Walipo mastaa Arsenal waliocheza fainali Ulaya miaka 20 iliyopita
Muktasari:
- Timu zote mbili zilikwenda kwenda fainali hiyo zikitoka kuchukua ubingwa wa ligi za ndani ya nchi, huku PSG ikiwa pia ndiye bingwa mtetezi wa mashindano hayo makubwa kabisa kwa ngazi ya klabu barani humo ilioubeba msimu uliopita.
LONDON, ENGLAND: JUMAMOSI iliyopita Arsenal ilishindwa kubeba ubingwa wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kupoteza kwa penalti 4-3 dhidi ya PSG katika Uwanja wa Puskas uliopo Budapest, Hungary. Timu hizo zilifungana bao 1-1 hadi muda wa kawaida ulipomalizika na hivyo kulazimika kwenda katika matuta.
Timu zote mbili zilikwenda kwenda fainali hiyo zikitoka kuchukua ubingwa wa ligi za ndani ya nchi, huku PSG ikiwa pia ndiye bingwa mtetezi wa mashindano hayo makubwa kabisa kwa ngazi ya klabu barani humo ilioubeba msimu uliopita.
Lakini, nyuma ya safari hiyo ya Arsenal ilitanguliwa na ile fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Mei 17, 2006 ambayo ni miongoni mwa kampeni zinazokumbukwa zaidi katika historia ya klabu hiyo. Mwaka huo kikosi cha Arsene Wenger kilifika fainali ya Ulaya kwa mara ya kwanza kikionyesha uimara mkubwa wa safu ya ulinzi njiani na kufungwa kwa mbinde na Barcelona mjini Paris, Ufaransa.
Licha ya Sol Campbell kuifungia Arsenal bao la kwanza, lakini mabao ya Samuel Eto'o na Juliano Belletti katika kipindi cha pili yalihakikisha Barcelona inashinda 2-1. Arsenal ilikuwa na mchanganyiko wa wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa kimataifa pamoja na vipaji vilivyokuwa vinachipukia, wengi wao wakifurahia maisha marefu ya soka barani Ulaya na kwingineko.
Miaka 20 baadaye, wachezaji wa kikosi cha kwanza pamoja na wale walioingia kama wa akiba wamechukua njia tofauti kabisa baada ya kuondoka kaskazini mwa London. Kutoka ukocha, uchambuzi wa soka, biashara hadi changamoto za maisha binafsi hapa tunaangalia walipo sasa wachezaji wa Arsenal waliofika fainali ya Ligi ya Mabingwa 2006.
Kikosi cha kwanza (mfumo 4-4-2)
JENS LEHMANN (Kipa – Ujerumani)
Ilipofika fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza Lehmann alikuwa katika msimu wake wa tatu Arsenal. Alikuwa mhimili muhimu wa safari hiyo na aliweka rekodi ya kutoruhusu mabao katika mechi 10 mfululizo kwenye mashindano hayo. Baada ya kuhamia Stuttgart, alitangaza kustaafu 2010, lakini alirejea Arsenal kwa muda kutokana na tatizo la majeraha kwa makipa. Alicheza mechi moja dhidi ya Blackpool kabla ya kustaafu rasmi. Mwaka 2020 alijiunga na Hertha Berlin katika bodi ya usimamizi, lakini alifukuzwa mwaka mmoja baadaye baada ya kutuma ujumbe uliotafsiriwa kuwa wa kibaguzi kwa mchambuzi Dennis Aogo. Kwa sasa anafanya kazi kama mchambuzi wa televisheni nchini Ujerumani.
EMMANUEL EBOUE (Beki wa Kulia – Ivory Coast)
Eboue aliondoka Arsenal 2011 na kujiunga na Galatasaray ya Uturuki, ambako alishinda mataji kadhaa. Mwaka 2016 alisaini Sunderland, lakini akaachwa baada ya Fifa kumpiga marufuku ya mwaka mmoja kutokana na mgogoro na wakala wake wa zamani.
Baadaye alikumbwa na matatizo makubwa binafsi ya maisha, ikiwemo talaka iliyomfanya kupoteza nyumba, magari na fedha nyingi. Changamoto hizo ziliathiri afya yake ya akili, jambo ambalo amekuwa akilizungumza wazi ili kuhamasisha wachezaji kutafuta ushauri wa kifedha.
Mwanawe Mathis, ambaye hawana mawasiliano ya karibu alijiunga na akademi ya Chelsea 2025 na hivi karibuni aliitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha wakubwa.
KOLO TOURE (Beki wa Kati – Ivory Coast)
Toure aliondoka Arsenal kwenda Manchester City 2009 baada ya kucheza mechi 326. Akiwa City alishirikiana na mdogo wake Yaya Toure kusaidia klabu hiyo kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England 2012. Baada ya kucheza Liverpool na Celtic, alistaafu 2017 na kuingia moja kwa moja kwenye ukocha. Hivi karibuni alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la Manchester City, ingawa klabu hiyo imetangaza ameondoka baada ya Pep Guardiola kusepa.
