NYUMA YA PAZIA: Qatar wamepambana kweli hadi wamefanikiwa kuikaribisha dunia

NI fainali nyingine za Kombe la Dunia. Nipo Doha. Mji mkuu wa Qatar. Fainali za Kombe la Dunia zimefana kwa ujanja ujanja wa hali ya juu kutoka kwa watu wa Qatar. Utajiri wao umefanikisha kwa kiasi kikubwa kufanikiwa kwa fainali hizi.

Jaribu kufikiria, Qatar ina kilomita za mraba 11,571 wakati mkoa wote wa Morogoro una kilomita za mraba 73,039. Hii inamaanisha kwamba Qatar nzima ni kama wilaya moja tu ya Morogoro. Kuna wale wajanja wa zamani wa Fifa walichukua pesa kutoka kwa matajiri wa Qatar kisha wakawapa Kombe la Dunia.

Kama wangefuatilia vigezo vingi basi Qatar wasingepewa fainali hizo. Hata hivyo Kombe la Dunia limefana. Kuna sababu mbalimbali. Kwa mfano, walipogundua kwamba hoteli zisingetosha basi Qatar wakatengeneza nyumba feki au tuseme makazi ya muda kwa ajili ya wageni.

Ni kama tela fulani au kontena fulani za kisasa ambazo ni kubwa kidogo. Ndani zina vyumba viwili, sebule, jiko la gesi, bafu, choo na kila kitu. Ukiingia humo ndani ni kama upo katika chumba fulani kikubwa hivi. Hapo ndipo ninapokaa mimi. Panaitwa Caravan City.

Maelfu ya mashabiki wa soka kutoka nchi mbalimbali wanakaa humo. Hizo kontena zenyewe zina matajiri na ni wazi kwamba baada ya fainali za Kombe la Dunia hawatazihitaji tena. Wataziondoa na eneo hilo litabakia jeupe. Kwa sasa ni makazi ya watu na kuna kila kitu. Wameweka hadi supermarket ambazo zinakidhi mahitaji ya watu.

Kutokana na udogo wa nchi ya Qatar nadhani hizi ni fainali ambazo wazoefu wa kuhudhuria mechi za Kombe la Dunia watakuwa wamefaidi. Unaweza kutazama mechi mbili hadi tatu ndani ya siku moja. Ni kitu rahisi tu.

Unamaliza kutazama mechi moja, kisha unaingia katika treni. Ndani ya nusu saa utakuwa umefika katika uwanja mwingine kutazama mechi nyingine. Isingeweza kukutokea katika fainali tatu za Kombe la Dunia zilizopita.

Usingeweza kutoka Cape Town na kuwahi mechi ya Port Elizabeth pale Afrika Kusini. Usingeweza kutoka Rio de Janeiro kwenda Sao Paulo ndani ya siku moja na kuwahi mechi nyingine. Usingeweza kutoka Moscow kuwahi pambano jingine la soka pale Saint Petersburg nchini Russia.

Kwa Qatar imewezekana. Kama wilaya moja inaandaa mechi tatu za Kombe la Dunia zinazotofautiana saa mbili kwanini isiwezekane? Hiki ndicho ambacho watu wenye tiketi nyingi wanafaidi kwa kiasi kikubwa hapa Qatar.

Kwa kiburi cha pesa au namna ya kurahisisha mambo, treni zote ni bure kwa abiria kwa sasa. Sijui kama tukiondoka wataanza kulipisha watu, lakini kwa sasa treni zote za kisasa za umeme ambazo zinapita ardhini ni bure tu. Unapanda kadri unavyoweza na unashuka kadri unavyoweza.

Viwanja vyao ni vya kisasa zaidi. Haishangazi kwa sababu ni viwanja vipya. Hauwezi kulinganisha na viwanja kama Old Trafford, Santiago Bernabeu, San Siro, Nou Camp na vinginevyo. Labda ni kwa sababu vilijengwa zamani. Hivi ni vya teknolojia mpya na vina mvuto wa ajabu.

