Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Michezo iwe injini mpya ya ajira kwa vijana

SPORTS BIZ Pict

Muktasari:

  • Tunawahitaji wahasibu, wanasheria, wataalamu wa afya na lishe, wachambuzi wa takwimu, wapiga picha, wahariri wa video, wabunifu, watangazaji, wasimamizi wa matukio na wataalamu wa teknolojia. Pia kuna nafasi katika usafiri, malazi, usalama, chakula na uuzaji wa vifaa vya michezo.

UKIMUULIZA kijana kuhusu kazi katika michezo, huenda akataja mchezaji, kocha au mwamuzi. Hizo ni taaluma muhimu, lakini ni sehemu ndogo tu ya kazi zinazoweza kupatikana. Nyuma ya mechi, klabu na mashindano kuna watu wengi wanaotoa huduma ambazo bila wao michezo haiwezi kuendeshwa vizuri.

Tunawahitaji wahasibu, wanasheria, wataalamu wa afya na lishe, wachambuzi wa takwimu, wapiga picha, wahariri wa video, wabunifu, watangazaji, wasimamizi wa matukio na wataalamu wa teknolojia. Pia kuna nafasi katika usafiri, malazi, usalama, chakula na uuzaji wa vifaa vya michezo.

Hapo ndipo Tanzania inapaswa kubadili mtazamo. Si kila kijana mwenye shauku ya michezo atakuwa mchezaji wa kulipwa. Lakini anaweza kujenga kazi au biashara inayohudumia wachezaji, shule, mashabiki, klabu na jamii. Soko hilo linaweza kufikiwa kwa ujuzi tofauti, si kwa kipaji cha kucheza pekee.

Mhitimu wa uhasibu anaweza kusaidia akademi kuandaa bajeti na taarifa za fedha. Mtaalamu wa masoko anaweza kubuni kampeni za udhamini. Mwanasheria anaweza kusaidia mikataba ya wachezaji na masuala ya haki miliki. Mtaalamu wa programu anaweza kutengeneza mfumo wa usajili wa mashindano, tiketi au takwimu za wachezaji.

SPORT 01

Vyuo vina nafasi muhimu ya kuunganisha elimu na soko hili. Badala ya mafunzo kwa vitendo kufanyika katika ofisi za kawaida pekee, wanafunzi wa biashara, sheria, TEHAMA na mawasiliano wanaweza kufanya miradi inayosaidia klabu na waandaaji wa mashindano. Kwa njia hiyo, taasisi za michezo zinapata msaada huku vijana wakijenga uzoefu unaoweza kuuzwa sokoni.

Ujasiriamali wa michezo unaweza kuanza kwa mtaji mdogo. Kijana anaweza kuandaa mashindano ya mtaa kwa kufuata taratibu, kuuza huduma za upigaji picha au kutengeneza taarifa za michezo ya jamii. Akipata wateja na kusimamia vizuri mapato, biashara yake inaweza kukua hatua kwa hatua.

Mahitaji halisi yapo. Mashindano mengi ya jamii hukabiliwa na changamoto za ratiba, usajili, takwimu, matangazo na udhamini. Mjasiriamali anayeweza kutatua changamoto hizi kwa gharama nafuu anaweza kupata wateja. Shule nazo zinahitaji makocha wenye uwezo, vifaa salama na waandaaji wa mashindano.

Teknolojia imerahisisha kuingia kwenye baadhi ya kazi hizo. Simu janja na intaneti vinaweza kumwezesha kijana kuripoti matokeo ya ligi ya eneo lake, kufanya uchambuzi au kutangaza vipaji. Hata hivyo, mtandao wenye wafuasi wengi hauhakikishi mapato. Ubora, uaminifu na mpango wa biashara ni lazima.

Kabla ya kukopa ili kuanzisha biashara ya michezo, kijana ajibu maswali ya msingi: wateja ni akina nani, watahitaji huduma mara ngapi, watakuwa tayari kulipa kiasi gani, na gharama za kutoa huduma ni zipi? Utafiti mdogo wa soko unaweza kuzuia hasara kubwa.

SPORT 03

Benki, taasisi za mikopo na programu za vijana zinaweza kutoa elimu ya fedha, ushauri na ufadhili unaoendana na uwezo wa biashara. Mkopo si mafanikio yenyewe; biashara inayoweza kulipa gharama na kuendelea kutoa huduma ndiyo mafanikio.

