Sterling, Paige ni mwanzo, kati na mwisho!
Muktasari:
- Sterling ambaye amezichezea klabu kadhaa zikiwemo Liverpool, Manchester City, Chelsea na Arsenal, yeye na Paige tayari ni wazazi wenza wakiwa na watoto wawili ingawa bado hawajafunga ndoa hadi kufikia sasa.
WINGA wa zamani wa timu ya taifa ya England, Raheem Sterling, kwa muda mrefu amekuwa katika uhusiano na Paige Milian ambaye walifahamiana kabla mchezaji huyo hajapata umaarufu na mafanikio katika soka la kulipwa.
Sterling ambaye amezichezea klabu kadhaa zikiwemo Liverpool, Manchester City, Chelsea na Arsenal, yeye na Paige tayari ni wazazi wenza wakiwa na watoto wawili ingawa bado hawajafunga ndoa hadi kufikia sasa.
Uhusiano wao unajulikana na kufuatiliwa na mashabiki kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ambapo wao wenyewe wametoa fursa hiyo kwa miaka mingi ingawa baadhi ya mambo muhimu kuhusu maisha ya familia yao yameendelea kubaki kuwa siri.
Paige alikutana na kufahamiana na Sterling wakati mchezaji huyo alipokuwa akijifua katika akademi ya klabu ya Queens Park Rangers (QPR), wote wawili walikuwa bado vijana wadogo sana, mathalani Sterling alikuwa kwenye umri wa miaka 15 hivi.
Muda mfupi baada ya kufahamiana, Sterling aliondoka QPR na kujiunga na Liverpool, ambapo aliendelea kufanya vizuri huku akizidi kukua kisoka na kuwa miongoni mwa washambuliaji mahiri wa England.
Hatua hiyo ilifanya Paige kuacha kazi katika duka la vifaa vya michezo na kuhamia jijini Liverpool ili kuwa karibu na Sterling. Hata hivyo, waliachana na kuja kurudiana kipindi mchezaji huyo anajiandaa kujiunga na Man City mwaka 2015.
Kwa hiyo uhusiano wao ulikuwepo kabla ya Sterling kupata mafanikio makubwa akiwa Man City na alishinda taji la Ligi Kuu England (EPL) kwa mara nne chini ya kocha Pep Guardiola ambaye aliondoka katika klabu hiyo msimu uliopita.
Hata sasa na Sterling hana klabu ya kuichezea, bado Paige anaendelea kusalia kuwa mpenzi wake. Paige ameshudia hatua za awali kabisa za Sterling katika soka la kulipwa, mafanikio ya juu zaidi, na sasa ambapo anaelekea kuhitimisha safari yake ya soka kama mchezaji.
Utakumbuka baada ya Sterling kucheza Arsenal kwa mkopo, Chelsea ilitangaza kuachana naye kwa makubaliano ya pande zote mbili mnmo Januari 2026. Baadaye, Feyenoord ya Uholanzi ilimsajili kwa mkataba uliomalizika mwishoni mwa msimu wa 2025/26.
Sterling alimchumbia Paige mnano Machi 2018 ambapo alimvisha pete kubwa ya almasi. Wawili hao walipanga kufunga ndoa mwaka 2020, lakini mipango yao iliahirishwa kutokana na janga la Covid-19, na hadi sasa hakuna taarifa za mipango mingine ya ndoa.
Hivyo licha ya kuwa pamoja kwa miaka zaidi ya 10 na kujaliwa watoto wawili, bado Paige anatambulika kama mchumba wa Sterling na si mke. Watoto wao wa kwanza, Thiago alizaliwa Januari 2017, na wa pili, Thai alizaliwa Mei 2019.
Hata hivyo, Sterling ana mtoto mwingine aitwaye Melody Rose aliyezaliwa Juni 2012. Mtoto huyu wa kike alizaliwa katika uhusiano wa mchezaji huyo na mwanamke mwingine aitwaye Melissa Clarke na ndiye mtoto pekee wa kike wa Sterling.
Katika Kombe la Dunia 2022, Paige alibaki nyumbani na watoto wao, na hiyo ndio ilikuwa michuano ya mwisho ya kimataifa kwa Sterling kuichezea timu yake ya taifa ya England.
Wakati wa michuano hiyo iliyofanyika Qatar, nyumba ya familia yake ilivamiwa na kuibiwa vitu vya thamani lakini hakuna mtu aliyeumizwa.
Paige ni mwanamke kutokea Uingereza anayefanya biashara na amefahamika na wengi kupitia uhusiano wake wa muda mrefu na Sterling.
Taaluma yake ni mhasibu na amekuwa akiitumia vizuri katika biashara zake.
Amekuwa akijitenga sana na maisha ya umaarufu tofauti wapenzi wa mastaa wengi wa soka, haonekani akitafuta umaarufu kupitia mchezaji huyo, yeye yupo bize na familia na biashara zake.
Paige na Sterling ni wamiliki wa kampuni ya Milian Property Group Limited ambayo inajishughulisha na biashara ya majengo. Paige ndiye mwanzilishi wa kampuni hiyo na ndio sababu imebeba jina lake la pili, yaani Milian.
Katika mitandao ya kijamii, Paige amefanikiwa kukusanya wafuasi zaidi ya 100,000 kwenye ukurasa wake wa Instagram ambao mara nyingi anautumia kuposti picha akiwa pamoja na watoto wake, familia na miradi yake mbalimbali.