Nyagawa ilibaki kidogo tu nitue Yanga

IMEKUWA ni desturi kwa timu za Simba na Yanga kuporana wachezaji. Achana na suala la kuchukuliana wachezaji wao, lakini kuna hili la kuporana wanaotoka timu nyingine kwa nia ya kujiunga na timu hizo.
Kuna matukio mengi ya kuporana wachezaji kwa timu hizo kufanyia ‘umafia’ huo, mojawapo ni la kiungo wa zamani wa Mtibwa Sugar, Nico Nyagawa aliyekaribia kabisa kusajiliwa Yanga, lakini zikafanyika mbinu flani na kujikuta akitua Msimbazi badala ya Jangwani.
Ndivyo ilivyotokea baada ya Yanga kumficha hotelini. Nyagawa amefichua kilichotokea katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam.
“Nakumbuka ilikuwa mechi ya mwisho ya ligi ilichezwa Morogoro kati ya Mtibwa na Simba, baada ya mechi Nteze John alinifuata na kuniambia anapenda navyocheza na angetamani siku moja nicheze Simba, aliniuliza kama nitakuwa tayari nikamjibu nipo tayari muda wowote,” anasema Nyagawa.
“Wakati nacheza Mtibwa nilikuwa winga. Nilikuwa natengeneza sana nafasi za kufunga ingawa sikuwa mfungaji nadhani hicho ndicho kilimvutia Nteze.
“Aliniahidi kwenda kuzungumza na viongozi. Hivyo ligi ilipoisha nilirudi kwetu Njombe, nilikaa huko pasipo kupokea simu ya Simba, baadaye kuna mwanachama wa Yanga alikuwa ni kiongozi wa Yanga Family anaishi Morogoro alikuwa maarufu sana alinipigia kuhusu kunisajili. Enzi hizo Yanga yeyote mwenye pesa anafanya usajili na kipindi hicho ilikuwa Yanga ya kuungaunga.
“Nakumbuka ni kipindi alichosajiliwa Mohamed Banka na Tito Andrew. Nilitumiwa nauli kutoka Njombe hadi Morogoro na kulipiwa hoteli nikiwekewa ulinzi mkali wa makomandoo kwani nao walisikia kuwa Simba walikuwa wakinihitaji. Tulizungumza na nilikuwa tayari kusaini Yanga kwa mkataba wa miaka miwili kwa Sh4.5 milioni.
“Nilikaa hotelini siku ya kwanza, ya pili hamna kinachoendelea niliwauliza inakuwaje niliambiwa kuna pesa zinasubiriwa. Siku ya tatu nikiwa pale nilipigiwa simu na mwanachama mwingine wa Simba ni aliitwa Hassan Bantu (marehemu kwa sasa) naye anaishi Morogoro.
“Nilimwelezea kila kitu na kwamba nimefanya hivyo kwasababu niliona upande wa Simba ulikuwa kimya, ndio aliniambia Hassan Hassanol wakati huo akiwa katibu mkuu wa Simba alimpigia simu kuwa anatoka Dar kwenda Morogoro kuja kumalizana na mimi.
“Kazi ilikuwa ngumu, nilifikiria nachomokaje hotelini maana kulikuwa na makomandoo wa kunilinda. Bantu aliniambia hiyo kazi nimwachie yeye. Tito alikuwa mtu wa Morogoro na alikuwa amesaini tayari, hivyo Bantu akazungumza na Tito ili aje anichukue hotelini kwani wale makomandoo wasingempinga.
“Aliambiwa awaombe makomandoo kuwa chakula cha usiku naenda kula kwake Tito maana tayari walikuwa wamempoza. Hivyo akakubali kunitorosha hotelini.
“Kweli dili la kuondoka hotelini pale lilifanikiwa na kwenda kuonana na Hassanol maeneo ya Mikese kwani hakufika mjini. Nilimalizana naye mkataba wa miaka miwili kwa dau la Sh5.5 milioni.
“Sikurudi Njombe siku hiyo, nilihama hoteli na kwenda kufungua akaunti ya benki na kuweka pesa yangu yote na kubakiza kiasi kidogo tu mfukoni. Huo ndiyo ukawa mwanzo wangu wa kutua Simba ingawa aliyenipa nauli kutoka Njombe Mzee Madinda (kwa sasa ni marehemu) alinipigia simu na kunitakia kila la heri niendako ingawa hakuficha kwamba alikasirika lakini baadaye aliona ni heri akubaliana na hali halisi.”
