Mastaa hawa wanajitafuta upya Championship
Muktasari:
- Hii ni kutokana na baadhi ya mastaa wakiwamo wakongwe walivyogawana vipande kila mmoja akisaka riziki na maisha katika soka na kuendeleza vipaji vyao huku wakisikilizia pakutokea.
BAADA ya kupotea kwenye Ligi Kuu Bara, baadhi ya mastaa waliowahi kutesa katika timu mbalimbali zikiwamo Simba na Yanga, wameanza kujitafuta upya wakikipiga Ligi ya Championship kurejesha makali yao.
Hii ni kutokana na baadhi ya mastaa wakiwamo wakongwe walivyogawana vipande kila mmoja akisaka riziki na maisha katika soka na kuendeleza vipaji vyao huku wakisikilizia pakutokea.
Mwanaspoti linakuletea baadhi ya nyota waliowahi kutesa ndani na nje ya Tanzania katika timu kubwa ambao sasa wanakiwasha kwenye Ligi ya Championship msimu huu wa 2026-2027 wakiwa tegemeo la kuzipandisha timu hizo kucheza Ligi Kuu.
KELVIN YONDANI - KENGOLD
Beki huyu aliyekuwa moto akiitumikia Yanga, Simba na Taifa Stars, kwa sasa ndiye nyota mwenye jina kubwa kikosini huku pia akiwa na uzoefu kwenye soka.
Yondani aliyecheza kwa muda mrefu Ligi Kuu Bara akiwa na Simba kuanzia 2006 hadi 2012 kisha akahamia Yanga aliyoitumikia hadi 2020, amewahi kuitumikia Polisi Tanzania, Geita Gold na sasa anakipiga KenGold, tayari ameisaidia timu hiyo kuvuna pointi nne kwenye mechi mbili.
ABDALLAH SHAIBU ‘NINJA’ – IAA
Hakuna asiyekumbuka zile ‘tackling’ na kasi uwanjani kipindi akikipiga Yanga na kuwa moja ya nyota waliokuwa wakitumainiwa kwenye eneo la beki wa kati. Ninja kwa sasa anakipiga IAA ya jijini Arusha.
Ninja aliyehudumu kwa ‘Wananchi’ kwa nyakati tofauti akiingia kwa mara ya kwanza 2017, tangu alipoondoka kikosini humo 2023 akitimkia DR Congo kujiunga na FC Lubumbashi, kisha St-Éloi Lupopo, ni kama alipotea, lakini IAA imemuibua upya ikimuonesha njia ya kurejea tena kwenye medani za soka.
Pia Ninja amewahi kucheza nje ya Afrika katika timu za MFK Vyskov ya Czech Republic na LA Galaxy II ya Marekani.
Pia kikosi hicho kinao nyota wengine akiwamo kipa Benedict Haule aliyewahi kuitumikia Tanzania Prisons na Singida Black Stars, Aron Kalambo na beki Joram Mgeveke wote wakisaka upya kurudi juu kisoka.
GEOFREY MWASHIUYA - BIGMAN
Tangu alipoondoka Yanga misimu zaidi ya nane sasa, kiungo huyo alikuwa akihama timu tofauti akicheza Kagera Sugar na DTB, kabla ya kutoonekana kwenye soka la ushindani.
Kwa sasa nyota huyo ameibukia Bigman (zamani Mwadaui) ya jijini Tanga na katika mechi mbili alizocheza, anatajwa kuonyesha kiwango bora, huku kocha wake, Omary Kapilima akimtabiria kurudi Ligi Kuu haraka.
Mbali na staa huyo, wengine ni Nourdine Balora raia wa Burikina Faso aliyewahi kucheza timu kadhaa zikiwamo Biashara United na Namungo, huku akitokea timu ya Ligi Kuu nchini kwao, Etoile Filante.
MAKAPU & ADEYUM - MBUNI
Said Juma Makapu si mchezaji mpya kwenye masikio ya wana soka nchini, akikumbukwa zaidi kwenye ubora wake alipokuwa akikipiga Yanga kabla ya kuhamia timu zingine zikiwemo Ihefu na Mashujaa.
