Siku 120 za maajabu ya Minziro Pamba Jiji FC

Muktasari:
- Katika kipindi hicho, Minziro ameibadilisha Pamba Jiji kwa kiasi kikubwa na kuifanya kuwa timu ya ushindani ambapo ameiongoza katika mechi 11 za Ligi Kuu na kushinda nne, sare mbili na kupoteza tano huku ikivuna alama 14.
FEBRUARI 17 kwa kocha Fred Felix ‘Minziro’ itakuwa ni miezi minne kamili ambayo ni sawa na takribani siku 120 ndani ya Pamba Jiji ya Mwanza tangu alipoteuliwa na kupewa majukumu Oktoba 17, 2024 akirithi mikoba ya Goran Kopunovic aliyetimuliwa kutokana na matokeo mabaya.
Katika kipindi hicho, Minziro ameibadilisha Pamba Jiji kwa kiasi kikubwa na kuifanya kuwa timu ya ushindani ambapo ameiongoza katika mechi 11 za Ligi Kuu na kushinda nne, sare mbili na kupoteza tano huku ikivuna alama 14.
Chini ya Minziro, Pamba imefunga mabao saba na kuruhusu saba huku ikipanda kwa nafasi tatu kutoka ya 15 hadii ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na kufufua matumaini ya kubaki kwenye michuano hiyo.
Pamba Jiji ya Minziro haijaruhusu mabao zaidi ya moja katika mechi zake 11 za Ligi Kuu tofauti na hali ilivyokuwa kabla ya ujio wake timu hiyo ikiwa chini ya kocha Goran Kopunovic.

Baada ya kucheza mechi 18 za Ligi Kuu, Pamba Jiji inakamata nafasi ya 12 ikiwa na alama 18, ikishinda nne, sare sita na kupoteza nane, huku ikifunga mabao tisa na kuruhusu 16.
Matokeo ya Pamba chini ya Minziro msimu huu wa 2024/2025 ni Kagera Sugar (1-1), Tabora United (1-0), Namungo (1-0), Fountain Gate (1-3), Simba (1-0), Ken Gold (0-1), JKT Tanzania (0-0), KMC (1-0), Tanzania Prisons (1-0), Dodoma Jiji (0-1) na Azam FC (0-1).
Chini ya Kopunovic aliyetupiwa virago Oktoba 16, 2024, Pamba Jiji ilicheza mechi saba za ligi bila ushindi ikiambulia sare nne na kupoteza michezo mitatu huku ikivuna alama nne na kukamata nafasi ya 15.
Katika mechi hizo saba, timu hiyo ilifunga mabao mawili pekee na kuruhusu tisa huku safu yake ya ushambuliaji ikiwa butu kwani ilicheza mechi sita bila kufunga bao ambapo mabao mawili waliyofunga yalipatikana kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa FC uliomalizika kwa sare ya 2-2.
Matokeo ya Pamba chini ya Kopunovic, Tanzania Prisons (0-0), Dodoma Jiji (0-0), Azam (0-0), Singida (1-0), Mashujaa (2-2), Coastal Union (2-0) na Yanga (4-0).

USAJILI WAMBEBA
Baada ya kutua Pamba, Minziro alisisitiza kuwa wachezaji wenye majeraha ya muda mrefu na wasio na msadaa kwenye timu wataondolewa dirisha dogo ili kuleta watu watakaoleta ushindani kikosini na kuongeza nguvu kwenye timu.
Katika usajili wa dirisha dogo timu hiyo ilifanya usajili wa maana akileta vyuma vipya 12 huku saba wakiwa nyota wa kimataifa na wachezaji watano wazawa.
Wachezaji wa kigeni ni kipa Mohamed Camara (Sierra Leone) na kiungo Abdulaye Camara raia wa Guine waliotoka kwa mkopo Singida Black Stars.
Wengine ni washambuliaji Francois Bakari (Cameroon), Mathew Tegis (Kenya), kiungo mshambuliaji Shassir Nahimana (Burundi), mabeki Modou Camara (Gambia) na Sharif Ibrahim (Cameroon).
Wazawa waliosajiliwa ni Deus Kaseke, Habib Kyombo, na Hamad Majimengi (Singida Black Stars), Zabona Mayombya (Tanzania Prisons), na Abdallah Sebo (huru).
Walioachwa ni Daniel Joram, Erick Okutu, John Mtobesya, Emmanuel Boateng, Robert Kouyala na Salim Kipemba, huku waliotolewa kwa mkopo ni George Mpole (Kagera Sugar) na Yusuph Mashaka (Stand United).

