Prime
PUMZI YA MOTO: Japo FIFA inataka Saa 72 za mapumziko, kwa Ligi Kuu Bara tunahitaji muda zaidi

Muktasari:
- Moja ya maeneo yanayotoa picha hiyo ni ratiba ya mechi.
- Hii imekuwa changamoto kubwa kwa miaka mingi, ikianza na viporo na sasa kuna tatizo lingine kubwa ndani yake.
LIGI Kuu Bara inazidi kukua kila uchao lakini bahati mbaya sana uendeshaji wake haukui au unarudi nyuma.
Moja ya maeneo yanayotoa picha hiyo ni ratiba ya mechi.
Hii imekuwa changamoto kubwa kwa miaka mingi, ikianza na viporo na sasa kuna tatizo lingine kubwa ndani yake.
Tatizo hilo ni mechi kurundikana ndani ya muda mfupi bila kutoa muda wa wachezaji kupumzika.
Hili ni tatizo baya kuliko hata viporo kwa sababu linakwenda kuathiri afya za wachezaji wetu moja kwa moja.
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), hutaka angalau kuwe na saa 72 za wachezaji kupumzika, kutoka mechi moja hadi nyingine.
Lakini Bodi ya Ligi (TPLB) huwa hawaliangalii hata kidogo.
Wao hupanga ratiba kwa bila kujali saa 72 kutoka mechi moja hadi nyingine, umbali ambao timu itasafiri na off course hata ugumu wa mpinzani.
Nitatoa mfano wa Azam hivi karibuni. Aprili 3 walikuwa Mbeya kwenye Uwanja wa Sokione kucheza na KenGold. Aprili 6 wakatakiwa kuwa Singida kwenye Uwanja wa Liti kucheza na Singida Black Stars.
Hii ni kinyume cha matakwa ya FIFA ya angalau saa 72 kutoka mechi moja hadi nyingine.
Hizi saa 72 ambazo FIFA wanazitaka, ni muda wa katikati ambao mchezaji atapumzika.
Yaani mchezaji anapaswa kupumzika kwa saa 72 kabla hajacheza mechi nyingine.
Lakini kutoka tarehe 3 hadi 6 ni chini ya saa 72.
Lakini zaidi ya hapo, Azam walitakiwa kusafiri kutoka Mbeya hadi Singida, ndani ya huo muda ambao wachezaji walipaswa kupumzika.
Kutoka Mbeya hadi Singida ni zaidi ya kilomita 600, na ni safari ya barabarani ya zaidi ya saa 10.
Singida hakuna uwanja wa ndege, hivyo ukipanda ndege itakubidi ushukie Dodoma.
Hata hivyo, hakuna safari ya ndege kutoka Mbeya hadi Dodoma, hata kama ungetamani kwenda na ndege.
Kwa hiyo ni lazima tu utumie zile saa zaidi ya 10 za barabarani kuzikata hizi kilomita zaidi ya 600.
Pata picha, wachezaji ambao walitakiwa wapumzike kwa saa 72, hawakupumzika...na bado inawabidi wasafiri kwa saa 10 barabarani.
Haya ni mateso ya hali ya juu sana.
Aprili 10 Azam wakatakiwa kuwa Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Azam Complex kuwakaribisha Yanga.
Angalau hapa walipata hizo saa 72, lakini hata hivyo, hebu angalia hiyo ratiba.
Singida, Azam na Yanga ndiyo timu zinazounda lile kundi la Big 4, ikiwamo Simba.
Kuwa na mechi mfululizo dhidi yao, katika mazingira ya kuchoshana kama haya, sio sawa.
Hii sio kwa Azam peke yao. Haya ndiyo maisha ya kawaida kwa timu zote za Tanzania.
Msimu uliopita, Kagera Sugar walianzia Kigoma dhidi ya Mashujaa, Agosti 15.
Agosti 18 wakapelekwa Mbalali kucheza na Ihefu...hebu dhania.
Bodi ya ligi wanapanga ratiba utadhani wao hawapo nchini hivyo hawajui jiografia ya nchi yetu.
Japo FIFA wanapendekeza saa 72 kwa wachezaji kupumzika, lakini Tanzania tunahitaji zaidi ya hizo saa 72.
Tanzania ni nchi kubwa yenye uhaba wa miundombinu, usafiri wake ni mgumu sana.
Wachezaji wetu wanacheza kwenye viwanja vigumu sana...na programu za kurudisha miili katika hali ya kawaida ni duni sana.
Hapo bado hujazingatia lishe na tiba kwa wachezaji wetu.
Naam, FIFA wanapendekeza saa 72, lakini sisi tu tunahitaji zaidi ya hizo.
Hii ni kwa sababu FIFA wanapotunga sheria zao huangalia mazingira ya Ulaya na nchi zilizoendelea.
Kupanga ratiba isiyozingatia mzingira yetu ni kukosa umahiri katika majukumu.
KWA NINI FIFA WANATAKA SAA 72?
Shirikisho la soka la kimataifa, FIFA, linapendekeza angalau saa 72 za kupumzika kwa wachezaji kutoka mechi moja hadi nyingine.
Hii ni ili kulinda afya za wachezaji kuepusha hatari ya majeraha.
Mapendekezo haya ya FIFA yanaungwa mkono na utafiti uliofanywa na chama cha kimataifa cha wachezaji wa soka la kulipwa FIFPro, ambacho ni chama kikubwa zaidi cha wachezaji duniani.
Utafiti huu unaonesha kwamba angalau siku tatu za mapumziko kwa wachezaji zinahitajika kutoka mechi moja hadi nyingine ili kulinda afya za wachezaji.
Zifuatazo ni sababu za msingi zinazofanya saa 72 za mapumziko kuwa muhimu sana kwa wachezaji.
1. Mwili kurejea katika hali ya kawaida:
Mwili wa mchezaji unahitaji muda wa kutosha ili kurejea katika yake ya kawaida baada ya misukosuko ya mechi.
Muda huu husaidia kuponya uchovu na kutibu misuli pamoja na hata vitu vidogo vidogo kama viuvimbe vidogo vidogo ambavyo hutokana na kugongana uwanjani.
Kwa mtu ambaye amecheza mpira, ngazi yoyote ile, anajua hali anayoisikia baada ya mechi au hata mazoezi.
Lakini akipumzika, baadaye anajisikia vizuri. Sasa kwa mpira wa kulipwa ambao matumizi yake ya nguvu huwa makubwa zaidi...wachezaji huhitaji zaidi muda wa kuipumzisha miili ili irudi katika hali yake ya kawaida.
Mchezaji akipata muda huu atakuwa katika hali nzuri ya kuepuka majeraha yenye ushusiano na uchovu.
2. Ufanisi:
Tafiti zinaonesha kwamba wanamichezo wanaweza wasifikie uwezo wa ufanisi wao kwa asilimia mia ndani ya saa 48 na baadhi ya michakato ya kikemia ya miili huchukua hadi saa 72 kukaa sawa.
3. Msimamo wa FIFA:
Mapendekezo ya FIFA ya saa 72 kutoka mechi moja hadi nyingine ndiyo kiwango rasmi cha dunia kwa ajili ya ustawi wa afya za wachezaji.
4. Uhalisia katika utekelezaji:
Wakati mashindano mbalimbali yanaweza kuwa na ratiba zake, mapendekezo ya FIFA husimama kama miongozo kuhakikisha wanakuwa na muda zaidi wa kupumzika.