Zaka Zakazi kisa Dube amfutia jina mwanawe -1

Muktasari:
- Kijana mmoja mjuzi wa taarifa za kumbukumbu za zamani mwenye ujuzi wa ubishani ambaye akiamua kubishana na wewe uwe umejipanga kwani sio rahisi kukubali matokeo, aliyetua Azam kuchukua nafasi ya mkongwe Jaffar Idd, muda ambao Zaka amedumu ndani ya Azam, Mwanaspoti limefanya naye mahojiano na akazungumzia mambo mbalimbali ndani na nje ya kazi yake ikiwamo kumpa jina la Prince Dube, mshambuliaji wa sasa wa Yanga kipindi kile akikipiga Azam FC, lakini akalifuta baada ya staa huyo kutimkia Yanga.
KWENYE soka la Tanzania kwa sasa ukitajiwa jina la Zaka Zakazi akili yako itahamia sehemu mbili tu. Utajiuliza labda anakusudiwa hayati Zacharia Hans Poppe aliyekuwa kiongozi wa Simba ukiambiwa hapana basi akili yako itatua kwa ofisa habari na msemaji mkuu wa Azam FC, Thabit Zakaria maarufu kwa jina la Zaka za Kazi.
Kijana mmoja mjuzi wa taarifa za kumbukumbu za zamani mwenye ujuzi wa ubishani ambaye akiamua kubishana na wewe uwe umejipanga kwani sio rahisi kukubali matokeo, aliyetua Azam kuchukua nafasi ya mkongwe Jaffar Idd, muda ambao Zaka amedumu ndani ya Azam, Mwanaspoti limefanya naye mahojiano na akazungumzia mambo mbalimbali ndani na nje ya kazi yake ikiwamo kumpa jina la Prince Dube, mshambuliaji wa sasa wa Yanga kipindi kile akikipiga Azam FC, lakini akalifuta baada ya staa huyo kutimkia Yanga.
AFUTA JINA LA MWANAWE PRINCE
Akizungumzia jina la Prince alilompa mwanawe baada ya Dube kuifunga Yanga mwaka 2021 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambalo lilimfanya Zaka afurahi, anasema: "Nilimuita mwanangu jina la Dube kwa sababu tulicheza mechi na Yanga 2021 halafu akafunga bao karibu na katikati ya uwanja ndio maana nikasema kwa heshima nimuite mwanangu jina hilo.

"Kwa sasa nimebadilisha jina kwa sababu sifurahi kumuita mtoto wangu hilo jina tangu (Dube) alipoondoka Azam, lakini kwa sasa sitamuita mwanangu jina la aina yoyote."
Zaka anasema yeye ni mmoja kati ya wanaume ambao kila mwanamke angetamani kuwa naye maishani licha ya kwamba hajakamilika kama binadamu wengi wengineo walivyo.
"Mimi ni baba ambaye kila mke angependa niwe baba wa mtoto wake. Unafikiri mwanamke anapenda nini kwa mzazi mwenzake.. ila mimi sio mkamilifu sana. Ila napenda familia hata mwanangu wa kike atamani kuwa na mwanaume mwenye sifa kama za baba yake," anasema na kuongeza:
"Mwanaume unatakiwa ujipime na ujiangalie katika mazingira kama haya mtoto wako atatamani kuwa na mwenza kama wewe.
Mimi nimejipima naona kabisa ili niwe baba bora nyumbani ni lazima kuwe na vitu vingi sana niwe nimevifuata licha ya upungufu wangu.
CHANGAMOTO KAZINI
Kutoka kuwa mwandishi wa habari anayechakata maudhui katika chumba cha habari hadi kuwa ofisa habari wa klabu, Thabit Chumwi Zakaria anataja changamoto ambazo aliwahi kuzipitia baada tu ya kupewa majukumu hayo.

