Mzigo: Barca ya tano, Man Utd tisa
Muktasari:
- Nayo Chelsea inashika nafasi ya sita ikiwa na thamani ya Euro 1.15 bilioni (zaidi ya Sh3.4 trilioni), ikifuatiwa na Liverpool yenye Euro 1.09 bilioni (takriban Sh3.23 trilioni). Bayern Munich inakamilisha orodha ya klabu zenye vikosi vyenye thamani inayozidi Euro 1 bilioni ikiwa na thamani ya Euro 1.04 bilioni (zaidi ya Sh3.08 trilioni).
ORODHA ya vikosi 100 vyenye thamani kubwa zaidi duniani imetolewa, huku Real Madrid ikiongoza kwa thamani ya Euro 1.5 bilioni (zaidi ya Sh4.4 trilioni), huku Manchester City na Arsenal zikifuatia kwa mujibu wa Transfermarkt.
Transfermarkt imetoa tathmini hiyo mpya ya thamani za wachezaji katika ligi mbalimbali kubwa Ulaya, hatua inayowezesha kubaini klabu zenye vikosi vyenye thamani kubwa zaidi duniani, ikiwamo Ligi Kuu England (EPL), Hispania (LaLiga), Italia (Serie A), Ufaransa (Ligue 1) na Ujerumani (Bundesliga). Katika tathmini hiyo, Lamine Yamal wa Barcelona na Erling Haaland wa Manchester City wanaendelea kuongoza kwa kuwa na thamani ya Euro 220 milioni (takriban Sh652.34 bilioni) kila mmoja.
Mchezaji aliyepanda thamani kwa kiwango kikubwa zaidi ni Yan Diomande kufuatia uhamisho wake kwenda Real Madrid, huku Jamal Musiala wa Bayern Munich akiwa miongoni mwa wachezaji ambao thamani zao zimeshuka zaidi. Florian Wirtz wa Liverpool anamfuatia Musiala kwa upande wa kushuka kwa thamani. Tathmini hizo zitabaki kama zilivyo hadi marekebisho yanayofuata yatakapofanyika Desemba, mwaka huu.
REAL MADRID KILELENI
Real Madrid inaendelea kuwa klabu yenye kikosi chenye thamani kubwa zaidi duniani ikiwa ni Euro 1.5 bilioni (zaidi ya Sh4.4 milioni). Thamani ya kikosi hicho imeongezeka kwa euro milioni 40 (takriban Sh118 bilioni) katika tathmini ya LaLiga.
Madrid ina wachezaji watano ambao kila mmoja ana thamani ya Euro 100 milioni (takriban ya Sh299.4 bilioni) au zaidi. Kylian Mbappe ndiye mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi katika kikosi hicho, akiwa na thamani ya Euro 200 milioni (zaidi ya Sh590.9 bilioni).
Manchester City inashika nafasi ya pili kwa thamani inayokadiriwa kukaribia Euro 1.5 bilioni (zaidi ya Sh4.4 trilioni), ingawa thamani yake halisi ni chini kidogo ya Madrid. Thamani ya kikosi hicho imeongezeka kwa Euro 66 milioni (zaidi ya Sh195.7 bilioni) kufuatia usajili wa Enzo Fernandez, Ayyoub Bouaddi na Elliot Anderson katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Arsenal inashika nafasi ya tatu ikiwa na thamani ya Euro 1.38 bilioni (takriban Sh4.09 trilioni), baada ya kuongezeka kwa Euro milioni 48 (zaidi ya Sh141.8 bilioni), huku wachezaji wa Arsenal kina Max Dowman na Myles Lewis-Skelly, kila mmoja ameongeza thamani hadi Euro 20 milioni (takriban Sh59,05 bilioni). Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, PSG wanashika nafasi ya nne kwa thamani ya Euro 1.36 bilioni (takriban Sh4.03 trilioni), huku Barcelona ikikamilisha tano bora ikiwa na thamani ya Euro 1.30 bilioni (zaidi ya Sh3.85 trilioni).
Nayo Chelsea inashika nafasi ya sita ikiwa na thamani ya Euro 1.15 bilioni (zaidi ya Sh3.4 trilioni), ikifuatiwa na Liverpool yenye Euro 1.09 bilioni (takriban Sh3.23 trilioni). Bayern Munich inakamilisha orodha ya klabu zenye vikosi vyenye thamani inayozidi Euro 1 bilioni ikiwa na thamani ya Euro 1.04 bilioni (zaidi ya Sh3.08 trilioni).
Ukiachana na hizo hapo juu zenye thamani ya zaidi ya Euro 1 bilioni, Manchester United inashika nafasi ya tisa kwa thamani ya Euro 928.8 milioni (takriban Sh2.75 trilioni), huku Tottenham Hotspur ikikamilisha 10 bora ikiwa na thamani ya Euro 836 milioni (zaidi ya Sh2.47 trilioni).
Licha ya Tottenham kuendelea kufanya vibaya ikilinganishwa na matarajio yake chini ya kocha Roberto De Zerbi, kikosi chake bado kina thamani kubwa katika soko la wachezaji.
LIGI KUU ENGLAND YATAWALA
Orodha ya klabu 20 zenye vikosi vyenye thamani kubwa zaidi duniani imetawaliwa na timu za Ligi Kuu England, jambo linaloonyesha ukubwa wa uwekezaji wa ligi hiyo katika wachezaji. Ni timu sita tu zisizotoka England ambazo zina vikosi vyenye thamani kubwa kuliko Brighton ambayo thamani ya kikosi chake inafikia Euro 700 milioni (zaidi ya Sh2.06 trilioni).
PSG ndiyo klabu pekee kutoka Ligue 1 ya Ufaransa iliyowakilishwa katika kundi hilo. Bundesliga ya Ujerumani inawakilishwa na Bayern Munich na Borussia Dortmund, huku Inter Milan ikiwa klabu yenye kikosi chenye thamani kubwa zaidi kutoka Serie A ya Italia ikiwa nacho cha Euro 738.3 milioni (zaidi ya Sh2,18 trilioni), ikiendelea kuonyesha nafasi yake miongoni mwa klabu zenye vikosi vya thamani kubwa barani Ulaya.
Kwa upande mwingine, orodha hiyo inaonyesha kuwa thamani ya kikosi pekee haitoshi kuhakikisha mafanikio uwanjani, kwani baadhi ya klabu zenye thamani kubwa bado zinakabiliwa na changamoto ya kutimiza matarajio ya mashabiki wao.