Swali ambalo wageni tumekuwa tukiulizana ni namna gani wataweza kuvitumia mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia. Hawana ligi kubwa, hawana mashabiki wengi na zaidi ni kwamba hawana timu kubwa zenye mvuto ambazo zinaweza kuvuta mashabiki kutoka katika nchi nyingine. Watavitumiaje?

Pombe? Wamenishangaza kidogo watu wa Qatar. Wamenishangaza Waarabu. Nilidhani hakutakuwa na pombe kabisa. Zilikuwepo. Ungeweza kuona tatizo kama una tabia ya kutembea na pombe mkononi. Na ungeweza kuona tatizo kama una tabia ya kunywa katika baa ambazo zipo kando ya barabara. Ukweli ni kwamba pombe zipo kwa kiasi kikubwa.

Kuna maeneo ambayo mashabiki wametengewa kwa ajili ya kutazama mechi za Kombe la Dunia. Zimewekwa ‘screen’ kubwa na mashabiki zaidi ya 3000 hujitokeza katika eneo moja kutazama hizo mechi. Hapo ndipo pombe zinauzwa, hasa za wadhamini wakubwa wa michuano hii - Budweiser.

Pia kuna baa zilizopo katika hoteli kubwa nazo huuza pombe kama kawaida. Hakuna tatizo. Watu wanalewa kama kawaida isipokuwa hauruhusiwi kuondoka na kinywaji chako mkononi na hatua kali zinaweza kuchukuliwa dhidi yako.

Katika viwanja pombe ni marufuku, lakini ilinishangaza katika pambano la Ufaransa dhidi ya Tunisia ambapo nilipata tiketi maalumu ambayo iliniwezesha kupata huduma maalumu ndani ya uwanja. Huduma hiyo ingetolewa kabla na baada ya mechi. Ni huduma ya kula vyakula mbalimbali kadri unavyojisikia, kunywa vinywaji mbalimbali kadri unavyojisikia. Nikiwa na mwanamuziki Diamond Platnumz na watu wengine tulijitoma katika eneo hilo kwa sababu tiketi zetu zilituruhusu. Tulikuta pombe za kumwaga.

Tofauti ni kwamba maeneo mengine yote ya uwanja hayana vilevi. Hawajaweka kaunta zinazozunguka nyuma ya majukwaa kama ilivyo katika viwanja vyote vya Ulaya ambavyo nimewahi kwenda. Nadhani wamefanya makusudi kwa sababu wanafahamu kwamba hawatakuwa na matumizi ya pombe pindi wageni wakiondoka.

Maisha mengi ya tamaduni nyingine yanaruhusiwa. Wanawake wa Magharibi wanavaa nguo fupi kama kawaida. Kitu ambacho nakifahamu kuhusu Qatar kabla hata ya Kombe la Dunia ni kwamba kuna idadi kubwa ya wageni kuliko wenyeji. Wafanyakazi karibu wote wa nchi nzima ni wageni. Rafiki zetu Wakenya ndio wapo wengi zaidi wakisaka maisha. Watanzania sio wengi na nadhani ujamaa umetulemaza tu.

Hii ina maana kwamba wageni walishakubali kuwepo kwa tamaduni za nchi nyingine kabla hata ya Kombe la Dunia ingawa wamekataza pombe na baadhi ya vitu vingine. Kwa nilichogundua ni kwamba mara baada ya kumalizika kwa fainali hizi tutatazama nyuma na kugundua kwamba zilikuwa fainali zenye mafanikio ndani na nje ya uwanja. Inawezekana waliohudhuria wangeweza kufurahia zaidi fainali hizi kama wangekuwa nchi nyingine za kujiachia lakini mpaka sasa hakuna mambo mengi yaliyoharibika tofauti na ilivyodhaniwa awali.