"Kutoka kuwa mtafuta habari mpaka kuwa chanzo cha habari hiyo ilikuwa changamoto sana. Nilizoea kuhoji watu halafu mimi ndio nakuja kuhojiwa... halafu mimi nilikuwa nimezoea kuelezea mambo kwa kina sana (kupitia habari alizoandika). Kwa hiyo kuja kuhojiwa na mwandishi naanza kuchambua tena na sio kutoa habari.
"Kuna muda unatamani kuulizwa aina fulani ya swali kwa sababu naona kabisa stori iko hapa mpaka mahojiano yanakwisha inabidi nidakie tu mwenyewe. Ukishakuwa katika nafasi kama hii kuna mambo ya ndani huwezi kuyatoa kuna mipaka mingi. Kwa hiyo wakati mwingine unajisahau mpaka unafungiwa (mamlaka za soka)."
Mwaka 2022 Zaka alifungiwa miezi mitatu na kupigwa faini ya Sh500,000 na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kile kilichodaiwa na mamlaka za soka kuwa ni kumtuhumu mwamuzi kuinyima Azam FC penalti mbili kwenye mechi dhidi ya Tanzania Prisons iliyomalizika kwa kufungwa bao 1-0.
Zaka anaeleza ilivyotokea: "Ilikuwa mbaya kiukweli. iliniumiza sana kwa sababu nilifungiwa wakati tunakwenda kucheza mechi ya kimataifa Libya halafu tulianzia ugenini tukafungwa mabao matatu. Hivyo marudiano ilibidi tuwe na tamasha la Azamka ili kuamsha ari za mashabiki. Kwa hiyo halikufanikiwa kwa sababu mimi nilikuwa niko kwenye kifungo.
"Tulikuwa tumetoka kucheza mechi na Tanzania Prisons tulipoteza ugenini, nikaona mwamuzi hakutenda haki. Kwa hiyo nikakata matukio yote kwenye mchezo ule na kuanza kuyaweka mitandaoni.
"Nikawa mkali sana. Nikakosea kweli, maana nilimuandama mwamuzi. Baadaye kichwa kilivyokuja kutulia ndio nikagundua kwamba sikutenda sawa wala Bodi ya Ligi haikukosea (kumfungia) kwa sababu walinionya sana kabla ya hilo. Mpaka siku hukumu inatoka nimeshapoa tayari."

AZAM KITAMBO
Zaka anasema kuwa haikuwa bahati mbaya kwake kufanya kazi na Azam FC licha ya kuwa mwandishi wa habari, kwani alikuwa mdau wa klabu hiyo tangu kitambo.
"Nilikuwa na mapenzi na Azam, sikuja kwa bahati mbaya. Ila wao wenyewe waliona ninavyoikubali hii timu tangu zamani nimeanza kufanya nao kazi nyuma ya pazia katika maeneo mengi. Toka uwanja haujajengwa," anasema msemaji huyo.
"Tangu 2010 unaangushwa mti mkubwa hapa (Azam Complex) kwa ajili ya ujenzi. Kwa hiyo nilikuwa mwandishi lakini nilikuwa nafanya nao kazi kwa karibu sana."
Zaka anazungumzia maisha ndani ya Azam FC yalivyo akisema kuwa wengi wanadhani ni klabu tajiri, lakini kinachofanyika ni kutimiza wajibu kwa wachezaji wa timu hiyo.
"Kwanza kuna hizo kauli kwamba Azam ni timu tajiri, ila ni kwa sababu ni klabu ya bosi. Unajua hawawezi kutofautisha mtoto wa bosi, saa nyingine wanamuona kuwa naye ni sawa na baba yake," anasema.
"Mfano hata mbwa wa bosi ni bosi wa mbwa wengine. Kwa hiyo siyo kitu kibaya hata klabu yenyewe inafanana kuitwa hivyo. Hii inamilikiwa na familia ya Bakhresa hawanaga makuu wala kupenda kufahamika... mmiliki mwenyewe tu siyo mtu wa kuonekana sana, labda sasa kwa sababu ya mitandao ya kijamii.
"Hata Azam ni klabu ya hivyo, inajali sana weledi, inataka kubadilisha kitu kwenye mpira wa Tanzania. Hata mipango ya klabu ni kuendeleza vipaji chipukizi. Sisi (Azam FC) ndio tulianza na akademi hizi za vijana, unajua watu hawaelewi hata hii ligi ya U20 ni wazo la Azam FC. Hicho kitu hakijazungumzwa vya kutosha.

