Prime
Yanga ilivyoipiga bao Simba Ligi Kuu

Muktasari:
- Ukiangalia takwimu za duru la kwanza, kisha ukalinganisha na zile za duru la pili, utabaini Yanga imepiga hatua mbele, huku Simba ikipigwa bao katika suala zima la kukusanya pointi na kufunga mabao.
KUNA mstari mwembamba sana unaozitenganisha Yanga na Simba katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu. Hii inatokana na namna ambavyo timu hizo zilimaliza duru la kwanza na zilivyoanza duru la pili hadi sasa zilipofikia.
Ukiangalia takwimu za duru la kwanza, kisha ukalinganisha na zile za duru la pili, utabaini Yanga imepiga hatua mbele, huku Simba ikipigwa bao katika suala zima la kukusanya pointi na kufunga mabao.
Yanga inayopambania kutetea taji lake la Ligi Kuu Bara, ilimaliza duru la kwanza ikiwa nyuma ya Simba kwa tofauti ya pointi moja, lakini sasa yenyewe ipo kileleni kwa tofauti hiyohiyo ya pointi moja.
Simba inayosaka taji la Ligi Kuu Bara ililolikosa kwa misimu mitatu mfululizo, ilipambana duru la kwanza na kumaliza kileleni ikikusanya pointi 40 katika mechi 15 baada ya kushinda 13, sare moja na kupoteza moja.

Wakati Simba ikimaliza kileleni, Yanga ilikuwa na pointi 39 baada ya mechi 15, ikishinda 13 sawa na Simba, lakini ikapokea vichapo viwili huku ikiwa haina sare. Kupoteza mechi mbili kwa Yanga ndiyo ilichangia wao kuzidiwa na Simba.
Kitendo cha Yanga kupoteza mechi mbili mfululizo za duru la kwanza baada ya kushuka dimbani mara 10, fasta ikaachana na Kocha Miguel Gamondi, kijiti chake kikachukuliwa na Sead Ramovic ambaye aliiongoza timu hiyo katika mechi sita za ligi na kushinda zote kabla ya kusepa akimwacha Abdihamid Moulin kusimamia mechi moja dhidi ya KenGold na kushinda kwa mabao 6-1, ndipo akaja Miloud Hamdi.
Hadi sasa katika mechi tano za ligi ambazo Hamdi ameiongoza Yanga, ameshinda nne na sare moja dhidi ya JKT Tanzania ambayo ilikuwa ya kwanza kwake kukaa benchi baada ya ile ya kwanza kuwa jukwaani akiishuhudia timu hiyo ikiichapa KenGold.
Kwa takwimu za duru la pili kulinganisha na zile za duru la kwanza, Yanga imeonekana kufanya vizuri zaidi baada ya kukusanya pointi nyingi (19) zaidi ya Simba (17) huku zote zikishuka dimbani mara saba. Katika kuzisaka pointi 21 kwenye mechi saba, Yanga imepoteza mbili na Simba ikipoteza nne.

Wakati Yanga ikifanya mabadiliko ya benchi lake la ufundi kwa timu hiyo kunolewa na makocha watatu, Simba imeendelea kubaki na Fadlu Davids ambaye alianza msimu na kikosi hicho.
Hata hivyo, licha ya Simba kupoteza mechi moja ya ligi na kutoka sare tatu msimu huu, bado wenyewe wanasisitiza wanajenga timu kwa ajili ya baadaye ingawa moto wanaouwasha umekuwa tishio kwa wapinzani.
Mabadiliko ya Yanga yameifikisha hapo ilipo sasa kwani mbali na kukusanya pointi nyingi, pia imekuwa imara katika kufunga mabao kulinganisha na Simba.
Katika duru la kwanza, Yanga ilipocheza mechi 15, ilifunga mabao 32 ikiwa ni wastani wa kufunga mabao 2.1 kwa mechi.
Katika duru la pili, Yanga ikiwa imecheza mechi saba, imefunga mabao 26, wastani wa mabao ni 3.7 kwa mechi, ukiongezeka kwa 1.6 kutoka duru la kwanza.

