Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Staa Singida BS ataja sababu kubadili uraia kuwa Mtanzania

CAMARA Pict

Muktasari:

  • Lakini kwa Mohammed Damaro Camara, kijana mwenye umri wa miaka 22 kutoka Guinea, hilo ndilo limekuwa jambo kubwa zaidi alilowahi kulifanya kubadili uraia na kuikumbatia Tanzania kama ardhi ya ndoto zake.

NI nadra sana kwa mchezaji wenye umri mdogo kutoka Afrika Magharibi kuhamia kwenye nchi za Afrika Mashariki na si tu kuzoea maisha, bali pia kuamua kuifanya nchi hiyo kuwa nyumbani.

Lakini kwa Mohammed Damaro Camara, kijana mwenye umri wa miaka 22 kutoka Guinea, hilo ndilo limekuwa jambo kubwa zaidi alilowahi kulifanya kubadili uraia na kuikumbatia Tanzania kama ardhi ya ndoto zake.

Katika dunia ya soka, uamuzi wa kubadili uraia mara nyingi huwa unaambatana na matarajio ya mafanikio binafsi au mazingira bora ya maisha, lakini kwa Damaro, hii ni hadithi ya moyo, imani na mapenzi ya kweli kwa taifa lililompokea kama mmoja wao.

Ni simulizi inayovuka mipaka ya soka na kuingia moja kwa moja kwenye misingi ya utu na mshikamano wa kiafrika. Huyu ni mmoja wa wachezaji watatu wa Singida BS ambao kwa pamoja wameamua kubadili uraia wengine ni Emmanuel Keyekeh, ambaye ni raia wa Ghana, Josephat Bada wa Ivory Coast.

Akiwa amevalia jezi ya Singida Black Stars, Damaro hajawa tu kiungo mkabaji wa kuaminiwa, bali amegeuka kuwa nembo mpya ya mabadiliko, mshikamano na matumaini kwa vijana wengi wanaotamani kulifikia soka la juu.

Katika kila pasi, mikimbio, na kila tackle, kuna hadithi ya kujitoa na kutafuta nafasi ya kuandika jina kwenye historia ya taifa alilolipenda.

Katika mahojiano haya Damaro ameeleza kila kona ya maisha yake kutoka mitaa ya Guinea hadi mitaa ya Singida, kutoka kupambana na changamoto ya lugha hadi kutaka kuvaa jezi ya Taifa Stars.

CAMA 05

CHANGAMOTO YA LUGHA

Moja ya changamoto aliyokutana nayo Damaro alipotua Tanzania ilikuwa ni lugha ya Kiswahili na tamaduni za kitanzania. Kiungo huyo anauwezo wa kuongea Kifaransa tu.

Hata hivyo, alithibitisha kuwa ufanisi wa mchezaji unategemea kujitahidi na kujifunza. Alijitahidi kujua Kiswahili japo kwa maneno machache kwa msaada wa wachezaji wenzake, na hii inamsaidia kufanya mawasiliano na wachezaji na viongozi wa timu.

"Lugha ilikuwa changamoto kubwa sana mwanzoni, lakini kwa msaada wa wachezaji wenzangu, nilijitahidi kujifunza na sasa naweza kuelewa baadhi ya maneno hasa yale ya salamu," anasema Damaro.

"Kama mchezaji, ni muhimu kuwa na uwezo wa kuwasiliana na wachezaji wenzako kwa haraka, na hii ilinisaidia kujenga uhusiano mzuri na wachezaji wa Singida japo muda mwingine nimekuwa nikitumia ishara."

Aidha, alizungumzia jinsi alivyoweza kupokea tamaduni za Tanzania, akieleza kuwa chakula na maisha ya kila siku yalikuwa vigumu mwanzoni lakini ameweza kuzoea haraka. Alielezea jinsi tamaduni za Tanzania zilivyomvutia na kumfundisha umuhimu wa umoja na mshikamano kati ya wachezaji na jamii.

"Chakula cha Tanzania kilikuwa kigumu mwanzoni, lakini sasa ninapenda matunda kama vile mapapai na ndizi, na hiyo inafanya maisha yangu kuwa rahisi. Tamaduni za hapa pia zinanivutia sana,” anaongeza Damaro.

CAMA 03

KWANINI SINGIDA BS

Moja ya maamuzi bora kwa Damaro ni kujiunga na Singida Black Stars. Kiungo huyo mwenye miaka 22 anasema kuwa anajivunia kujiunga na timu hiyo kwa sababu ya uongozi wake bora na mchakato mzuri wa usajili.

