SPOTI DOKTA: Bidhaa za tumbaku tishioo kwa wanasoka

Muktasari:
- Bidhaa hizo zinazojulikana kwa jina snus na nikotine tobacco free punches au vapors, sigara za kielektroniki ndio zinazotajwa nchini Uingereza kutumiwa na wanasoka wa EPL.
KATIKA taarifa ya utafiti iliyotolewa mwezi Mei 2024 na kuchapishwa na vyombo vikubwa vya habari nchini Uingereza ikiwemo Sky News, Reuters na The Mirror ilionyesha kuwa katika kila wanasoka watano wa EPL mmoja hutumia bidhaa za tumbaku za kisasa.
Bidhaa hizo zinazojulikana kwa jina snus na nikotine tobacco free punches au vapors, sigara za kielektroniki ndio zinazotajwa nchini Uingereza kutumiwa na wanasoka wa EPL.
Utafiti huo ulitoa onyo kwa wanasoka kuachana na matumizi ya bidhaa hizo kwani ni hatari kwa afya zao na mustakabali wa vipaji vyao katika soka.
Uvutaji wa tumbaku na matumizi ya bidhaa zake ikiwamo shisha na vapors ambayo hapa nchini zipo na zimekuwa maarufu sana katika maeneo ya burudani, ni tishio kwa utimamu wa wanasoka. Utafiti huo pia ulieleza kuwa wachezaji ambao wanatumia bidhaa hizo wako katika hatari ya kupata uraibu pamoja na kuharibika katika utimamu wao wa kiafya na hatimaye kushuka kiwango chao.
Ripoti hizo zilieleza kuwa katika mahojiano wanasoka wamekiri wameathirika lakini wanahofia kuomba msaada kwani wanaweza kunyanyapaliwa na kutengwa.
Pia wachezaji inaonekana wanakuwa wavutaji wa pili kutokana na kuonekana mara kwa mara wakijirusha na marafiki wanaotumia bidhaa hizo ikiwamo shisha na vijikopo vya kuvuta snus.
Bidhaa za tumbaku zinaweza kuingia kwa njia za panya na hatimaye kuwafikia watumiaji pasipo bidhaa hizo kukaguliwa kama ni salama kwa afya ya mtumiaji. Bidhaa hizo zimekuwa zikiwaingiza mtegoni wanasoka mastaa kutokana na mvuto wake ulivyo, harufu za matunda na pia ile sifa ya kutumiwa na watu maarufu wenye pesa.
Kule nchini Uingereza mchezaji wa Leicester City, Jamie Vardy aliweka wazi kuwa alitumia bidhaa ya snus miaka ya 2016 kama kiburudisho tu hasa anapotoka katika mechi au mazoezi.
Mshambuliaji huyu alisema aliachana na matumizi hayo hasa baada ya taarifa hasi dhidi ya bidhaa hizo kuripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari mchini Uingereza.
Mwaka 2021 kocha mkuu wa Sunderland, Lee Johnson alilinganisha snus sawa na kuvuta sigara 3 au 4 mara moja, alieleza kuwa alikuwa na wachezaji ambao walikuwa na uraibu wa juu wa bidhaa hizo.
Uraibu ni moja ya tatizo la afya ya akili, ni hali inayomfanya mtumiaji wa kilevi au kisisimua mwili kukihitaji kila mara. Anapokikosa hupata hali kama ya ugonjwa akiwa na dalili za woga, kutetemeka na kukosa utulivu.
Snus inayotajwa sana nchini Uingereza ni halali kwa matumizi ya watu wazima nchini Uingereza, lakini haramu kununua au kuuza hivyo watumiaji mara nyingi huagiza kutoka nje ya nchi.
Mara nyingi hufananishwa na nikotini punches, lakini tofauti kuu ni hiyo snus ina tumbaku.
Asilimia 18 ya wachezaji 628 wa soka wa kiume kutoka EPL walioulizwa katika utafiti walisema wanatumia snus au vimkebe vya nikotini punches.
Bidhaa hizo ziko hivi
Mtumiaji huitaji kununua tofauti na kikopo cha kuvutia au kutumia bomba kwa upande wa shisha, mchanganyaji hutengeneza mkorogo au mtu binafsi hujichanganyia.
