NIONANYO: Mapinduzi Cup 2025 na funzo la fainali za CHAN

Muktasari:
- Tofauti na mashindano ya miaka ya hivi karibuni yaliyohusisha klabu, mashindano ya mwaka huu yalijumuisha timu za Taifa za Zanzibar, Tanzania Bara, Kenya na Burkina Faso.
MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi (Mapinduzi Cup) ambayo hufanyika kama sehemu ya maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya visiwa vya Zanzibar yalitamatika juma hili.
Tofauti na mashindano ya miaka ya hivi karibuni yaliyohusisha klabu, mashindano ya mwaka huu yalijumuisha timu za Taifa za Zanzibar, Tanzania Bara, Kenya na Burkina Faso.
Uganda na Burudi walialikwa pia lakini wakajitoa mwishoni. Kujitoa kwa mataifa hayo kulilazimisha waandaaji kubadili mfumo wa mashindano kutoka mfumo wa makundi kwenda mfumo wa ligi ambayo hata hivyo ilikuwa na fainali kati ya mshindi wa kwanza na mshindi wa pili.

Timu ya taifa ya Zanzibar iliibuka mshindi kwa kuifunga Burkina Faso kwa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali. Awali, kwenye ligi, Burkina Faso iliifunga Zanzibar Heroes kwa bao 1-0.
Mashindano ya timu za taifa yalikuwa ni muafaka hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania kwa kushirikiana na majirani zake Kenya na Uganda wangeandaa mashindano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) mnamo mwezi Februari 2025.
Mashindano hayo sasa yamesogezwa mpaka mwezi wa Agosti 2025 kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya miundombinu katika mataifa hayo.

Timu ya taifa ya Tanzania Bara ilishika mkia kwa kufungwa michezo yote katika michuano hiyo. Kufanya vibaya kwa Kilimanjaro Stars kulipunguza mvuto wa mashindano hayo hasa kwa mashabiki wanaotokea bara ambao kwa miaka mingi wamekuwa wafuatiliaji wakubwa wa mashindano hayo.
Timu ya bara, pamoja na kutokuwa na wachezaji wa Yanga na Simba, haikuwa popote karibu na hadhi ya kuwakilisha taifa.
Najaribu kujiuliza kama hata ingeunganishwa na Zanzibar Heroes wangeweza kufikia uwezo wa Burkina Faso ambao licha ya kupoteza fainali bado walikuwa ni timu bora na ndio walioongoza ligi.

Wanaohusika na kuandaa timu ya taifa ya mashindano ya CHAN wanatakiwa kuweka mkakati kabambe ili kuepuka yasitokee yaliyoipata Kilimanjaro Stars kule Pemba.
Kwa kuwa mashindano yamesogezwa mpaka Agosti, ina maana mashindano ya CHAN yanaweza kufanyika kabla ya ligi kuanza na utimamu wa wachezaji utakuwa chini.
Ni lazima timu ipatikane kambini mwezi wa Julai 2025 kama kweli tunataka kufanya vizuri katika mashindano hayo.Hatuwezi kusema mashindano yamefanikiwa iwapo timu mwenyeji inatolewa raundi za awali.

Ushindi wa Zanzibar Heroes katika mchezo wa fainali unaweza kuhesabiwa kuwa ndiyo mafanikio ya mashindano ya Mapinduzi Cup.Iwapo Zanzibar Heroes wangepoteza fainali, na huku Kilimanjaro wamekwishatolewa mapema basi mashindano haya yangeonekana ni hasara kwa Tanzania.
Pamoja na mahitaji mengine muhimu kama viwanja vya mashindano na mazoezi, usafiri, hoteli, usalama na kadhalika kufanya vizuri kwa timu mwenyeji ni moja ya maandalizi muhimu ambayo yanatakiwa kufanywa unapoandaa mashindano makubwa.
Tanzania, Kenya na Uganda lazima waweke nguvu nyingi kuhakikisha timu zao ni imara kwa ajili ya mashabiki wao na kwa ajili ya mashindano ya CHAN.Kama timu zikifanya vibaya, hakuna atakayekumbuka barabara nzuri au uwanja mzuri.
Timu za wenyeji zikifanya vizuri, mashindano yamefanya vizuri. Kwamba Rais Hussein Mwinyi ameandaa dhifa ya chakula kuwapongeza Zanzibar Heroes, ni ujumbe kwamba ushindi wa Zanzibar Heroes ulikuwa unasubiriwa kwa hamu kwani mcheza kwao hutuzwa.
Bila shaka kulikuwa na upungufu kadhaa kama vile kiwango kidogo cha waamuzi lakini bado kufanya vizuri kwa wenyeji Zanzibar Heroes ndiyo habari ya mjini kwani mcheza kwao hutuzwa.
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.