Nyuma ya pazia penzi la Kim Kardashian na Hamilton
Muktasari:
- Kim, mtangazaji wa realty show ya Keeping Up with the Kardashians, kabla ya Hamilton aliwahi kuhusishwa na wanaume kadhaa ila aliofunga nao ndoa ni watatu.
MWANAMITINDO wa Marekani, Kim Kardashian, 55, kwa sasa anagonga vichwa vya habari duniani kutokana na uhusiano wake na staa wa mbio za magari ya Formula 1, Lewis Hamilton, 41, kutokea Uingereza.
Hata hivyo, licha ya Kim kumpenda Hamilton kwa muda mrefu kama vyanzo mbalimbali vilivyoeleza, ilimbidi dereva huyo kusubiri kwa miaka 12 hadi kuwa na uhusiano rasmi na mwanamitindo hiyo.
Kim, mtangazaji wa realty show ya Keeping Up with the Kardashians, kabla ya Hamilton aliwahi kuhusishwa na wanaume kadhaa ila aliofunga nao ndoa ni watatu.
Akiwa na umri wa miaka 19, aliolewa na mtayarishaji muziki, Damon Thomas lakini ndoa yao ilidumu kwa miaka mitatu tu, kabla ya wakisilisha kesi ya talaka mahakamani mwaka 2003.
Mchezaji wa zamani wa New Jersey Nets inayoshiriki Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), Kris Humphries, akaja kumuoa Kim hapo Agosti 2011, ila baada ya siku 72 wakatalikiana!
Haikuishia hapo, Kim alikuja kuolewa na rapa Kanye West (Ye), wawili hao walifunga ndoa huko Florence, Italia hapo Mei 2014 na kuachana 2022, huku wakiwa na watoto wanne.
Tangu talaka na Kanye West, Kim hakuwahi kuthibitisha uhusiano wake wowote kwa umma hadi alipofanya sasa akiwa na Hamilton.
Mnamo Novemba 2025, Kim kupitia Keeping Up With The Kardashians amesema anatamani kuendelea kuwa single.
"Unapokaa muda mrefu ukiwa single, unazidi kuzoea, na mawazo ya kuwa na mtu wa karibu yanapungua na hata kukosa mvuto," amesema Kim.
Kauli yake ilikuja baada ya mwigizaji Sarah Paulson ambaye wamecheza pamoja tamthilia, All’s Fair (2025), kumtaka Kim kuwa na mpenzi na kuacha kujilinda kupita kiasi.
Wakati hayo yakiendelea, Hamilton alikuwa sehemu akimtamtaza tu Kim, na pangine tayari walishaanza mchakato wa jambo lao kwa sababu tetesi za kuwa pamoja zilianza miezi miwili baadaye.
Wawili hao wamefahamiana kwa miaka zaidi ya 10, yaani tangu Kim yupo na Kanye West (Ye), wakati huo kila walipokutana walizungumza kama marafiki ila sasa simulizi kuhusu wao imebadilika.
Katika hafla ya GQ Men of the Year 2014, Kim alimsalimia Hamilton kwa kumbusu shavuni kama ishara ya urafiki, na tangu hapo waliendelea kukutana katika hafla mbalimbali kama tuzo za WSJ. Magazine Innovator 2021.
Mwaka 2023 baada ya kuhudhuria show ya Pharrell Williams, Chanzo kimoja kilidokeza kuwa Kim na Hamilton wamekuwa na utamaduni wa kuzoeana kupitia kiasi kwa sababu wamefahamiana kwa miaka mingi.
Tetesi za kuwa pamoja zilizidi kupamba moto baada ya TMZ kurusha video iliyowaonyesha wawili hao wakiwasili katika hoteli moja jijini Paris, Ufaransa baada ya kushuka kwenye gari aina ya SUV hapo Februari 2, 2026.
Kwa mujibu wa mtandao huo maarufu kwa habari za mastaa, Kim na Hamilton walisafiri pamoja kutoka Uingereza kwenda Ufaransa kwa kutumia usafiri wa ndege binafsi unaoendana na hadhi yao na kulinda faragha yao.
Ilidaiwa lengo la kwenda Paris ni kwa ajili ya kujadiliana kuhusu uhusiano wao ambao tayari ulishaanza na kubwa zaidi ni jinsi ambavyo wataliweka jambo hilo mbele ya umma bila kuharibu heshima yao.
Takribani wiki moja baadaye, walionekana katika Super Bowl LX ambapo waliketi pamoja katika chumba maalumu na siku iliyofuatia Hamilton alionekana katika video ambayo Kim iliiposti Instagram, kitu kilichothibitisha rasmi ni wapenzi.
Chanzo kimoja kiliuambia mtandao wa People, Kim amekuwa kila mara akitoka nyumbani kwake Los Angeles kwa ajili ya kwenda kuonana na Hamilton iwe kwao London au Paris.
"Ni mwanamume ambaye amemvutia kwa dhati kwa muda mrefu. Amekuwa akimpenda kila wakati. Anafurahia uhusiano wao wa kimapenzi. Hamilton anamfanya Kim ajisikie salama na anafurahia sana kutumia muda wake pamoja naye," kilisema chanzo hicho.
Katika mahojiano na Podcast ya dada yake, Khloe in Wonder Land mnano Januari 2026, Kim alimweleza kuhusu sifa anazozitaka kwa mwanamume wake ajaye baada ya kuwa single kwa muda mrefu.
“Awe mtu mwenye maadili na misingi mizuri, mtu mtulivu na anayeaminika. Mtu anayekubali kuwajibika. Nafikiri hicho ndio kipaumbele changu namba moja," amesema Kim.
Hivyo ni wazi kuwa kwa sasa ndoto ya Kim Kardashian imetimia kwa namna ambavyo anaonekana sehemu mbalimbali duniani akiwa ameongozana na Hamilton. Kila mmoja ana uhuru wa kuposti picha za mwenzake, kitu ambacho Kim alikikosa kwa muda mrefu.