SOL CAMPBELL (Beki wa Kati – England)
Licha ya kufunga katika fainali, Campbell alikuwa na msimu mgumu kutokana na majeraha na kushuka kiwango. Aliondoka Arsenal kwenda Portsmouth 2006, baadaye akarudi Arsenal kwa kipindi kifupi kabla ya kumalizia soka Newcastle United. Alijaribu kuingia kwenye siasa, lakini hakufanikiwa. Pia amefundisha Macclesfield na Southend. Hivi sasa anajihusisha zaidi na biashara, teknolojia ya akili bandia (AI) katika soka na maendeleo ya mifumo ya uchambuzi wa vipaji.
ASHLEY COLE (Beki wa Kushoto – England)
Cole alihama kwa utata kutoka Arsenal kwenda Chelsea 2006, jambo lililoharibu uhusiano wake na mashabiki wa Arsenal. Hata hivyo, akiwa Chelsea alishinda mataji mengi ikiwemo Ligi ya Mabingwa mwaka 2012. Baada ya kustaafu mwaka 2019, amejenga taaluma ya ukocha katika Chelsea, Everton, Birmingham City na timu ya taifa ya England. Mwaka huu alipata kazi yake ya kwanza kama kocha mkuu wa Cesena nchini Italia.
ROBERT PIRES (Kiungo wa Kulia – Ufaransa)
Pires alimwambia Wenger kwamba angeondoka baada ya fainali 2006 kwa sababu alihisi hakuwa tena sehemu ya mipango ya kocha huyo. Baadaye alichezea Villarreal, Aston Villa na Goa ya India kabla ya kustaafu 2015. Kwa sasa anashiriki shughuli mbalimbali za uchambuzi wa soka na miradi ya Baller League.
GILBERTO SILVA (Kiungo – Brazil)
Baada ya kuondoka Arsenal 2008, Silva alicheza Panathinaikos ya Ugiriki na baadaye kurejea Brazil kumalizia soka. Alistaafu 2015 na tangu wakati huo amekuwa mchambuzi wa soka, balozi wa Fifa na Arsenal.
CESC FABREGAS (Kiungo – Hispania)
Fabregas alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi wa Arsenal baada ya fainali hiyo. Alihamia Barcelona 2011 kabla ya kurejea England kuichezea Chelsea, ambako alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu England, FA na Europa League. Baada ya kumalizia soka Como ya Italia, alistaafu 2023 na kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo. Ameiongoza Como kupanda daraja na kufuzu Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.
ALEXANDER HLEB (Kiungo wa Kushoto – Belarus)
Baada ya kuondoka Arsenal 2008, Hleb alikuwa na safari ndefu ya kuhamahama klabu mbalimbali ikiwemo Barcelona, Birmingham City na Wolfsburg. Alistaafu 2019 na sasa ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka la Belarus.
FREDDIE LJUNGBERG (Mshambuliaji – Sweden)
Ljungberg aliondoka Arsenal 2007 na kuchezea West Ham United, Seattle Sounders, Chicago Fire, Celtic na Shimizu S-Pulse. Alistaafu 2014 na kurejea Arsenal kama kocha 2016. Kwa sasa anajihusisha na miradi midogo ya soka na kazi za uchambuzi wa soka mara kwa mara.
THIERRY HENRY (Nahodha – Ufaransa)
Henry ndiye mchezaji anayekumbukwa zaidi katika historia ya sasa ya Arsenal. Baada ya kuondoka Arsenal alichezea Barcelona na New York Red Bulls, huku akirejea Arsenal kwa mkopo wa muda mfupi. Alistaafu 2014 na kuingia kwenye ukocha akifanya kazi Monaco, CF Montreal na timu za vijana za Ufaransa. Aliiongoza Ufaransa kushinda medali ya fedha katika Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024. Kwa sasa ni mchambuzi mkuu wa soka wa CBS Sports na FOX Sports. Ingawa hakushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa Arsenal alitwaa taji hilo akiwa Barcelona 2009 baada ya kuifunga Manchester United baoa 2-0.
Wachezaji wa Akiba
Manuel Almunia (Hispania), alistaafu 2014 kutokana na tatizo la moyo na amekuwa mbali na maisha ya soka; Philippe Senderos (Uswisi), anafanya kazi Fifa chini ya Arsene Wenger kama msaka vipaji vya vijana; Gaël Clichy (Ufaransa), kwa sasa ni kocha mkuu wa SM Caen nchini Ufaransa na Mathieu Flamini (Ufaransa) huyu amefanikiwa sana katika biashara. Alianzisha kampuni ya kemikali zinazotumika katika nishati endelevu na, kwa mujibu wa Forbes, utajiri wake umefikia Pauni 10 bilioni.
Wengine waliokuwa benchi katika fainali hiyo ni Jose Antonio Reyes (Hispania), alifariki kwa ajali ya gari 2019 akiwa na umri wa miaka 35 na
Robin van Persie (Uholanzi) ambaye baada ya kustaafu soka aliingia kwenye ukocha na kwa sasa ni kocha mkuu wa Feyenoord nchini Uholanzi.