Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mikasa ya Edmundo 'The Animal'

EDMUNDO Pict

Muktasari:

  • Kama ilivyotarajiwa, mshambuliaji huyo wa zamani wa Brazil alikuwa ameandaa sherehe kubwa, hata akawaleta wasanii wa sarakasi ndani ya bustani yake. Wanaharakati wa haki za wanyama walikasirika, lakini Edmundo alisimama kidete akidai kwamba hakuvuka mipaka yoyote.

BRASILIA, BRAZIL: NI katika sherehe ya siku ya kwanza ya kuzaliwa ya mwanawe, mmoja wa wanasoka maarufu zaidi duniani aliyezua gumzo kwa kumpa bia na whisky sokwe aitwaye Pedrinho, aliyekuwa amevalishwa tracksuit. Hilo linaweza kuonekana kuwa ni jambo la ajabu sana, lakini siyo kwa Edmundo, mchezaji aliyepewa jina la utani “The Animal” yaani Mnyama.

Kama ilivyotarajiwa, mshambuliaji huyo wa zamani wa Brazil alikuwa ameandaa sherehe kubwa, hata akawaleta wasanii wa sarakasi ndani ya bustani yake. Wanaharakati wa haki za wanyama walikasirika, lakini Edmundo alisimama kidete akidai kwamba hakuvuka mipaka yoyote.

Hilo ni moja tu ya matukio mengi ya utata yaliyomhusu Edmundo. Katika maisha yake ya soka, hakugombana tu na makocha na wachezaji wenzake, bali pia alihusika katika ajali mbaya ya gari iliyoua watu watatu, aliiacha timu yake ili kuhudhuria Carnival ya Rio, na aliingia katika uhasama mkali na mshambuliaji mwenzake wa Brazil enzi hizo, Romario De Souza.

EDMUN 01

Jina lake la utani “The Animal” lilistahili kabisa, na lilibuniwa na mtangazaji Osmar Santos wakati wa mechi kati ya Palmeiras na Guarani 1993.

Akizungumzia jina lake hilo la kipekee, Edmundo anasema: “Bila shaka lina maana chanya na hasi. Ukilinganisha na majina mengine kama ‘The Phenomenon’ au ‘The Emperor’, huenda langu likawa na utata zaidi. Lakini langu ni la kipekee.”

Nyota huyo alizaliwa na kukulia Niteroi karibu na Rio de Janeiro. Edmundo Alves de Souza Neto anajulikana kwa jina la Edmundo. Lakini alifanya nini hasa hadi kupata jina hilo? Alikuwa mchezaji mwenye kasi, kipaji kiufundi, nguvu na akili, ambaye aliboresha uwezo wake kupitia futevolei, aina ya mpira wa wavu wa ufukweni unaochezwa kwa miguu. Hata hivyo, pia alikuwa maarufu kwa hasira zake kali.

EDMUN 02

Katika kipindi cha miaka 17, Edmundo alizichezea timu 13 tofauti, mara nyingi akiondoka katika mazingira ya utata. Alianza maisha yake ya soka Vasco da Gama 1991, lakini baada ya miaka miwili alihamia Palmeiras ambako mara kwa mara aligongana na kocha Wanderley Luxemburgo.

Hatimaye alifukuzwa baada ya kupigana na mchezaji mwenzake Antonio Carlos. Katika mahojiano 2017 kwenye kipindi cha ESPN Bola da Vez, Carlos alimpa Edmundo alama “10 kama mchezaji na sifuri kama binadamu”, akifichua kuwa hizo zilikuwa pande zote mbili zinazomhusu.

Kwa ujumla, Edmundo alifunga mabao 10 katika mechi 39 alizoichezea Brazil, lakini kwa utata mkubwa aliachwa nje ya kikosi kilichoshinda Kombe la Dunia 1994, na mara nyingi alishindwa kuwatoa kikosini magwiji kama Bebeto, Romario na Ronaldo.

Baadaye alijiunga na Flamengo ambapo 1995 yeye na Romario walitoa wimbo wa rap ulioitwa Rap Dos Bad Boys, uliokuwa ukionya watu dhidi ya kuleta matatizo. Moja ya ujumbe wao ulikuwa: “Usilete matatizo.”

Kufikia wakati huo, Edmundo na Romario walikuwa maarufu kwa mchezo wao mgumu na maisha ya starehe yaliyopita kiasi. Wakati mgumu zaidi katika maisha ya Edmundo ulifika Desemba 1995 alipokuwa akiichezea Flamengo.

EDMUN 03

Baada ya kutoka usiku wa manane, alikuwa akiendesha Jeep Cherokee iliyogongana na gari aina ya Fiat wakati wa Carnival ya Rio, na kusababisha vifo vya watu watatu akiwemo mwanamke aliyekuwa abiria wake. Mwanzoni alipatikana na hatia ya kuua bila kukusudia na kuhukumiwa kifungo cha miaka minne na nusu gerezani. Hata hivyo, kutokana na rufaa mbalimbali, muda wake gerezani ulikuwa mfupi sana.