Bidhaa hizo ambazo huwa zinafuka moshi mweupe unaofufurika kupitia katika kimiminika maalum hatimaye mvutaji hupokea na kuvuta na kuingia katika mapafu.
Moshi huo si kama una maji, huwa na kampaundi inayojulikana kama proplylene glycol, mafuta ya gylcerol, nikotini, vileta ladha na kemikali nyingine hatari zisizoorodheshwa.
Vimewekwa ladha nzuri na harufu za kuvutia za zabibu, tikiti maji, beri, vanila na minti. Hapa lengo kuteka akili ya mtumiaji wa bidhaa hizo ili kumpumbaza kuwa ni salama kutumia.
Baadhi ya bidhaa zinatengezwa kwa sirisiri na kuingia na kusambaa kwa njia za kimagendo. Mbaya zaidi bidhaa hizo huwa dawa za kulevya na kemikali zisizojulikana ili kumsisimua na kumpa uraibu.
Uwepo wa tumbaku ndani yake ambapo huwa ina kimekali hatari ya Nikotini ambacho ni kihatarishi cha kutokea kwa saratani zote ikiwamo ya mapafu, bomba la chakula na kongosho.
Nikotini husababisha uraibu mkali kwa mtumiaji, hatimaye huwa ni vigumu kuacha kutumia.
Madhara ya kiafya ni haya
Athari anazopata mvutaji wa kwanza ni sawa na athari za mvutaji wa pili, ambaye yeye hupokea moshi huo kutokana na kuwa jirani nao. Kama mwanasoka anafuatana na marafiki wavutaji basi na yeye ni mvutaji.
1. Mfumo wa fahamu
Kiambata cha Nikotini husababisha uraibu kwa ubongo mchanga wa vijana hatimaye kuleta madhara hasi katika upigaji hatua za ukuaji wa ubongo.
Huathiri umakini wa kiakili katika kutenda mambo mbalimbali na huku ikiathiri hisia na utunzaji wa kumbukumbu. Vile vile huchangia matatizo ya kiakili kama vile woga, hofu na sonona.
2. Mapafu na mirija ya hewa
Aina zote za uvutaji wa mazao ya tumbaku yana athari kubwa katika mapafu ikiwamo kusababisha magonjwa sugu ya mfumo wa mapafu na kifua kikuu.
Kuharibika kwa utendaji kazi wa mapafu kuna athari hasi kwa utimamu kwa mwanasoka ambaye misuli yake inahitaji damu yenye hewa safi ya oksijeni.
3. Moyo na mishipa ya damu
Ni mfumo muhimu unaotawanya damu sehemu mbalimbali mwilini ikiwamo misuli. Kuharibika kwa mishipa ya damu na moyo kunachangia kuchoka kirahisi na kukosa nguvu.
4. Misuli na mifupa
Utumiaji wa tumbaku una athiri kila eneo katika mwilini ikiwamo misuli na mifupa ambayo ndio nyenzo kwa mchezaji kuweza kufanya mambo yote uwanjani.
5. Mfumo wa chakula
Mchezaji mtumiaji bidhaa hizi hukosa hamu ya chakula, Ikumbukwe kuwa mchezaji anahitaji kula lishe bora yenye virutubisho muhimu ili kuweza kuwa na mwili wenye Afya bora.
6. Kupata majeraha kirahisi na kutopona
Mchezaji mvutaji wa 1 au 2 kwa muda mrefu huweza kuwa na kinga dhaifu hatimaye anapopata majeraha ya michezo anachelewa kupona.
Kupungua kwa madini yanayojenga uimara wa mfupa hatimaye kuwa katika hatari ya kupata mivunjiko kirahisi wakati wa kucheza.
Kwa kawaida mwili unapotoka katika mechi au mazoezi makali huhitaji kujihudumia ili kuponesha vijijeraha vya ndani kwa ndani yanayotokea kipindi hiki. Uwezo huu wa mwili unashuka.
7. Kutopata usingizi
Mchezaji anayetumia bidhaa hizo na kupata uraibu huwa ni kawaida kutopata usingizi au kupata usingizi unaokatika katika. Mchezaji asiyepumzika vizuri ni ngumu kupata utimamu wa mwili.