Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Raheem:  Kibu, Sillah... ni kazi kuwakaba

Muktasari:

  • Huyu ni Raheem Shomary. Alijiunga na KMC akitokea KVZ ya Zanzibar aliyoitumikia kwa miezi sita akitokea timu ya vijana ya Simba kwa mkopo.

Siyo maarufu sana, lakini ubora wake msimu huu umemfanya apate namba na zaidi ni kuzivutia klabu mbalimbali zinazotamani kuinasa saini yake.

Huyu ni Raheem Shomary. Alijiunga na KMC akitokea KVZ ya Zanzibar aliyoitumikia kwa miezi sita akitokea timu ya vijana ya Simba kwa mkopo.

Kutokana na kiwango alichoonyesha hadi sasa, moja ya timu alizozivutia ni Al Hilal ya Sudan inayokipiga kwa sasa katika Ligi Kuu ya Mauritania kutokana na usalama mdogo nchini kwao.

Alianza kupata jina baada ya kuchaguliwa mchezaji bora chipukizi msimu wa 2023/24, akimpiku kiungo wa Coastal Union, Charles Semfuko.

Mwanaspoti limepiga stori na beki huyo ambaye amezungumza mambo mbalimbali ikiwamo kumtaja Charles Luhende ndiye beki aliyekuwa akimtazama kabla ya kuanza kucheza soka la ushindani. 


KIBU, SILLAH SIO MCHEZO

Wakati baadhi ya mashabiki wa soka wakimtaja Kibu Denis hana kazi anayoifanya uwanjani kutokana na kutumia nguvu pekee, lakini hiyo ni tofauti kwa Raheem anayedai kumkaba mshambuliaji huyo inabidi beki awe amejiandaa vya kutosha.

“Kibu ni mshambuliaji mgumu kumkaba kwa sababu ana nguvu, kasi na maarifa hivyo sio rahisi ukiingia kichwa kichwa anaweza akakusababishia shida, kama sio kuonyeshwa kadi, basi utampa nafasi ya kupata penalti,” anasema Raheem anayeweza pia kucheza winga zote mbili na kiungo mkabaji.

“Vivyo hivyo kwa kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Gibril Sillah. Ni aina ya uchezaji wa Kibu kwa sababu anatumia akili sana, ana kasi na ana maarifa. Nikijua nakutana na timu zao huwa najiandaa na kucheza kwa akili dhidi yao.”

Anasema pia anapendezwa na aina ya uchezaji kwani wanabadilika ili wasizoeleke na huo ni ubunifu wao.


TSHABALALA, MSINDO HATARI

Anasepa pia anavutiwa na ubora wa mabeki wanaocheza nafasi kama yake wa Azam, Simba na Coastal Union.

“Ni nyota wengi wanafanya vizuri kwenye nafasi ninayocheza, lakini nimekuwa nikiwatazama Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Pascal Msindo na Miraji Abdallah kutoka Coastal Union. Ni vipaji vikubwa,” anasema na kuongeza; “Hakuna mdau wa soka atakayepingana na mimi nikisema Tshabalala ni bora Afrika. Amefanya mambo mengi makubwa, amehudumu kwa ubora muda mrefu. Ukiondoa yeye pia kuna Msindo ni mchezaji ambaye anakuja kwa kasi na amekuwa bora eneo hilo, anajua kukaba na kufunga anakufunga.”

Raheem anasema ukiondoa wazoefu hao, pia amekuwa akimtazama na kujifunza vitu kwa beki wa Coastal Union, Miraj ambaye pia anamtaja ni bora kwa sasa kwenye ligi kwa wachezaji wa ndani.


MOALLIN KOCHA WA PASI

Raheem alijiunga na KMC ikiwa chini ya Kocha Abdihamid Moallin ambaye sasa ni mkurugenzi wa ufundi wa Yanga, na hapa anasema kocha huyo ndiye aliyemuamini na kumpa nafasi ya kucheza katika kikosi ambacho kilimpa tuzo ya beki bora chipukizi, huku akimzungumzia ni aina ya makocha wanaopenda mchezo wa pasi nyingi.

“Moallin kwangu sio kocha tu ni mzazi. Ni kutokana na namna alivyokuwa anatulea kambini na kuishi na sisi kama wanawe, ilikuwa ni rahisi mno kumuelewa nini anataka tukifanye. Naweza kumtaja ndiyo sehemu ya mafanikio yangu msimu wangu wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara,” anasema na kuongeza:

“Ni kocha kiongozi, aliniamini aliniambia nimekuamini nifanyie kazi... nikafanya kwa juhudi na ubora mkubwa, ndio ukawa mwanzo wa mimi kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, pia Moallin ni muumini wa damu changa.”

LUHENDE ALIMVUTA LIGI KUU

Wakati akiwataja nyota watatu kutoka timu tatu tofauti, Raheem anamzungumzia mkongwe David Charles Luhende kuwa ni mmoja wa nyota ambao walimfanya apambanie malengo ya siku moja kucheza soka la ushindani.

“Nakumbuka kipindi hicho nilikuwa namtazama huku nikiwa sielewi nitacheza nafasi gani hadi hivi sasa nacheza beki - nafasi ambayo yeye pia ndio anaicheza,” anasema Raheem.

“Sikuishia kumtazama tu nilipopata nafasi ya kuonana naye nilimueleza ukweli yeye ndiye aliyenifanya niingie kwenye mpira wa ushindani, alifurahia na kuniambia kuwa mimi pia nina kipaji kikubwa nitafika mbali.”

Beki huyo anasema hadi sasa amekuwa akipokea simu nyingi kutoka kwa mchezaji huyo ambaye amegeuka kuwa mwalimu kwake na mlezi kutokana na namna anavyomjenga na kumpa mbinu za kufanya, ili aweze kuhudumu kwenye soka nini azingatie.

ZAO LA SIMBA B

Haikuwa ajabu kuibuka mchezaji bora chipukizi ukiwa ni msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara kama anavyodai Raheem ni mchezaji ambaye amekuzwa kwenye vituo, hivyo uchezaji wake sio wa kubahatisha.

“Nimeanza kucheza mpira tangu nikiwa na umri mdogo na sijakuzwa na soka la mtaani. Nilipata bahati ya kuchukuliwa na vituo nikianzia kituo cha kukuza vipaji baada ya hapo nikapata nafasi ya kutua kikosi cha timu ya vijana cha Simba ambacho nimehudumu kwa muda na baadaye nilitolewa kwa mkopo kwenda KVZ,” anasema.

“Nilitua Simba msimu wa 2019/20 hadi msimu wa 2022/23 ndipo nilipotolewa kwa mkopo miezi sita ya mwisho na baada ya hapo ndipo nilipopokea simu kutoka kwa kiongozi wangu wa kituo nilichokuzwa ambaye aliniambia kuna timu inanifuatilia kwa ajili ya kunisajili, ndipo nilipomalizana na KMC ambayo naitumikia hadi sasa.”

Anasema KMC alisajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili na unamalizika mwishoni mwa msimu huu akiwa ametumika soka la ushindani kwa miaka miwili na kupata mafanikio ya kuwa mchezaji bora chipukizi msimu wake wa kwanza.