inaweza kuichukua nafasi ya pili kwani zina uwezo wa kufikisha pointi hizo ikishinda mechi zao zote.

Lakini kwa namna ambavyo Simba imekuwa ikicheza msimu huu, ni wazi itakuwa ngumu kwao kuipoteza nafasi hiyo kwani ikishinda mechi mbili tu kati ya zile tatu za viporo, basi itazima moja kwa moja ndoto ya Azma na Singida Black Stars kumaliza ligi nafasi ya pili msimu huu.

Simba ikishinda mechi hizo mbili zijazo, itafikisha pointi 53 ambazo Azam nayo ikishinda mechi zake zote zilizobaki itakomea hapo, lakini itabaki nafasi ya tatu kufuatia Simba kuwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kwa sasa Azam na Singida Black Stars, hazina uwezo wa kumaliza ligi nafasi ya kwanza kufuatia Yanga kufikisha pointi 67 ambazo haziwezi kufikiwa na timu hizo, hivyo vita ya ubingwa imebaki kwa Yanga na Simba pekee.

Ikiwa hivyo, vita itabaki kwa Azam na Singida Black Stars kuwania nafasi ya tatu ambayo hutoa tiketi ya moja kwa moja kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Azam kwa sasa hesabu zao kubwa ni kuhakikisha haitoki hapo ilipo ili kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, inafahamu kwamba ikimaliza ligi ya nne, basi itakuwa haina uhakika wa kucheza kimataifa, itasubiri matokeo ya fainali ya Kombe la FA itakuwaje.

Ipo hivi; kwa sasa Tanzania ina nafasi ya kuingiza timu nne kwenye michuano ya kimataifa, mbili Ligi ya Mabingwa na nyingine Shirikisho.

Timu mbili zitakazomaliza nafasi za juu kwenye ligi, zinakwenda kushiriki Ligi ya Mabingwa, huku bingwa wa Kombe la FA na itakayomaliza nafasi ya tatu kwenye ligi ndiyo wawakilishi wa Tanzania Kombe la Shirikisho.

Endapo bingwa wa FA ndiye bingwa wa ligi, basi timu itakayopoteza mchezo wa fainali Kombe la FA, itachukua nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho, lakini ikitokea zote zilizoingia fainali ndizo zenye tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa, basi timu inayomaliza ligi nafasi ya nne itapewa tiketi hiyo.

Kwa sasa michuano ya Kombe la FA ipo hatua ya robo fainali, Azam imeondolewa, wakati Singida Black Stars inaendelea kupambana, hivyo inabaki kuwa mtego kwa Azam wakati Singida Black Stars inafahamu kuingia tu kwake fainali kwenye michuano hii, itajihakikishia nafasi hiyo. Ikitokea Singida Black Stars imeingia fainali na timu nyingine tofauti na Simba na Yanga, hapo niwazi Azam itaikosa nafasi ya uwakilishi wa nchi kimataifa. Mbali na Simba, Yanga na Singida Black Stars zilizopo robo fainali ya Kombe la FA, zingine ni Mbeya City, Stand United, JKT Tanzania, Kagera Sugar na Pamba Jiji.


MASKINI KENGOLD

Katika upande mwingine wa msimamo, hali ni tete kwa timu zilizo kwenye nafasi ya chini. Vita ya kubaki Ligi Kuu ndiyo yenye hofu zaidi kwani huchukua majira yote ya msimu, lakini husababisha vilio na furaha mwishoni.

Kuanzia nafasi ya tano inayoshikwa na Tabora United, hadi ile ya 16, hakuna aliye salama kabisa. Yeyote anaweza kushuka, kama si moja kwa moja, basi kupitia mechi za mtoano. Hivi sasa KMC ambayo ipo kwenye mstari wa kucheza mechi za mtoano ikiwa na pointi 27, kama itashinda mechi tano zilizobaki itafikisha pointi 42 na kuipikua Tabora United kama itapoteza zote.

Timu zilizo kwenye hatari hiyo na pointi zao kwa sasa ni Tabora United (37), Dodoma Jiji (34), JKT Tanzania (32), Mashujaa (30), Fountain Gate (29), Coastal Union (28), Namungo (28), Pamba Jiji (27), KMC (27), Tanzania Prisons (24), Kagera Sugar (22) na KenGold (16). 

Kengold FC, waliopanda Ligi Kuu msimu huu, ndio wanaonekana kama timu ya kwanza kushuka daraja. Wakiwa na pointi 16 katika michezo 26, wamebakiwa na mechi nne tu dhidi ya Coastal Union, Pamba Jiji, Simba na Namungo.  Kama watapoteza mechi mbili mfululizo zijazo, itakuwa rasmi imeshuka daraja kwani haitakuwa na uwezo wa kumaliza ligi hata nafasi ya 14 ambayo ingeweza kuwapa mwanya wa kucheza mechi za mtoano kuepuka kushuka daraja. Kwa upande mwingine, timu kama Kagera Sugar, Tanzania Prisons na KMC zinahitaji kujitetea kwenye michezo yao ili kuondoka kwenye mstari wa hatari wa kushuka daraja. Kagera kwa sasa ipo kwenye mstari mwekudnu wa kushuka, huku Tanzania Prisons na KMC zikikamata nafasi za mtoano.


WASIKIE WADAU

Kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Gwambina, Mohamed Badru anasema: “Ligi msimu huu imekuwa ngumu kwa namna ambavyo ushindani umekuwa mkubwa kutoka timu za juu hadi zile zinazopambana kutoshuka daraja.

Kitu kizuri zaidi ni namna ambavyo timu kama Yanga na Simba zimeonyesha ubora kwa kushinda michezo mingi, lakini vilevile Azam na Singida Black Stars walivyoleta changamoto, hasa katika mzunguko wa kwanza.

Hili ni jambo zuri kwa maendeleo ya soka letu, maana linaamsha ari na ushindani wa kweli.”

Naye nyota wa zamani wa Yanga, Credo Mwaipopo anasema: “Hii ni Ligi bora. Kikubwa watendaji wa Bodi ya Ligi waongeza juhudi kwenye masuala ya upangaji ratiba na uboreshaji wa viwanja, tunaweza kuzifikia Ligi za Afrika Kaskazini katika miaka michache ijayo.”