KOCHA HAKUMUELEWA
Hata hivyo, Nyagawa anasema: “Kumbuka kipindi ambacho natua Simba ilikuwa ile ya moto ambayo ilitinga robo fainali ya Caf 2003. Hakuna mchezaji ambaye ungeweza kumgusa aanzie benchi halafu mimi niingie. Nilikaa zaidi ya miezi mitatu nikiangalia mpira jukwaani.
“Nilimkuta Kocha Tauzany (Nzoyisaba). Hakunielewa kabisa, kila gazeti liliniandika kuwa Simba imesajili galasa. Nilivurugwa kabisa, ingawa nilipotua Simba nilikuwa na mchecheto kutokana na umri mdogo niliokuwa nao na kikosi imara zaidi.
“Nteze na Juma Kaseja walikuwa wananipa moyo sana kuwa ipo siku watanielewa tu, maana nafasi yangu ilikuwa na mawinga kama Ulimboka Mwakingwe, Yahya Akilimali, Yusuph Mgwao ambao huwaambii kitu watu wa Simba kuhusu wachezaji hao. Ilikuwa ni vigumu kuwa-nyan-g’anya namba.”
MOLOTO AMWELEWA
Baada ya kuondoka Tauzany, alitua kocha mpya aliyeanza kumuwelewa.
“Baadaye Kocha Tauzany aliondoka akaja Troti Moloto, huyo ndiye alianza kunikubali. Tulisajili watatu wakati huo mimi, Shaban Nditi na Mussa Mgosi, mwaka uliofuata Nditi aliamua kurudi Mtibwa Sugar maana mimi na yeye tulikuwa tunakaa jukwaani,” anasema.
“Hapo nilianza kucheza. Ndani ya Simba nilicheza nafasi zote kasoro kipa tu. Kocha alikuwa akiona sehemu kuna upungufu basi alinipanga.
“Kipindi nilichopitia nikiwa nacheza nakifananisha kama anachopitia Mzamiru Yassin, unajua ni mchezaji ambaye anaweza sana ila hadi mtu uwe na jicho la tatu ndipo utaona na kufahamu ana kitu gani kwenye miguu yake. Hata Sadio Kanoute anafanya kazi kubwa uwanjani, watu kama hao huwa wanadumu sana kwenye mpira.”
APANGWA STRAIKA
Akizungumza zaidia, Nyagawa anasema: “Msimu wa 2004/05 Athuman Machupa aliondoka kwenye timu. Wakati anaondoka ilibaki kama wiki hivi tucheze na Yanga, Mgosi na Victor Costa nao waliondoka kwenda Afrika Kusini, Seleman Matola akiwa nahodha alinifuata kuniambia hiyo mechi nicheze namba tisa yaani straika.
“Nilijiuliza sana nitawezaje kucheza straika kwenye mechi kubwa na ngumu kama hiyo, Matola aliniambia nitacheza, walinipa moyo sana kwani ilikuwa ni mara ya kwanza kucheza mechi kubwa kama hiyo.”
AITUNGUA YANGA MABAO MBILI
Katika mechi na Yanga, Nyagawa anasema: “Kabla ya hapo nilichaguliwa kuwa nahodha wale mafaza wa timu waligoma kabisa wakidai mimi ni mdogo ingawa nilipendekezwa na Kocha Julio (Jamhuri Kihwelo), sasa nilipocheza ile mechi na kufunga mabao yote mawili hapo kila mtu alinikubali nipewe unahodha, basi nikawa msaidizi.
“Naikumbuka ile mechi kwa sababu ilinirahisishia sana jambo langu la ndoa maana wakati nacheza zilibaki wiki mbili mbele kufunga ndoa, hivyo kila ninayempelekea kadi alinipa mchango kirahisi na ndoa yangu kupata urahisi sana nilipewa michango iliyoshiba.”
Nyagawa anasema baada ya mechi hiyo kuna mtu alimpigia simu na kumpongeza.