"Nilichagua Singida Black Stars kwa sababu ya uongozi wa timu na mazungumzo bora niliyokuwa nayo na rais wa klabu. Alikuwa na maono ya mbali, na alinisikiliza na kuniambia kuhusu mipango yao ya baadaye," anasema Damaro.

Damaro aliongeza kuwa ushirikiano wa timu na viongozi wao unamfanya kuwa na morali ya kupigania mafanikio kwa timu hiyo.

Singida Black Stars inajivunia kuwa na kikosi cha wachezaji wenye uwezo wa juu, na Damaro ni mmoja wao. Anaamini kuwa Singida inaweza kuwa moja ya klabu tishio sio tu kwenye ligi ya Tanzania hadi kimataifa.


NDOTO ILIVYOANZA

Damaro anaeleza kuwa safari yake ya soka ilianzia akiwa mdogo katika mji wake wa Guinea, ambapo alijitahidi kupata nafasi katika klabu za ndani ambazo ni Hafia FC na Milo FCkabla ya kuhamia kwenye soko la kimataifa.

Hata hivyo, alikiri kuwa kujenga jina kubwa katika soka la kimataifa lilikuwa ni safari ngumu lakini yenye mafanikio makubwa. Aliendelea kusema kwamba kila hatua aliyopita, alijifunza na kujivunia mafanikio yake.

"Mimi ni mfano wa mchezaji ambaye ameweza kufika mbali kwa jitihada na bidii. Kila hatua inahitajika kuwa na uvumilivu, lakini pia kwa msaada wa wachezaji wenzangu na makocha, ninaamini kuwa soka linaweza kutufikisha mbali,” anasema Damaro.

CAMA 02

SINGIDA NI KAMA MAN CITY

Damaro amefananisha timu yake na Manchester City ya England kutokana na ubora wa kikosi chao na ari waliyonayo.

Akiwa mmoja wa wachezaji tegemeo katika kikosi hicho, Damaro amesema walianza msimu kwa kasi nzuri kabla ya kukumbwa na vipindi vigumu, lakini hilo haliwakatishi tamaa. “Tulianza vizuri sana kwenye ligi, tukawa na mwendelezo mzuri, lakini baadaye changamoto zikatukumba."

Kwa mujibu wa Damaro, Singida Black Stars ni moja kati ya klabu bora kwenye ligi kwa sasa sambamba na Simba, Yanga lakini tofauti yao ni kuwa bado hawana historia ndefu kama vigogo hao wawili.

Hata hivyo, anaamini hilo halizuii ndoto yao ya kufika mbali msimu huu. “Hizi ni klabu kubwa kwenye ligi. Ukiangalia ligi ya England imetawaliwa kwa miaka mingi na timu kongwe lakini ikaibuka Manchester City ambayo kwa sasa ni tishio hata kwa Singida inawezekana ni suala la muda tu," anasema.


LIGI YA TANZANIA

Ligi Kuu Bara ni mojawapo ya mashindano yenye ushindani mkubwa katika ukanda  wa Afrika Mashariki, na Damaro  alikiri kuwa alikumbana na changamoto kubwa alipotua Tanzania.

"Nilijua kuwa ligi ya Tanzania ni ngumu, lakini pia ni ya kupigiwa mfano kwa maendeleo ya wachezaji," anasema Damaro. "Ligi hii imekuwa ni sehemu nzuri ya kuonyesha uwezo wangu na kuchangia mafanikio ya timu yangu. Changamoto zipo, lakini zilikuwa ni sehemu ya ukuaji wangu."

CAMA 01

KUBADILI URAIA

Uamuzi wa kubadili uraia si jambo dogo, lakini kwa kiungo Damaro, ilikuwa ni hatua ya maisha iliyojaa maana. Akiwa ameshamudu mazingira ya Tanzania, si ndani ya uwanja tu bali hata mitaani, Damaro aliamua kusikiliza moyo wake na kukubali kuitwa Mtanzania.

"Maisha ni nafasi, na pale fursa inapojitokeza, kwa nini usiikamate?" anasema Damaro akitabasamu, huku akielezea safari yake ya kutoka kwa mchezaji wa kigeni hadi kuwa mzawa.

Damaro anakiri kuwa haikuwa ndoto yake kuichezea Tanzania, lakini maisha yalimpeleka kwenye njia hiyo ambayo leo anaiona kama baraka. "Sikuwa nimeota kuchezea Tanzania, lakini ilipotokea, nilijua ni nafasi ya kipekee. Hakuna ajuaye hatima yake, na soka limenifundisha kuwa na moyo wa kupokea mabadiliko," anasema.

