Prime
Mtego wa TFF unavyosaka 'mchawi' wa Ligi Kuu Bara
WAKATI Ligi Kuu Bara ikienda ukingoni, kuna vita nyingi kila kona, upande wa kumpata Mchezaji Bora wa Msimu (MVP), ni sehemu inayotazamiwa zaidi, kutokana na viwango bora vya wachezaji wa timu mbalimbali hadi sasa.
Mchezaji Bora wa Ligi Kuu huchaguliwa na Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuzingatia mchango mkubwa uwanjani, takwimu binafsi, ushawishi kwenye timu, nidhamu na uthabiti.
Kwa vigezo hivyo Mwanaspoti limewaangalia wachezaji hawa jinsi watakavyowapa wakati mgumu wajumbe kuchagua jina moja mwisho wa msimu.
Nyota wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ndiye aliyechangia mabao mengi ya Ligi Kuu Bara hadi sasa, baada ya kufunga 12 akiwa ni kinara na kuasisti manane akihusika na 20, akiivunja rekodi yake ya msimu wa 2024-2025, alipohusika na mabao 17 tu baada ya kufunga manne na kuasisti 13.
Mbali ya Fei Toto yupo kiungo wa Yanga, Mganda Allan Okello ‘Star Boy’ aliyejiunga na kikosi hicho Januari 12, 2026, akitokea Vipers SC ya Uganda, baada ya mwanzo mgumu ila amekuwa lulu na miongoni mwa wachezaji pendwa wa mashabiki, kutokana na kiwango chake.
Okello anashika nafasi ya pili kwa nyota waliochangia mabao mengi, akihusika na mabao 16, ya Ligi Kuu, baada ya kufunga tisa na kuasisti saba, akiendeleza kiwango bora kinachoashiria huenda akaingia katika vita ya MVP mwisho mwa msimu huu.
Mwamba wa Lusaka Clatous Chama ‘Triple C’, baada ya kurejea Simba dirisha dogo la Januari 2026, akitokea Singida Black Stars, kiungo huyo ameendeleza kiwango cha kuvutia, licha ya baadhi ya mashabiki kutokuwa na imani naye mwanzoni alipotua hapo.
Chama anayeichezea Simba kwa mara ya tatu baada ya awali msimu wa 2024-2025, kuichezea Yanga aliyoifungia mabao sita ya Ligi Kuu Bara, msimu huu anashika nafasi ya tatu kwa nyota waliochangia mabao mengi, ambapo hadi sasa amehusika na mabao 14.
Hadi sasa Chama amefunga mabao manane ya Ligi Kuu Bara, ambapo mawili ameyafunga akiwa na Singida Black Stars na sita ameyafunga Simba na kuasisti sita zote akizitoa na kikosi hicho cha Msimbazi, kikiwa ni kiwango bora kwa mchezaji huyo kabla ya mechi ya jana dhidi ya Dodoma.
Licha ya mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube kutokuwa na mwenendo mzuri, ila anashika nafasi ya nne kwa kuhusika na mabao mengi ya Ligi Kuu Bara, akihusika na 12, baada ya kufunga tisa sawa na nyota mwenzake, Okello na kuasisti matatu.
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Elie Mpanzu amehusika katika mabao 11 ya Ligi Kuu akifunga matatu na kuasisti manane, sawa na Pacome Zouzoua wa Yanga aliyefunga saba na kutoa asisti nne, licha ya kiwango cha kupanda na kushuka kwa nyota huyo.
Nyota wa Azam FC, Idd Seleman ‘Nado’ amechangia pia mabao 11, ya Ligi Kuu, baada ya kufunga manane na kuasisti matatu, akifuatiwa na Maxi Nzengeli wa Yanga, aliyechangia 10, kikosini humo kufuatia kufunga matano na kutoa asisti tano.
Mshambuliaji nyota wa Simba, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, aliyejiunga na timu hiyo kwa mkopo akitokea Wydad Casablanca ya Morocco, amehusika katika mabao tisa ya kikosi hicho msimu huu, baada ya kufunga manane na kuasisti moja.
Gomez alijiunga na Wydad Casablanca ya Morocco, Januari 31, 2025 kwa mkataba wa miaka minne, akitokea Klabu ya Fountain Gate, ambapo kwa msimu wa 2024-2025, nyota huyo alifunga mabao sita ya Ligi Kuu, japo kwa sasa ameivunja rekodi yake.
Kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya amechangia mabao tisa pia, baada ya kufunga manane na kuasisti moja, huku nyota wa Singida BS, Mrundi Mossi Nduwumwe aliyejiunga na timu hiyo Januari 2026, akitokea Flambeau du Centre FC ya Burundi akifunga manane.
Nduwumwe amekuwa ni miongoni mwa nyota wa kutazamwa kutokana na kiwango chake anachoendelea kukionyesha, ambapo licha ya kutokuwa na asisti yoyote hadi sasa, ila ugeni wake sio tatizo la kuendelea kucheka na nyavu za wapinzani kwa msimu huu.
Nyota huyo aliyezaliwa Januari 1, 2002, alijiunga na Flambeau du Centre FC Julai 1, 2023, baada ya kuachana na Musongati FC ya kwao pia Burundi, ambapo aliwavutia zaidi mabosi wa Singida walipokutana katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Singida ilikutana na Flambeau katika hatua ya pili kusaka tiketi ya kufuzu makundi, ambapo ilifuzu kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare ya bao 1-1, Burundi, Oktoba 19, 2025, kisha kushinda jijini Dar es Salaam, mabao 3-1, Oktoba 25, 2025.
Winga wa Singida Black Stars, Mgambia Lamine Jarjou aliyejiunga na timu hiyo Agosti 16, 2025, akitokea Grenoble Foot 38 ya Ufaransa, amechangia mabao manane ya Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya kufunga mawili na kutoa asisti sita hadi sasa.
Stephane Aziz KI anayecheza kwa sasa Al-Ittihad SC ya Libya, ndiye mchezaji wa mwisho wa Ligi Kuu Bara kushinda tuzo ya MVP msimu wa 2023-2024, akiwa na Yanga, alipokuwa mfungaji bora baada ya kufunga mabao 21 na kutoa asisti nane kikosini.
Aziz KI aliyejiunga na Wydad Casablanca ya Morocco Juni 1, 2025, akitokea Yanga kisha Januari 24, 2026, kujiunga na Al-Ittihad SC, alikuwa MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast kwa msimu wa 2021-2022, kabla ya kutua Yanga, akitokea ASEC Mimosas.
Rekodi zinaonyesha katika misimu mitatu nyuma, Tuzo ya MVP wa Ligi Kuu Bara imebebwa na nyota wa Yanga, Yannick Bangala msimu wa 2021-2022, Fiston Mayele (2022-2023) na Stephane Aziz KI (2023-2024), huku msimu wa 2024-2025, hazijafanyika.