Prime
Pole sana Metacha, hata Okello alitumia akili
Kwanza nianze kwa kumpa pole kipa wa Singida Black Stars, Metacha Mnata, si kwa kuruhusu bao la kwanza la mkwaju wa adhabu uliopigwa na Allan Okello wa Yanga, bali kwa hatua zilizofuata baada ya kufanya kosa hilo.
Mnata alidhani amewapanga vizuri mabeki wake upande wa kushoto kwake wakati wa adhabu hiyo na hivyo kuacha eneo kubwa upande huo akijua mpigaji atapata shida kuupitisha mpira juu ya ukuta huo au pembeni mwao, jambo ambalo lingesababisha mpira ama kupaa juu ya goli au kwenda pembeni ya goli kama mpigaji hana shabaha wala stadi ya kuupindisha mpira usipae au kwenda nje.
Lakini Okello hakutamanishwa na ukubwa wa eneo la kushoto lililoachwa na kipa na badala yake akaamua kuupeleka mpira upande uleule aliokuwa amesimama Metacha.
Lakini bado kipa huyo wa zamani wa Yanga akaona Mganda huyo anepiga mpira upande wa kushoto wa goli na hivyo wakati Okello anapiga, tayari Metacha alishanyanyua mguu wa kushoto kujiandaa kuruka.
Hilo likawa kosa kubwa kuotea Okello angepiga kushoto kwake na ndiyo maana ilikuwa shida kwake kurudi upande wa kulia na hivyo kuishia kuukodolea macho mpira wakati ukijaa wavuni.
Ni pigo la kawaida na hasa kwenye mipira ya penati ambako mpigaji humhadaa kipa au kipa huotea na kwenda upande tofauti na ule aliodhani mpira ungepelekwa.
Katika mipira ya adhabu nyingine karibu na lango, nyuma ya mpira husimama kuanzia watu wawili na mara nyingine mmoja hutangulia na kuuruka mpira kumpoteza kipa, au mwingine husogelea mpira kama anataka kupiga lakini hurudi nyuma kumuachia mpira mpigaji ili kusumbua akili ya kipa.
Ungetegemea benchi la ufundi limtulize Metacha, lakini mara moja kocha akaamuru kipa mwingine aanze kupasha joto mwili na baadaye kumuita nje kipa huyo aliyefungwa.
Lilikuwa ni tukio la kikatili kwa mchezaji anayefanya kosa kubwa au anayedhaniwa amefanya kosa kubwa, kutolewa nje mara baada ya tatizo hilo.
Kwa kawaida kitendo hicho humsababishia fedheha kubwa mchezaji anayetolewa, humdhalilisha kwa mashabiki na kinaweza kumsababishia mchezaji kufikiria kupita kiasi na kufanya makosa zaidi katika mechi zinazofuata.
Pia kitendo hicho huweza kumsababishia mchezaji kujenga hofu ya kubadilishwa na hivyo kuwa makini kupita kiasi na kuepuka kujaribu jambo kubwa kwa hofu anaweza kufanya kosa jingine na hivyo kuiweka timu yake hatarini zaidi.
Kwa mfano kwa kipa kama huyo, anaweza kuona kutoka golini ili kuongeza idadi ya mabeki wakati wanamiliki mpira eneo lao, ni hatari na hivyo kusalia golini hata pale anapohitajika.
Hatua kama hiyo huweza kusababisha kushusha morali wa timu.
Kama wachezaji wataoana kocha ana tabia ya kutafuta kisingizio cha kufanya vibaya badala kuwa pamoja nao, morali utashuka na kuondoa Imani kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Zaidi ya yote, hatua hiyo inaweza kutuma ujumbe mzito hakuna mchezaji mkubwa kuliko timu na wanatakiwa wacheze kwa viwango vya juu.
Mabadiliko ya haraka pia hufinya idadi ya wachezaji ambao kocha alitarajia kuwatumia kutoka benchi na hivyo kuvuruga mpango wake wa mechi.
Hata hivyo, wakati mwingine mabadiliko ya haraka pale mchezaji anapofanya kosa huweza kuiimarisha nafasi aliyokuwa akicheza.
Makocha kama Alex Ferguson na Pep Guardiola walitumia mbinu hiyo. Ferguson aliita “hair dryer treatment”, yaani kukausha nywele kwa kutumia mashine.
Hata hivyo, makocha wa kisasa na wanasaikolojia hawatumii mbinu hizo na mara nyingi hupendelea kumuacha mchezaji uwanjani ili ajenge kujiamini na kumua kushughulikia suala hilo sakati wa mapumziko au mazoezini ili kulinda maendeleo ya mchezaji ya muda mrefu.
Nimeona Metacha ameomba radhi kwa kitendo chake cha kutaka kugoma kutoka uwanjani kabla ya kushauriwa na wenzake kutoka.
Nahisi wakati wakimsihi atoke pengine kuna busara zilitumika kuelezea kwa nini anatakiwa kumtii kocha nap engine hizo na mazungumzo ya baadaye yamemsaidia kipa huyo kurudi katika hali yake na kuomba radhi.
Siwezi kulishauri benchi la ufundi la Singida Black Stars lisifanye tena mabadiliko ya haraka kama hayo, bali nachoweza kumpa pole na kumtia moyo Metacha kwa tukio hilo la kumfedhehesha la kumtoa bila ya kutafakari kwa kina madhara yake na pia kuona kwa karibu tukio hilo lilikuwaje.
Najua fikra za wengi zikajikita kwenye kupanga matokeo, kubeti na ujinga mwingine mwingi, lakini huu ni wakati wa Metacha kuwa imara kisaikolojia na kiakili.
Najua mazungumzo wakati wa mechi hiyo yalikuwa kwamba Metacha alipanga vibaya ukuta, lakini picha za marudio zilionyesha alipanga vizuri kuzuia upande wake wa kushoto akijiamini angeweza kulinda upande wa kulia, lakini mpigaji akatumia akili kubwa zaidi.
Yako matukio mengi ya makipa kufungwa mabao ya namna hiyo, tena makipa wakubwa wa hapa Tanzania, Afrika na duniani.
Lakini nyakati nyingine ni muhimu pia kummwagia sifa mpigaji adhabu. Sio kila mara kipa akipanga ukuta basi mpira hauwezi kuingia golini. Na wapigaji nao hutumia muda mwingi kuangalia ni sehemu gani ataweza kupitisha mpira baada ya kipa kupanga wachezaji wake.