Akikumbuka tukio hilo 2012 baada ya Mahakama Kuu Brazil kuamua kuwa kesi yake imefutwa kwa sababu muda wa kisheria ulikuwa umeisha, alisema: “Hii inaweka mwisho wa jambo ambalo limenisumbua kwa miaka 15. Nina furaha, lakini dhamira yangu bado inabeba ukweli kwamba mateso ya familia za wanaoteseka hayatakwisha kamwe. Lazima niendelee na maisha yangu lakini siwezi kusahau kilichotokea.”

Maisha yake Flamengo yalikuwa mafupi, kwani alitafuta mwanzo mpya Corinthians, lakini akaondoka kabla hata ya kucheza mechi yoyote kutokana na uvumi wa ugomvi katika mazoezi. Baadaye Edmundo alihamia Ulaya na kujiunga na Fiorentina 1998, ambapo alicheza pamoja na nyota kama Rui Costa na Gabriel Batistuta.

EDMUN 04

Licha ya kipaji chake, migogoro iliendelea, ikiwemo mabishano na wachezaji wenzake pamoja na migongano na kocha Giovanni Trapattoni.

Tukio maarufu zaidi lilitokea msimu wa 1998-99 wakati Fiorentina ilikuwa inaongoza Serie A.

Edmundo alitumia kifungu maalumu katika mkataba wake kilichomruhusu kuhudhuria Carnival ya Rio, na akarudi Italia siku mbili baada ya muda uliokubaliwa, jambo lililowakasirisha wachezaji wenzake. Aliporejea, Trapattoni alimwambia wazi: “Ni wakati wa kuacha upuuzi. Ni wakati wa kukua na kuwa mtu mwenye wajibu kwa sababu bila kutumia akili yako vizuri hutafika mbali licha ya kipaji chako.”

Lakini, nyota huyo hakusikia ushauri huo. Kwanza, aliondoka klabuni Aprili 1999. Pili, aliingia katika mgogoro wa muda mrefu na rafiki yake wa zamani Romario ambao kwa haki unaweza kusema Romario ndiye aliyeuanzisha. Akiwa amekasirishwa na uteuzi wa Edmundo katika kikosi cha Kombe la Dunia cha Brazil 1998 wakati yeye aliachwa nje kutokana na jeraha la misuli ya mguu na migogoro na viongozi wa timu, Romario aliweka picha ya kumdhalilisha Edmundo nje ya vyoo katika baa yake huko Rio.

Akizungumzia mchoro huo, Edmundo anasema: “Nilimpigia simu kumuuliza maelezo. Hakunishawishi. Kwa sababu hiyo niliamua kumaliza urafiki wetu.” Kisha likaja tukio maarufu la “chimp-gate”.

Licha ya uhusiano wao mbaya, Edmundo na Romario walipocheza pamoja Vasco da Gama 1999 walikuwa tishio kubwa. Hata dhidi ya Manchester United katika Kombe la Dunia la Klabu 2000, ambapo kikosi cha Sir Alex Ferguson ambacho kilikuwa kimeacha kushiriki FA ili kuhudhuria mashindano hayo, kilichapwa mabao 3-1 na kutolewa.

EDMUN 05

The Animal alikata pasi dhaifu ya kurudisha nyuma kutoka kwa Gary Neville na kumzawadia Romario bao la kwanza. Romario akafunga la pili baada ya kosa jingine la aibu kutoka kwa Neville. Kisha Edmundo akafunga bao la ajabu sana – moja ya mabao bora zaidi katika historia ya mashindano hayo kwa kuunyanyua mpira kwa mguso wa aina ya Maradona kumkwepa Mikael Silvestre, kisha akamzunguka na kumshinda kipa Mark Bosnich.

Kwa upande wa soka, mambo yaliendelea kuwa magumu kwa Edmundo. Alifukuzwa katika kikosi cha Vasco Da Gama na makamu wa rais wa klabu Eurico Miranda kutokana na matatizo ya kinidhamu, na katika miaka minane iliyofuata alipitia vipindi 11 katika klabu mbalimbali za Brazil, Italia na Japan. Alipostaafu 2008, alikuwa ameichezea Vasco mara tano tofauti. Kwa ujumla alifunga mabao 177 katika mechi 377.

Uhusiano wake na Vasco Da Gama pamoja na Palmeiras ulikuwa wa kushangaza lakini wa kuvutia aliouelezea hivi, “ninaipenda Vasco kama mama yangu; nilizaliwa hapo. Palmeiras ni kama mke wangu. Siwezi kusema nampenda mama yangu zaidi au mke wangu zaidi.”

Maisha ya Edmundo nje ya uwanja yalibadilika na kuwa mazuri zaidi alipokuwa mchambuzi wa soka katika televisheni za Brazil. Hata hivyo hakuna mengi yanayojulikana kuhusu maisha yake ya sasa, lakini jambo moja ni hakika kwamba mchezaji huyo mwenye tabia za kulipuka aliacha alama kubwa katika soka, ndani na nje ya Brazil.