Halmashauri zinaweza kusaidia kwa kutenga viwanja salama na kuweka taratibu zinazoeleweka za kufanya shughuli za michezo. Gharama kubwa za kutumia maeneo zinaweza kuwazuia wajasiriamali wachanga kujaribu mawazo yao. Ushirikiano kati ya serikali za mitaa, shule na sekta binafsi unaweza kupunguza kikwazo hicho.

Tusijikite Dar es Salaam pekee. Dodoma, Mwanza, Mbeya, Arusha, Morogoro na maeneo mengine yana shule, mashabiki na jamii zinazohitaji huduma. Kila mkoa unaweza kukuza shughuli zinazolingana na uwezo na mahitaji yake. Vijana wa kike na wenye ulemavu nao wanapaswa kupata fursa sawa za mafunzo na biashara.

Hatua ya mwisho ni kupima ajira zinazozalishwa. Tunahitaji taarifa kuhusu ajira za kudumu, za muda na kujiajiri katika shughuli za michezo. Bila takwimu hizo, sekta inaweza kuendelea kuonekana ndogo kuliko mchango wake halisi.

Kazi hizi zinahitaji ujuzi unaoonekana kwa vitendo. Kijana anayesema anaweza kusimamia mitandao ya klabu aonyeshe ratiba ya maudhui, mfano wa kampeni na namna atakavyopima matokeo. Anayetaka kuwa mchambuzi wa takwimu aanze kwa kurekodi matokeo na matukio ya mashindano ya jamii kwa usahihi. Kazi ndogo inayofanywa vizuri inaweza kuwa ushahidi wa uwezo mbele ya mteja mkubwa.

Vyuo na taasisi za mafunzo vinaweza kushirikiana na klabu kuanzisha miradi ya miezi michache yenye matokeo yanayopimika. Wanafunzi wa uhasibu watengeneze mfano wa bajeti, wa sheria wapitie masuala ya mikataba chini ya usimamizi na wa mawasiliano waandae mpango wa kuwafikia mashabiki. Ushirikiano huo uwe na malengo, wakufunzi na tathmini ili usigeuke ajira isiyolipwa bila kujifunza.

SPORT 02

Jambo muhimu ni kuelewa kwamba si kila shabiki ni mteja anayeweza kulipa. Kabla ya kuanzisha kampuni ya picha za michezo, kijana afanye mazungumzo na shule na waandaaji wa ligi ili kujua mahitaji yao. Anaweza kuanza kwa huduma moja iliyo wazi, makubaliano ya maandishi na bei inayojumuisha muda wa kazi na gharama za vifaa. Utaratibu huu humsaidia kutofautisha shauku na soko.

Programu za kukuza ajira zikiangalia michezo zisijikite kwenye kutoa vifaa pekee. Vijana wanahitaji pia mafunzo ya kutunza kumbukumbu, huduma kwa wateja, usalama wa watoto, maadili ya picha na utoaji wa huduma kwa wakati. Mjasiriamali mwenye kamera nzuri lakini asiyeheshimu makubaliano anaweza kupoteza wateja. Ujuzi wa biashara na uaminifu huamua kama kipaji kinaweza kuleta kipato endelevu.

Hatimaye, wazazi na walimu wanaweza kuwasaidia vijana kuona njia nyingi za kazi katika michezo. Kijana anayeipenda soka lakini hana nafasi ya kuwa mchezaji anaweza kusomea udaktari, TEHAMA, masoko au sheria na kuingia sekta hii baadaye. Tusifunge ndoto za vijana kwenye kufunga mabao pekee; tujenge mazingira ya kila ujuzi kupata nafasi ya kushiriki uchumi wa michezo.

Kila hatua inaweza kuandikwa kwenye jalada la kazi, ili mteja aone maendeleo ya kijana na matokeo ya huduma zake. Hilo huongeza uaminifu.

Tanzania haiwezi kuwafanya vijana wote kuwa nyota wa soka. Lakini inaweza kuwasaidia wengi kuwa watoa huduma na wamiliki wa biashara zinazozunguka michezo. Badala ya kuuliza ‘nitapataje nafasi ya kucheza?’, vijana wengi zaidi wanaweza kuuliza ‘ni tatizo gani kwenye michezo ninaweza kulitatua na kulipwa?’ Hapo ndipo michezo inaweza kuwa injini ya ajira.

Gastor Hilary Mtweve

Mchambuzi wa Uchumi wa Michezo na Mikakati ya Biashara