Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usilale na mapambo, madhara yake ni mengi

KULALA Pict

Muktasari:

  • Kuanzia maambukizi ya ngozi, maumivu ya masikio hadi matatizo ya mzunguko wa damu, wataalamu wa afya wanaonya kuwa ni vyema kuvua mapambo hayo kabla ya kwenda kitandani.

Unaweza kuona ni jambo la kawaida kulala ukiwa umevaa hereni, cheni, vikuku au pete zako uzipendazo. Wapo wanaofanya hivyo kwa mazoea, wengine kwa kuhofia kupoteza mapambo yao, lakini unajua tabia hiyo inaweza kuwa chanzo cha matatizo mbalimbali ya kiafya?

Kuanzia maambukizi ya ngozi, maumivu ya masikio hadi matatizo ya mzunguko wa damu, wataalamu wa afya wanaonya kuwa ni vyema kuvua mapambo hayo kabla ya kwenda kitandani.

Ingawa wengi huyaona kama sehemu ya urembo au utambulisho wao, ukweli ni kuyavaa wakati wa usingizi kunaweza kuathiri mwili kwa namna mbalimbali bila mtu kutambua mapema.

USING 03

MAAMBUKIZI YA NGOZI

Mapambo hukusanya jasho, mafuta ya mwili, vumbi na bakteria kwa siku nzima. Unapolala navyo, bakteria hao hubaki karibu na ngozi kwa muda mrefu zaidi na kuongeza hatari ya kupata maambukizi.

Pia sehemu za mwili zinazogusana moja kwa moja na hereni, cheni au vikuku zinaweza kuendelea kuwa na unyevunyevu kutokana na jasho, hali inayorahisisha ukuaji wa vijidudu vinavyoweza kusababisha matatizo ya ngozi.


MZIO WA NGOZI

Baadhi ya material zinazotumika kutengeneza hereni, pete au vikuku zinaweza kusababisha kuwashwa, vipele, wekundu wa ngozi au uvimbe kwa watu wenye ngozi nyeti.

Tatizo hili huwa kubwa zaidi kwa watu wanaolala na mapambo hayo kila siku kwa sababu ngozi hukaa muda mrefu ikigusana zinazoweza kuisababishia muwasho. Dalili zinaweza kuanza taratibu na baadaye kuwa tatizo kubwa ikiwa hatua hazitachukuliwa mapema.

USING 02

MAUMIVU YA MASIKIO

Hereni hasa kubwa au nzito zinaweza kubana sikio dhidi ya mto wakati wa usingizi na kusababisha maumivu au muwasho unaoweza kudumu hata baada ya kuamka. Kwa baadhi ya watu, maumivu hayo yanaweza kuambatana na uvimbe mdogo au hisia za kuchomachoma kwenye sehemu ya sikio iliyoathirika. Hali hii hujitokeza zaidi kwa watu wanaopendelea kulalia upande mmoja kwa muda mrefu.


KUPUNGUA KWA MZUNGUKO WA DAMU

Pete, vikuku au saa zinazobana zinaweza kuathiri mzunguko wa damu mikononi na vidoleni, hali inayoweza kusababisha ganzi na maumivu. Wakati wa usingizi mwili hubadilisha mkao mara nyingi na wakati mwingine sehemu fulani za mwili huvimba kidogo. Ikiwa pete au kikuku kimekaza, hali hiyo inaweza kuongeza usumbufu na kuathiri mtiririko wa kawaida wa damu.


MAJERAHA MADOGO

Wakati wa kujigeuza usingizini, hereni au vikuku vinaweza kunaswa kwenye shuka, mto au nguo na kusababisha michubuko au kuchanika kwa ngozi. Ingawa majeraha haya mara nyingi huwa madogo, yanaweza kuwa mlango wa maambukizi endapo sehemu husika haitatunzwa vizuri. Watoto na watu wanaotumia mapambo makubwa wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata tatizo hili.

USING 01

SHINGO KUWASHA

Cheni zinazobaki shingoni muda mrefu zinaweza kusababisha msuguano wa ngozi na kusababisha muwasho au alama shingoni.

Kadri mtu anavyojigeuza akiwa amelala, ndivyo cheni inavyoendelea kusugua ngozi. Kwa watu wenye ngozi nyeti, hali hiyo inaweza kusababisha wekundu, vipele au kuwashwa kwa muda mrefu.


USINGIZI USIO NA UBORA

Mapambo yanayobana au kusumbua mwili yanaweza kukufanya uamke mara kwa mara usiku bila kujua chanzo chake, jambo linalopunguza ubora wa usingizi. Usingizi bora ni muhimu kwa afya ya mwili na akili, hivyo kitu chochote kinachosababisha usumbufu wakati wa kulala kinaweza kuathiri mapumziko ya mwili na uwezo wa kuamka ukiwa na nguvu siku inayofuata.