Prime
Ubingwa Arsenal ni kuamini katika mchakato
WIKI iliyopita Arsenal ilifikia mafanikio ambayo imekuwa ikiyasaka kwa miaka 22, lakini ikaja kuwa na mpango mkakati mwaka 2019 ilipomuajiri mchezaji wake wa zamani, Mikel Arteta awe kocha wake mkuu, huku mchezaji mwenzake wa zamani, Edu akiwa mkurugenzi wa ufundi.
Ni matokeo ya mpango wa hatua tano uliobuniwa na Edu na baadaye kurekebishwa baada ya Arteta kuajiriwa. Edu, ambaye alikuwamo kwenye kikosi cha Arsenal kilichotwaa ubingwa mara mbili, alianza mpango wake kwa kupendekeza kuajiriwa kwa kocha Unai Emery.
Hata hivyo, baada ya kumaliza msimu mmoja mambo yalionekana kwenda kombo na hivyo Emery akatimuliwa. Edu, raia wa Brazil alimtafuta Arteta na baada ya mazungumzo kujua kama angekuwa tayari kumalizia vizuri ndipo walipokutana na kumpa mkakati huo wa hatua tano.
Waliusoma pamoja, kujadiliana na kufanya marekebishona ndipo Arteta alipoutangaza katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari baada ya kuajiriwa.
Mpango huo ulihusisha kipindi kigumu na katili cha kuondoa wachezaji wakongwe waliokuwa wakilipwa mishahara mikubwa. Hatua hiyo ya kwanza ilihusisha wachezaji kama Mezut Ozil, Willian, Pierre-Emerick Aubemeyang, Henrich Mikhitaryan, Sokratis Papastathopoulos na Hector Ballerin. Baadaye akafuata Micolas Pepe ambaye wakati huo ndio alikuwa mchezaji ghali.
Hatua ya pili ilikuwa ni kusajili wachezaji vijana wenye umri chini ya miaka 24 na ambao walinunuliwa kwa bei rahisi. Wachezaji kama Ben White, Martin Odergaard na Aaron Ramsdale waliwasili katika hatua hii, huku kuibuka kama Bukayo Saka na Emily-Smith Rowe kutoka shule ya Arsenal ya Hale End kuliimarisha hatua hiyo. Hatua ya tatu ilikuwa ni kuongeza ubora zaidi kwenye timu.
Hapa walihusika wachezaji kama mshambuliaji mkongwe Mbrazili Gabriel Jesus na beki kiraka Oleksandr Zinchenko ambaye alikuwa na uzoefu wa Ligi Kuu. Wawili hao na wengine walisaidia kuongeza akili ya ushindi na uzoefu.
Katika hatua ya nne, Arteta na Edu walikubaliana kuwa kulikuwa na haja ya kusajili mchezaji nyota wa England ambaye ana heshima na sifa njema kila sehemu; kwa vyombo vya habari, ndani ya klabu katika kila jambo “kwa sababu sisi ni klabu ya England na tunahitaji kuwa na mchezaji bora wa England kwenye kikosi chetu kama Saka,” kwa mujibu wa Edu alipoongea na ESPN.
Kwa kifupi Edu alifupisha mpango huo kwa kuuita “mlete Declan Rice hapa.” Rice alinunuliwa kutoka West Ham kwa ada iliyoweka rekodi ya klabu ya Pauni 105 milioni. Baadaye akanunuliwa Kai Harvertz na hapo kikosi kikaanza kuimarika.
Wengine walioingia kipindi hicho ni Jurien Timber na kipa David Raya.
Edu aliondoka mwaka 2024 na nafasi yake kuchukuliwa na Andrea Berta wa Hispania, ambaye msimu wake wa kwanza wa usajili aliwanunua wachezaji kama Victor Gyokeres, Martin Zubimendi, Eze, Madueke na Piero Hincapie ambaye kwanza alichukuliwa kwa mkopo.
Hatua ya mwisho ilikuwa ni kujenga utamaduni wa kushinda na njaa ya vikombe.
Hatua hiyo ndiyo iliyowawezesha kuweka ushindani thabiti kwenye ubingwa kiasi cha kushika nafasi ya pili mara tatu mfululizo, wakikosa ubingwa mwishoni mwa msimu kwa kupoteza mechi.
Wakati wote walipopoteza mechi za mwezi Machi na Aprili ambazo ni muhimu katika mbio za ubingwa, Arsenal walidhihakiwa, huku Arteta akikumbana na maswali mengi kuhusu mchakato huo wa hatua tano, lakini aliamua kujibu kwa kifupi na hata baada ya kuinshida West Ham siku moja kabla ya Manchester City kupoteza pointi mbili zilizoipa Arsenal ubingwa, kocha huyo Mhispania alikwepa swali kuhusu mpango huo.
Hata hivyo, mbele ya mmiliki wa wa klabu hiyo, Kroenke na mtoto wake, Arteta na Edu walitetea mpango huo kwa hoja na kuonyesha imani yao kuwa ungezaa matunda ambayo walikuwa wakiyawazia.
Huu ni mfano mzuri wa kuwa na imani katika mchakato (trust the process) na kuvumilia vikwazo vinavyojitokeza katikati.
Viongozi wengi wa klabu kubwa huwa hawana uvumilivu wa namna hiyo. Wengi wanataka matokeo ya haraka bila ya kufanya tathmini ya hali ya klabu na kujua inahitaji dawa gani. Kutoka kiwango cha kugombea ubingwa hadi kushika nafasi ya kumi, hakukuhitaji mpango wa matokeo ya haraka.
Kulihitaji mpango mkakati ambao mchakato wake unahitaji muda kuutekeleza.
Na leo Arsenal, si tu imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England kwa mara ya 14 baada ya kuukosa kwa miaka 22, bali Mei 30 itakuwa inajaribu kutwaa kwa mara ya kwanza ubingwa wa Ulaya.