Kwa upande wa Simba, duru la kwanza ilifunga mabao 31 ikiwa ni wastani wa mabao 2.0 kwa mechi.
Duru la pili, Simba imecheza mechi saba na kufunga mabao 21 huku wastani ukiwa ni mabao matatu kwa mechi ikionyesha hakuna mabadiliko yoyote.
KINACHOWEZA KUTOKEA
Yanga na Simba kila moja imebakiwa na mechi nane ikiwemo moja itakayowakutanisha baada ya kuahirishwa Machi 8, mwaka huu. Mchezo huo unaweza kuleta taswira nyingine katika mbio za ubingwa kwani Yanga ikishinda, itaiacha Simba kwa pointi nne, lakini ikiwa tofauti, Simba itakaa juu kwa tofauti ya pointi mbili. Sare itaendelea kuwafanya kukimbizana kwa tofauti ya pointi moja.
Katika mechi nane zilizobaki, Yanga italazimika kucheza nne ugenini dhidi ya Tabora United, Azam, Fountain Gate na Tanzania Prisons, huku zingine nne nyumbani dhidi ya Simba, Coastal Union, Namungo na Dodoma Jiji. Kati ya zile za ugenini, moja pekee dhidi ya Azam haitasafiri kwenda nje ya Dar es Salaam, zilizobaki italazimika kusafiri.
Katika duru la kwanza, Yanga ilipocheza dhidi ya timu hizo, ilikusanya pointi 18 kati ya 24 kutokana na kushinda sita na kupoteza mbili huku matokeo yakiwa hivi; Simba 0-1 Yanga, Coastal Union 0-1 Yanga, Yanga 0-1 Azam, Yanga 1-3 Tabora United, Namungo FC 0-2 Yanga, Yanga 4-0 Tanzania Prisons, Dodoma Jiji 0-4 Yanga na Yanga 5-0 Fountain Gate.

Simba kwenye mechi nane zilizobaki, nne nyumbani na nne ugenini huku hizo mechi nane moja pekee dhidi ya KenGold ndiyo itasafiri kwenda nje ya Dar kucheza, zilizobaki zote itacheza Dar es Salaam.
Mechi zilizobaki za Simba ni dhidi ya Yanga, Mashujaa, JKT Tanzania, Pamba Jiji, KMC, Singida Black Stars, KenGold na Kagera Sugar.
Katika duru la kwanza dhidi ya timu hizo, Simba ilikusanya pointi 21 kati ya 24 baada ya kushinda saba na kupoteza moja matokeo yakiwa hivi; Simba 0-1 Yanga, Mashujaa 0-1 Simba, Simba 4-0 KMC, Pamba Jiji 0-1 Simba, Simba 2-0 KenGold, Kagera Sugar 2-5 Simba, Simba 1-0 JKT Tanzania na Singida BS 0-1 Simba
MATOKEO SIMBA DURU LA KWANZA
Simba 3-0 Tabora United
Simba 4-0 Fountain Gate
Azam FC 0-2 Simba
Dodoma Jiji 0-1 Simba
Simba 2-2 Coastal Union
Simba 0-1 Yanga
TZ Prisons 0-1 Simba
Simba 3-0 Namungo
Mashujaa FC 0-1 Simba
Simba 4-0 KMC
Pamba Jiji 0-1 Simba
Simba 2-0 KenGold
Kagera Sugar 2-5 Simba
Simba 1-0 JKT Tanzania
Singida BS 0-1 Simba

MATOKEO YANGA DURU LA KWANZA
Kagera Sugar 0-2 Yanga
KenGold 0-1 Yanga
Yanga 1-0 KMC
Yanga 4-0 Pamba Jiji
Simba 0-1 Yanga
Yanga 2-0 JKT Tanzania
Coastal Union 0-1 Yanga
Singida BS 0-1 Yanga
Yanga 0-1 Azam
Yanga 1-3 Tabora United
Namungo FC 0-2 Yanga
Yanga 3-2 Mashujaa
Yanga 4-0 TZ Prisons
Dodoma Jiji 0-4 Yanga
Yanga 5-0 Fountain Gate
MSIMAMO DURU LA KWANZA
P W D L F A PTS
1. Simba 15 13 1 1 31 5 40
2. Yanga 15 13 0 2 32 6 39

MATOKEO SIMBA DURU LA PILI
Tabora United 0-3 Simba
Fountain Gate 1-1 Simba
Simba 3-0 TZ Prisons
Namungo FC 0-3 Simba
Simba 2-2 Azam FC
Coastal Union 0-3 Simba
Simba 6-0 Dodoma Jiji
MATOKEO YANGA DURU LA PILI
Yanga 4-0 Kagera Sugar
Yanga 6-1 KenGold
JKT TZ 0-0 Yanga
KMC FC 1-6 Yanga
Yanga 2-1 Singida BS
Mashujaa FC 0-5 Yanga
Pamba FC 0-3 Yanga
MSIMAMO DURU LA PILI
P W D L F A PTS
1. Yanga 7 6 1 0 26 3 19
2. Simba 7 5 2 0 21 3 17
MECHI ZILIZOBAKI SIMBA
Yanga v Simba
Simba v Mashujaa
JKT TZ v Simba
Simba v Pamba Jiji
KMC FC v Simba
Simba v Singida BS
KenGold v Simba
Simba v Kagera Sugar
MECHI ZILIZOBAKI YANGA
Yanga v Simba
Tabora United v Yanga
Yanga v Coastal Union
Azam v Yanga
Fountain Gate v Yanga
Yanga v Namungo
TZ Prisons v Yanga
Yanga v Dodoma Jiji