Makosa ya urembo wanayofanya wanawake bila kujua
Muktasari:
- Mara nyingi makosa haya hutokana na ukosefu wa elimu sahihi ya urembo, kufuata mitindo bila kuelewa, au kutumia bidhaa zisizofaa kwa ngozi au mwili. Mwanaspoti inaangazia baadhi ya makosa hayo na namna ya kuyaepuka ili kufikia mwonekano bora na wa kuvutia zaidi.
KATIKA dunia ya leo ambapo urembo umepewa nafasi kubwa katika maisha ya kila siku, wanawake wengi wamekuwa wakijitahidi kuonekana nadhifu, wenye kuvutia na kujiamini zaidi. Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo, bado kuna makosa ya mara kwa mara yanayofanyika bila kujua, ambayo badala ya kuongeza mvuto, huweza kupunguza uzuri wa asili wa mtu.
Mara nyingi makosa haya hutokana na ukosefu wa elimu sahihi ya urembo, kufuata mitindo bila kuelewa, au kutumia bidhaa zisizofaa kwa ngozi au mwili. Mwanaspoti inaangazia baadhi ya makosa hayo na namna ya kuyaepuka ili kufikia mwonekano bora na wa kuvutia zaidi.
Mwanaspoti ilipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya warembo ambao walielezea sababu hasa zinazoweza kuleta madhara au kuharibu kabisa urembo wa mwanamke.
MATUMIZI YA VIPODOZI
Mwanadada, Rhobi Chacha anasema kuwa, “kosa la kwanza ni kuchagua vipodozi visivyolingana na aina ya ngozi. Wanawake wengi hununua bidhaa kwa sababu zimependekezwa au zinatrend, bila kuzingatia kama zinafaa kwa ngozi yao.”
“Ngozi ya mafuta, kavu au ya mchanganyiko huhitaji huduma tofauti. Kutumia bidhaa isiyofaa kunaweza kusababisha chunusi, muwasho au hata kuharibu ngozi kwa muda mrefu. Ni muhimu kufahamu aina ya ngozi yako kabla ya kuchagua bidhaa yoyote ya urembo.”
MAKE-UP
Mrembo Diana Songa anasema wanawake wengi wanafanya makosa ya kutokuamini kupitia uzuri walionao hasa wanapokwenda maeneo ya watu wengi wakitaka kuwa na mwonekano utakaovuta macho ya watu bila kujua ndivyo wanavyojiharibu.
“Kosa lingine ni kupaka make-up kupita kiasi, wengi huamini kuwa makeup nyingi huongeza uzuri, lakini ukweli ni kwamba matumizi ya kiasi kikubwa yanaweza kufunika uzuri wa asili na kufanya mtu aonekane wa bandia. Urembo wa kweli huonekana zaidi pale unapokuwa rahisi na unaoendana na mazingira husika.
“Pia, kuna tatizo la kutosafisha ngozi ipasavyo, hasa kabla ya kulala. Kulala na makeup ni moja ya makosa makubwa yanayofanywa na wanawake wengi. Hali hii huziba vinyweleo vya ngozi na kusababisha matatizo kama vile chunusi na ngozi kuchoka mapema. Kusafisha ngozi kila siku ni hatua muhimu katika kudumisha afya ya ngozi.
“Kutotumia bidhaa za kulinda ngozi dhidi ya jua ni kosa jingine kubwa. Watu wengi hudharau athari za mionzi ya jua, lakini ukweli ni kwamba jua linaweza kuharibu ngozi kwa kiasi kikubwa, kusababisha mabaka na hata kuharakisha kuzeeka kwa ngozi. Matumizi ya mafuta ya kukukinga yanapaswa kuwa sehemu ya kawaida ya utunzaji wa ngozi.”
MCHANGANYIKO WA VIPAKO
Mwanadada Vicky Mecky anasema kuna makosa hufanyika wakati wa kuchagua rangi kwa wanawake.
“Makosa mengine hujitokeza katika uchaguzi wa rangi za makeup. Kutumia ‘foundation’ isiyoendana na rangi ya ngozi kunaweza kufanya uso uonekane tofauti kabisa na sehemu nyingine za mwili,” anasema na kuongeza:
“Hii hupunguza mvuto na kuleta muonekano usio wa kawaida. Ni muhimu kuchagua rangi inayolingana na ngozi yako ili kupata mwonekano wa asili.”
SIO KILA MTINDO NI WAKO
Akizungumzia suala la mitindo, Olipa Assa anasema: “Kosa jingine ni kufuata kila mtindo unaotokea bila kujiuliza kama unamfaa mtu binafsi. Si kila ‘trend’ inafaa kwa kila mtu. Mwonekano mzuri hutegemea pia umbo la uso, mwili na hata rangi ya ngozi.”
“Ni busara kuchagua mitindo inayokufaa badala ya kuiga kila kinachotokea mitandaoni.”
“Vilevile, matumizi mabaya ya vifaa vya urembo kama brashi na sponge bila kuviosha ni hatari kwa afya ya ngozi. Vifaa hivi hukusanya bakteria ambao wanaweza kusababisha maambukizi ya ngozi. Kusafisha vifaa hivi mara kwa mara ni muhimu sana.
LISHE NA MATUMIZI
Nevumba Abubakar anasema kuwa: “Lishe duni pia ni kosa linalochangia kupungua kwa uzuri wa ngozi. Urembo hauanzi nje tu bali pia ndani ya mwili. Kula vyakula vyenye virutubisho kama matunda, mboga mboga na kunywa maji ya kutosha husaidia ngozi kuwa na afya na mng’ao wa asili.
KUTOJIAMINI
Jesca Lunyali anasema: “Kukosa kujiamini ni kosa kubwa ambalo halionekani moja kwa moja lakini linaathiri urembo kwa kiasi kikubwa. Mwanamke anaweza kuwa na makeup nzuri na mavazi ya kuvutia, lakini bila kujiamini, uzuri huo hauwezi kuonekana kikamilifu. Urembo wa kweli unaanza na jinsi unavyojihisi wewe mwenyewe ndani.
“Urembo si suala la kutumia bidhaa nyingi au kufuata kila kinachotokea, bali ni kuelewa mwili wako, ngozi yako na kile kinachokufaa. Kuepuka makosa haya ya kawaida kutakusaidia kuonekana nadhifu, mwenye afya na kuvutia kwa njia ya asili zaidi.