Uamuzi huo ulimfanya ajikute katika ukurasa mpya wa maisha yake, akiwa si tu mchezaji wa kulipwa, bali balozi wa nchi ambayo awali aliijua kwa jina tu.

Anasema kilichomgusa zaidi ni utulivu wa maisha, mapokezi ya Watanzania, na tamaduni zilizomfanya ajihisi kama yuko nyumbani. "Nilipenda sana utamaduni wa Watanzania. Jinsi wanavyoishi, wanavyopendana na namna walivyonikubali, yote hayo yalinifanya nione sababu ya kuchukua uraia," anasema.


AITAKA NAMBA STARS

Damaro ameweka wazi malengo yake ya muda mrefu katika soka kuwa ni kuichezea timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, na kupata hadhi ya mchezaji wa kimataifa anayetambulika kwenye ramani ya dunia.

Akiwa mchezaji aliyeonyesha kiwango bora akiwa na Singida Black Stars, Damaro amesema uamuzi wake wa kubadili uraia haukuwa tu wa kawaida, bali ni sehemu ya kujitolea kwa taifa ambalo limekuwa nyumbani kwake kwa sasa.

“Ndio, lengo langu ni kuchezea timu ya taifa ya Tanzania na pia kupata ule msisimko wa kuwa mchezaji wa kimataifa,” anasema Damaro.

Kwa Damaro, kuvaa jezi ya Taifa Stars kutakuwa ni heshima kubwa na hatua muhimu katika taaluma yake ya soka. Anaamini kuwa kwa kujitoa kwake kila siku mazoezini na uwanjani, siku moja jina lake litasikika likiimbwa na mashabiki wa Taifa Stars kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa au hata nje ya mipaka ya nchi.

“Ni zaidi ya soka, ni kuhusu kuwawakilisha watu na taifa ambalo limeamua kunipa nafasi. Hicho ni kitu kikubwa,” anasisitiza.

Kwa sasa, anachokifanya ni kuhakikisha anakuwa kwenye ubora wa hali ya juu kila wiki akiwa na klabu yake, huku akifahamu kuwa macho ya makocha wa timu ya taifa yako uwanjani. “Najua nafasi haziwi nyingi, lakini nipo tayari. Nitafanya kila linalowezekana kuhakikisha ndoto hiyo inatimia.”

CAMA 04

ANAVYOISHI KISHUA

Ukweli ni kwamba Damaro, ni miongoni mwa wachezaji wa Singida BS wanaoishi maisha ya daraja la juu kabisa. Akiwa ni mmoja wa wachezaji wa kimataifa waliowahi kuvutia macho ya mashabiki kutokana na kiwango chake uwanjani, maisha ya nje ya dimba yanamuweka kwenye daraja la juu pia daraja la wachezaji wanaojali hadhi yao, taswira yao, na utulivu wa maisha yao ya kila siku.

Damaro anakaa mtaa wa Singidani, eneo linalojulikana kwa mandhari ya kuvutia na nyumba za kisasa. Anakaa kwenye moja ya mijengo ya kifahari yenye flow mbili, ambapo ghorofa ya juu ni maskani yake huku ghorofa ya chini akiishi mchezaji mwenzake. Jengo hilo ni la kisasa, lenye usalama wa kutosha, mwonekano mzuri, na mazingira yanayotoa nafasi ya kupumzika kwa utulivu baada ya mazoezi au mechi ngumu.

Kama ilivyo kwa baadhi ya wachezaji wanaotambua thamani ya muda na uhuru wa harakati binafsi, Damaro anamiliki usafiri wake binafsi kwa ajili ya mizunguko ya hapa na pale kama ilivyo kwa wachezaji wengine wa kikosi cha kwanza.

Picha ya Damaro mitaani ni tofauti kabisa na ile wanayoijua mashabiki uwanjani. Huko, anajulikana kwa utulivu, staha na heshima kwa watu wanaomzunguka. Si mtu wa kelele wala kujionyesha kupita kiasi, bali huonekana kwenye maeneo ya kawaida ya chakula au maduka, akiwa mnyenyekevu lakini mwenye muonekano unaoonyesha kuwa ni mtu anayejitambua.

Moja ya vitu vinavyomtofautisha Damaro na wachezaji wengine ni mtazamo wake wa maisha. Anaamini nidhamu nje ya uwanja ni silaha muhimu kwa mafanikio ndani ya uwanja. Ndiyo maana hata anapokaa nyumbani kwake, anapenda utulivu, hutumia muda mwingi kusikiliza muziki laini au kuangalia mechi mbalimbali ili kuongeza uelewa wa mchezo wake.