Wanaotaabika EPL wana kipi kujibeba?
Muktasari:
- Msimu wa 2026/27 ulianza ukiwa na makocha 11 ambao waliteuliwa katika nafasi zao wakati fulani ndani ya mwaka 2026, jambo ambalo huenda limechangia utulivu wa mwanzo wa msimu huu.
LONDON, ENGLAND: KWA namna isiyo ya kawaida, klabu zote za Ligi Kuu England bado zina makocha walewale zilizoanza nao msimu huu, lakini huenda haitachukua muda mrefu kabla ya kocha wa kwanza kufutwa kazi. Katika misimu mitatu kati ya 10 iliyopita, mwezi Novemba ulianza bila klabu yoyote kufanya mabadiliko ya kocha.
Msimu wa 2026/27 ulianza ukiwa na makocha 11 ambao waliteuliwa katika nafasi zao wakati fulani ndani ya mwaka 2026, jambo ambalo huenda limechangia utulivu wa mwanzo wa msimu huu.
Ni lazima wapewe nafasi ya kujenga timu zao kulingana na falsafa na mipango yao. Hata hivyo, takribani robo ya msimu tayari imechezwa na ikiwa imesalia raundi moja tu ya michezo kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa, huenda kufutwa kazi kwa kocha wa kwanza kusiwe mbali sana.
Michael Carrick bado ndiye anayepewa nafasi kubwa zaidi ya kuwa kocha wa kwanza kuondoka katika nafasi yake, akifuatiwa na makocha wa klabu zinazoshika nafasi za kushuka daraja; Pierre Sage wa Crystal Palace, Regis Le Bris wa Sunderland na Oliver Glasner wa Nottingham Forest.
Inaonekana karibu kuwa jambo lisiloepukika kwa Carrick kuondoka hivi karibuni, hivyo uchambuzi unaovutia zaidi unahusu makocha wa timu tatu za mwisho kwenye msimamo wa ligi. Sunderland inashika nafasi ya 20 na kwa mujibu wa utabiri wa Opta inatarajiwa kumaliza papo hapo.
Hata hivyo, imekuwa na mwanzo mgumu wa msimu, ambapo kikosi hicho cha Le Bris kimekutana na klabu tano kati ya saba za juu kwenye msimamo wa sasa, idadi ambayo inalingana na Liverpool kuwa timu zilizokutana na wapinzani wengi zaidi wa kundi hilo.
Kocha huyo pia ana akiba kubwa ya heshima na imani kutoka kwa mashabiki baada ya kuirejesha Sunderland kwenye Ligi Kuu England na kisha kuifikisha kwenye mashindano ya Ulaya.
Licha ya ratiba ngumu, kabla ya michezo ya mwishoni mwa wiki Sunderland ilikuwa na upungufu wa pointi moja tu ya matarajio ikilinganishwa na Chelsea, Manchester United na Tottenham.
Hata hivyo, ilifungwa mabao 3-1 na Coventry katika mchezo ambao takwimu za ubora wa nafasi za kufunga mabao (xG) zilionyesha Sunderland ilikuwa na 1.8 dhidi ya 0.7 za wapinzani wake.
Matokeo hayo yanafanana na yale ambayo timu hiyo imekuwa ikiyapata msimu huu, ambapo imefunga mabao 6.2 pungufu ya idadi ya mabao iliyotarajiwa kufunga kulingana na ubora wa nafasi ilizopata.
Kwa kuwa wapinzani watano wanaofuata wa Sunderland katika ligi ni Chelsea, Aston Villa, Tottenham, Liverpool na Newcastle, changamoto ya kubaki Ligi Kuu haitakuwa rahisi hivi karibuni. Angalau matatizo yao ya kushindwa kutumia nafasi wanazopata kufunga mabao siyo makubwa kama yale ya Nottingham Forest.
HAWA VIPI?
Mashuti ya Forest yamekuwa na thamani ya mabao tarajiwa 14.7, idadi ya nne kwa ukubwa katika ligi baada ya michezo ya Jumamosi iliyopita. Hata hivyo, hakuna hata mchezo mmoja msimu huu ambao idadi ya mabao waliyofunga imefikia au kuzidi kiwango cha mabao tarajiwa. Hilo ni tatizo la umaliziaji wa nafasi, siyo suala la makipa wa timu pinzani kufanya maajabu ya kuokoa mipira dhidi yao.
Hatua ya juu zaidi ya uchambuzi kuliko takwimu za kawaida za mabao tarajiwa ni mabao yanayolenga lango. Hii hupima uwezekano wa shuti lililolenga lango kuzaa bao, kwa kuzingatia ubora wa nafasi na mahali mpira ulipoelekezwa. Takwimu za Forest za mabao yaliyolenga lango msimu huu ni 7.4, kiwango ambacho ni zaidi kidogo ya nusu ya mabao tarajiwa 14.7.
Kushindwa kuwalazimisha makipa wa timu pinzani kufanya kazi ngumu ya kutosha ni sawa na kueleza kwa nini kikosi cha Glasner kimefunga mabao sita pekee. Kwa mujibu wa takwimu za mabao tarajiwa, Forest inapoteza wastani wa karibu bao moja kwa kila mchezo kutokana na kushindwa kutumia nafasi zake vizuri.
Hakuna timu yoyote kati ya 96 zinazoshiriki ligi tano kubwa za Ulaya iliyokuwa na kiwango kibaya zaidi ya upungufu wa mabao 0.5 kwa kila mchezo ukilinganisha na mabao tarajiwa msimu uliopita.
Hali hiyo inaashiria kwamba huenda bahati mbaya ya Forest ikabadilika na kuwa nzuri zaidi. Lakini je, mmiliki wa timu, Evangelos Marinakis, ana uvumilivu wa kutosha kusubiri hilo litokee?
Takwimu za mabao tarajiwa za Forest zinaonyesha kiwango kizuri zaidi chini ya kocha Glasner kuliko zilivyokuwa chini ya makocha wengine wanne ambao mmiliki huyo aliwafukuza kazi msimu uliopita. Hata hivyo, kama anazingatia takwimu hizo au la, ni suala jingine.
Glasner alidokeza kwamba kikosi chake kina upungufu wa uwezo wa kimwili baada ya kufungwa na Brentford. “Tunazidiwa kwa mbio na wapinzani katika kila mchezo. Lazima tubadilishe hali hiyo,” alisema kocha huyo.
Takwimu za umbali wa kukimbia zilizokusanywa na FotMob zinaonyesha kwamba hali siyo hivyo kabisa, ingawa Forest ilizidiwa kwa umbali wa kukimbia katika michezo yake mitano iliyopita ya ligi. Hata hivyo, takwimu za msingi za mabao tarajiwa na zile za uwezo wa kimwili ni mbaya zaidi katika klabu ya zamani ya Glasner, Crystal Palace.
Kwa kuwa takwimu za mabao tarajiwa zina mchango mkubwa zaidi katika kutabiri kiwango cha baadaye cha uchezaji au matokeo kuliko takwimu za kukimbia, hizo ndizo zinazopaswa kuleta wasiwasi zaidi.
Vilevile, wastani wa mbio za kasi za Palace ni 96.9 kwa kila mchezo, kiwango cha chini zaidi katika Ligi Kuu England baada ya michezo ya Jumamosi. Klabu hiyo imewahi kukumbana na changamoto zinazofanana na hizo wakati wa mwanzo wa makocha wapya. Makocha wawili walioteuliwa na Palace kati ya misimu ni Frank de Boer na Patrick Vieira.