Kwa sasa kiungo huyo mkabaji mwenye uwezo pia wa kucheza beki wa kati anakiwasha Mbuni FC ya jijini Arusha akiungana na nyota wengine akiwemo kipa David Kisu aliyewahi kucheza Simba, Toto Africans, Singida United, Azam, Namungo, KMC, Biashara na Gor Mahia ya Kenya.
Pia kuna Adeyum Salehe aliyecheza Yanga, Dodoma Jiji na Geita Gold.
Hata hivyo, licha ya timu yao kutoanza vyema kwa kupoteza mechi zote mbili walizocheza Championship, lakini uwepo wa nyota hao unatoa hamasa na nguvu wakiamini lolote linawezekana.
DICKSON AMBUNDO - MBEYA KWANZA
Winga huyu mwenye uwezo na uwepesi mguuni awapo na mpira, hakuna asiyemfahamu katika soka, tangu akiwa na kikosi cha Nyamagana United, Alliance FC kabla ya kung’ara zaidi na Yanga.
Tangu alipomaliza mkataba wake Yanga alipotolewa kwa mkopo Dodoma Jiji, nyota huyo alipotea ghafla na sasa ni moja ya wanaojitafuta tena kupitia Mbeya Kwanza (Tabora United).
Nyota huyo anaungana na wengine waliowahi kuwasha moto Ligi Kuu akiwamo Joseph Mahundi aliyepita timu za Mbeya City, Ihefu (kwa sasa Singida Black stars) na Azam FC.
SESEME NA MAGULI - RHINO RANGERS
Kiungo Abdallah Seseme aliyewahi kuhudumu Simba na Kagera Sugar, kwa sasa yupo Rhino Rangers na kazi yake imeshaonekana akiipa pointi nne timu hiyo katika mechi mbili.
Mbali na kiungo huyo, straika aliyewahi kuvuma ndani na nje ya Tanzania akicheza soka la kulipwa, Elias Maguli ameanza kampeni mpya ya kusaka heshima kurudi Ligi Kuu akiitumikia timu hiyo ya mjini Tabora.
Maguli alishacheza soka Ligi Kuu nchini Oman akiwa na kikosi cha Dhofar, pia alicheza Simba, Stand United, Tanzania Prisons, Polisi Tabora na Ruvu Shooting, kwa sasa anakiwasha Rhino Rangers.
Katika mechi mbili walizocheza mastaa hao pamoja na kipa wa zamani wa Mbeya City na TRA United, Haroun Mandanda wameshinda moja dhidi ya Tanzania Prisons bao 1-0 na sare dhidi ya Songea United.
UGANDO & LOMALISA – BANDARI TANZANIA
Kila kijiji na wazee wake, ndivyo walivyofanya Bandari Tanzania kuwarejesha nyota waliotamba Ligi Kuu kwa kuwasainisha Haji Ugando aliyewahi kucheza Simba na Joyce Lomalisa nyota wa zamani wa Yanga.
Mbali na nyota hao, wapo wengine kadhaa kama Sixtus Sabilo, Ally Ramadhan, Issa Ngoah na Seleman Omary ‘Boban’ ambao walishatumika Ligi Kuu katika timu tofauti.
KAULI ZA WADAU
Helbert Mtete anasema kwa sasa mpira umebadilika na wachezaji wengi wanatafuta masilahi na wapo ambao wanaikataa Ligi Kuu kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni ushindani na malipo kiduchu.
“Kuna timu za Championship zinalipa vizuri lakini pia mchezaji anakuwa na uhakika wa namba kikosini, kwa maana hiyo wengine wanakuja kwa malengo yao ndio maana wapo nyota wa kigeni kwenye ligi hiyo,” amesema Mtete.
Salim Seleman anasema kila timu inayo malengo yake kwenye ligi, hivyo uwekezaji wa wachezaji mastaa unalenga kuitangaza timu husika na Championship kwa jumla kutokana na historia iliyopo kwenye soka la Tanzania.
“Wachezaji wengi wa kigeni wanatamani sana kucheza soka la Tanzania kwakuwa wanafahamu mazingira mazuri na hamasa wanayopata kwa mashabiki, ndio maana unaona wengine wakifika hawataki kurudi kwao,” amesema Seleman.