“Sikutegemea, baada ya kuifunga Yanga nilipigiwa simu na Madinda na kunipongeza, alisema hakuwa na kinyongo nilipomtoroka hotelini pamoja na kunitumia nauli yake kutoka Njombe.
“Mwaka 2008 nilipewa unahodha mkuu kuchukua nafasi ya Kaseja wakati huo alipoondoka kwenda Yanga.”
GOTI LAMSTAAFISHA
Nyagawa ni kati ya wachezaji wanaodaiwa kustaafu wakiwa na umri mdogo. Hapa anafunguka sababu iliyomfanya astaafu akiwa na mdogo.
“Nilistaafu kulingana na mazingira niliyokutana nayo. Niliumia goti ambalo hadi sasa linanisumbua, sikuwahi kufanyiwa upasuaji wala matibabu ya maana, nilikosa mtu wa kunisaidia.
“Niliumia goti nakumbuka Simba ikiwa chini ya uongozi wa mwenyekiti Ismaili Aden Rage, nilikaa kama miezi sita pasipo kucheza hadi Kocha Moses Basena wa Uganda ambaye aliwaambia viongozi ni lazima nitibiwe ndipo nirudi uwanjani, wakati wote huo nilikuwa nahangaika mwenyewe kujitibia, nilitumia pesa nyingi hadi nilikata tamaa sasa ndio maana nikaona ni bora nistaafu tu.
“Hadi sasa nasumbuliwa na goti, nikifanya mazoezi kidogo tu lazima nipate maumivu makali ila nashukuru Mungu maisha yanaendelea tu, sina namna ya kusema nitalifanyaje hili goti. Sikutangaza kustaafu tu, nilijua kama nitapona ili baadaye nirudi uwanjani, ila nilivyoona mambo magumu zaidi nikaamua kuachana na mpira kabisa, nikakaa zangu nyumbani tu ndipo nilipigiwa simu nirudi kama meneja wa timu ya Simba.”
SIMBA IKO KWENYE MAPITO
Nyagawa anasema Simba kwa sasa iko kwenye mapito ya muda tu, timu itakaa sawa na kurudisha makali yake kama ya msimu uliopita.
“Kutetea Ligi Kuu miaka minne sio jambo jepesi, wataalamu wanasema kukaa juu siku zote ni kazi kubwa kuliko kushuka chini. Simba wamekaa kwenye mafanikio kwa miaka minne mfululizo, uzuri viongozi wa Simba wameshituka mapema, wameanza kuingiza maingizo mapya, hizi nyakati zitapita tu.
“Kuelekea mechi ya robo fainali dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini, kama ningekuwa kocha, timu iliyocheza dhidi ya US Gandermarie nisingebadilisha kabisa. Ila kwenye mchezo wa marudiano wa ugenini ningeongeza nguvu kwenye kiungo ambapo Thadeo Lwanga angeingia kuchukua nafasi ya Bernard Morrison ambaye inadaiwa hawezi kwenda huko kusaidiana na wenzake.”
Nyagawa amewataka washambuliaji wa Simba kuwa watulivu tu ili timu ishinde mabao mengi katika mchezo wa nyumbani.
“Kwanza ni kuiheshimu Orlando Pirates na tusiidharau kama ilivyokuwa kwa Kaizer Chief,” anasema.
Kiungo huyo anasema wachezaji waliopo Simba wanatakiwa kuitumikia bila ya kujali udhaifu wao.“Hawa ndio wachezaji wetu kwa sasa. Wawe wazuri ama mabovu, kinachotakiwa ni kuzidisha umakini, kupambana na kujitoa wacheze kama hawatakuja kucheza tena, maana maisha yamebadilika hata figisu figisu za ugenini siku hizi zimepungua kwani timu zinajitegemea tofauti na zamani kila kitu kiliandaliwa na wenyeji.”
AIPONGEZA YANGA
Nyagawa anasema Yanga msimu huu inafanya vizuri kwenye Ligi Kuu na endapo itakosa ubingwa, basi Jangwani hakutakuwa na maelewano.
“Msimu uliopita walituzidi pointi kwa muda mrefu lakini baadaye tukawakuta na hatimaye kutetea ubingwa wetu. Msimu huu Yanga imejipanga vizuri zaidi, inaongoza ligi ila matokeo baadaye yakiwa mabaya hali ya hewa itachafuka.” ITAENDELEA KESHO