NGUVU YA BONASI
Ili kuhakikisha kazi ya Minziro inakuwa nyepesi na inaongezewa nguvu, uongozi wa klabu hiyo umeweka utaratibu mpya wa bonasi kwa wachezaji katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ili kuhakikisha malengo ya kubaki na kumaliza katika nafasi nzuri yanafanikiwa.
Utaratibu huo wa bonasi ni kuwa, timu ikishinda inapata Sh10 milioni, sare ni Sh5 milioni huku bonasi ikiongezeka kufikia Sh15 milioni hadi Sh50 milioni wakipata matokeo mazuri dhidi ya timu kubwa za Simba, Yanga na Azam FC.
Mbali na bonasi ya timu, wachezaji binafasi pia wametengewa motisha ambapo mfungaji wa bao atapata Sh 250,000, aliyetoa assisti ya bao ni Sh100,000 na kipa akipata cleenesheet anapata Sh100,000.
Hata hivyo, bonasi hizo zina masharti yake ambapo wachezaji watakaonufaika ni wale tu waliohusika na mchezo (kikosi cha kwanza na akiba) na kama ni mchezo wa ugenini wanapata wale waliosafiri na timu. Hii imewekwa ili kuwafanya wachezaji wajitume na kupata nafasi ya kucheza.

MSIKIE MINZIRO
Minziro alisema alipofika kwenye kikosi hicho alikutana na changamoto ya majeraha kwa wachezaji huku kukiwa hakuna mbadala kwenye nafasi mbalimbali, lakini kwa kushirikiana na uongozi wamefanya kazi kubwa dirisha dogo na kutibu tatizo hilo.
Alisema kwa sasa anafarijika kwasababu baadhi ya wachezaji wana majeraha lakini bado kila nafasi ina watu wawili mpaka watatu, hivyo anaamini usajili wa dirisha dogo umewasaidia kwa kiasi kikubwa.
“Ni kweli usajili tuliofanya umetuongezea nguvu, raundi ya kwanza tatizo kubwa nililolikuta ni majeruhi unakuta nafasi moja mtu yuko majeruhi hakuna mwingine mbadala kwahiyo kwenye timu inakuwa ngumu kufanya kazi namna hiyo,” alisema Minziro na kuongeza;
“Pia niushukuru uongozi wamekubaliana na jinsi ambavyo tumeweza kukaa na kuongea wakatusapoti wakakubali benchi la ufundi mapendekezo tuliyowapelekea mwisho wa siku matokeo ndiyo kama hayo mnavyoyaona.”
Kocha huyo alisema licha ya kupiga hatua na kufikisha pointi 18 lakini bado siyo salama kwani wana kazi kubwa ya kufanya kuondoa presha kwa watu na mashabiki wao kuhakikisha kwamba wanaendelea kushinda na kuondooka katika presha ya kushuka daraja.

MECHI ZIJAZO
Feb 15, 2025
v Coastal Union (nyumbani)
Feb 19, 2025
v Mashujaa (ugenini)
Feb 23, 2025
v Singida BS (ugenini)
Feb 28, 2025
v Yanga (nyumbani)
Mar 07, 2025
v Kagera Sugar (ugenini)
Apr 02, 2025
v Namungo (nyumbani)
Apr 05, 2025
v Tabora United (nyumbani)
Apr 08, 2025
v Fountain Gate (nyumbani)
Mei 08, 2025
v Simba (ugenini)
Mei 13, 2025
v KenGold (ugenini)
Mei 21, 2025
v JKT Tanzania (ugenini)
Mei 25, 2025
v KMC (nyumbani)