Vaa utokelezee usionekane mzee
Muktasari:
- Tatizo mara nyingi siyo umri, bali ni namna mtu anavyojisitiri. Watu wengi wakifikisha umri fulani huanza kuamini kwamba kuvaa nguo za kisasa siyo kwao tena. Matokeo yake huvaa mavazi yanayowafanya waonekane wakubwa kuliko umri wao halisi.
Jamani, kuna watu ukikutana nao unaweza ukaapa wana miaka 35, halafu ukija kuuliza unaambiwa tayari wana wajukuu watatu.
Wakati huo huo wewe mwingine ana miaka 42 tu, lakini ukimuona unaweza kudhani ameshastaafu kazi miaka mingi iliyopita.
Tatizo mara nyingi siyo umri, bali ni namna mtu anavyojisitiri. Watu wengi wakifikisha umri fulani huanza kuamini kwamba kuvaa nguo za kisasa siyo kwao tena. Matokeo yake huvaa mavazi yanayowafanya waonekane wakubwa kuliko umri wao halisi.
Ukweli ni kwamba, huwezi kuzuia umri kuongezeka, lakini unaweza kuchagua mavazi yanayokufanya uonekane mwenye nguvu, nadhifu na mwenye mvuto wa ujana.
Huhitaji kutumia fedha nyingi wala kubadilisha kabati lote la nguo. Unahitaji tu kufanya uchaguzi sahihi wa mavazi na kuyavaa kwa kujiamini.
CHAGUA NGUO ZINAZOKUTOSHA VIZURI
Nguo zinazobana kupita kiasi zinaweza kufanya mwili uonekane hauna uwiano, wakati nguo pana sana hukufanya uonekane mkubwa na mzito kuliko ulivyo. Suluhisho ni kuvaa nguo zinazokutosha vizuri.
Shati, suruali au gauni vinatakiwa kukaa mwilini kwa nafasi bila kukubana wala kukulegea kupita kiasi. Mavazi ya aina hii huufanya mwili uonekane wenye mpangilio mzuri na hukupa mwonekano wa kisasa unaovutia.
RANGI ZENYE MVUTO
Rangi unazochagua zina mchango mkubwa kwenye mwonekano wako. Watu wengi wakizeeka hukimbilia kuvaa nguo nyeusi au za rangi zilizofifia kila siku.
Jaribu kuvaa rangi kama bluu, kijani, cream, nyeupe, daki bluu au kahawia na nyepesi. Rangi hizi huleta mwonekano wenye mvuto sana na kukufanya uonekane mwenye uchangamfu bila kupoteza heshima ya umri wako.
USIVAE MAVAZI YENYE MAMBO MENGI
Nguo zenye michoro mikubwa, maandishi mengi au mapambo yaliyopitiliza mara nyingi hufanya mwonekano uonekane umechanganyika.
Badala yake, chagua nguo zenye muundo rahisi na wenye mpangilio. Mavazi ya aina hii yanaonekana ya kisasa na yanakupa sura safi inayovutia macho.
CHAGUA VIATU VYA KISASA
Watu wengi huwekeza kwenye nguo nzuri lakini husahau viatu. Ukweli ni kwamba viatu vinaweza kubadilisha kabisa mwonekano wako.
Sneakers safi za rangi nyeupe, viatu vya ngozi vilivyotunzwa vizuri au sendo za kisasa vinaweza kukufanya uonekane mdogo kwa umri bila kuonekana unajilazimisha kutembea. Hakikisha viatu vyako vinakuwa safi kila unapovitumia.
VAA JEANS, PUNGUZA NGUO ZA VITAMBAA
Jeans siyo za vijana pekee. Mzee anaweza kuvaa jeans na akaonekana nadhifu sana ikiwa amechagua aina sahihi.
Epuka jeans zilizochanika sana au zilizobana kupita kiasi. Chagua jeans za bluu au nyeusi ambazo zinakaa vizuri mwilini. Ukiunganisha na shati au fulana nzuri utapata mwonekano wa kisasa unaovutia.
CHANGAMYA MAVAZI KIDOGO
Kuvaa koti jepesi juu ya fulana, shati juu ya T-shirt au blazer nyepesi kunaongeza mvuto wa mavazi yako.
Hii huleta mwonekano wa kisasa na hukufanya uonekane mwenye mvuto unapozivaa.
Hakikisha tu rangi za nguo zako zinaendana ili usionekane umevaa rangi moja au mchanganyiko mwingi kwa wakati mmoja.
HIVI USIVISAHAU
Saa nzuri, mkanda wa ubora, miwani ya jua na pochi au mkoba(pochi) nzuri vinaweza kufanya mavazi yako yaonekane ya thamani zaidi.
Usitumie urembo mwingi kwa wakati mmoja. Kitu kidogo lakini chenye ubora huwa kinavutia zaidi kuliko kujaza mapambo mengi yasiyoendana.
USAFI MUHIMU
Unaweza kuvaa nguo ya gharama kubwa, lakini ikiwa imekunjamana au inaonekana chafu, haitakupa mwonekano mzuri.
Nguo safi, zilizopigwa pasi na zinazotoa harufu nzuri hukufanya uonekane unapenda mwonekano wako. Hilo pekee linaweza kukupa sura ya ujana na kujiamini zaidi.
UKIZIDISHA UTAHARIBU
Kuvaa kisasa hakumaanishi kila mtindo unaotoka kwenye mitandao ya kijamii. Chagua mavazi yenye muonekano wa kisasa lakini yanayolingana na umri wako.
Hii itakufanya uonekane mwenye mvuto bila kuonekana kama unajaribu kuiga vijana kwa nguvu. Mwishowe, siri ya kuonekana kijana haipo kwenye umri bali ipo kwenye namna unavyojitunza na kujisitiri.
Mavazi yanayokutosha, rangi sahihi, viatu vizuri na usafi wa nguo vinaweza kubadilisha kabisa mwonekano wako.