"Ilikuwa hivi, Azam kabla ya kuanzisha akademi ilikuwa ni timu ambayo ina vijana wengi ndio ikaona ili waweze kujiendeleza ikapeleka wazo TFF ianzishwe ligi hiyo, ili wapate sehemu ya kucheza."
USHINDANI KATIKA LIGI
Zaka anazungumzia jinsi timu hiyo inavyopambana katika Ligi Kuu Bara ili kuendelea kufanya vizuri, akisema ubora ilionao ni wa kipekee, lakini hukutana na wenzao walio bora zaidi na hapa ni kama anazizungumzia Simba na Yanga.
“Siyo kama tunapanga tuwe wa tatu (kwenye msimamo wa ligi) inatokea kwenye msimu sababu ya ubora wa wenzetu. Unafahamu kuna kitu watu hawakiangalii kwa mapana ya kutosha acha tukifanyie kazi tutakuja kuwa na majibu ya kutosha baadaye kwa sababu tupo kwenye ligi ambayo tunashindana na watu bora sana," anasema.
"Hicho kitu watu wakiangalie sisi tunahangaika kufananisha ubora wao. Wanaotubeza na wasiolewa watashindwa, lakini ni kwamba tunaoshindana nao ni bora na ukitaka kuona hilo wao wangalie wanapotoka kwenye mashindano ya kimataifa.
"Kitu cha kwanza ili uweze kushindana vizuri utambue nguvu ya mpinzani wako usijidanganye tofauti na hapo, na sisi tunatambua kuwa wenzetu ni bora sana. Kwa hiyo acha tulinganishe ubora wao kwanza halafu ndio tuanze kushindana nao kisawasawa.
"Kwa hiyo kila siku tunakaza nati flani na tunarekebisha maeneo kadhaa...tutakuja kufika sehemu ambayo tutakuwa tuko nao sawa kiushindani, lakini kwa sasa wametuzidi mizungu flani na hicho ndicho kila kitu kwenye mpira tofauti na watu wanavyotuona sisi tuna kila kitu, hapana.
"Wenzetu wana kila kitu kwenye mpira tutakuja kuwa sawasawa nao tu huko mbele, lakini kwa sasa tuzidi kujipa muda."

TOFAUTI IPO HAPA
Bosi huyo wa kitengo cha habari na mawasiliano cha Azam FC anazitaja tofauti zinazowafanya watofautiane na timu hizo kubwa nchini akisema, "kwanza jina, kila timu ina lake tofauti ya kwanza iko hapo. Nadhani malengo pia tofauti, sijui wenzetu misheni zao zikoje, lakini ukija kuangalia kwenye hali halisi kwenye kupima kwetu sisi tunataka kukuza vipaji vya vijana.
"Ukiwangalia wengine hawana sana hiyo kitu. Asilimia kubwa nadhani hiyo ndio tofauti, lakini nyingine kubwa nayoiona ni namna tunavyopambana kwenye ligi. Unafahamu hakuna timu katika historia ya mpira wa Tanzania ambayo ilikuja ikajitahidi kupambana na Yanga, Simba kama Azam FC kwa sababu wao wenzetu ndio wanaishi kwenye huu mpira.
"Wamekaa muda mrefu sana kwenye mpira huu wa Bongo, ligi zote ambazo unaziona wao wameshiriki kuzianzisha na kutengeneza mfumo. Mfano huu ni mfereji wa maji waliuchepusha kutoka mtoni kuelekea nyumbani kwao. Kwa hiyo wao wanapata maji kutokea sebuleni tu wanachota.
"Kwa hiyo kupambana nao hawa inataka muda, uwekezaji mkubwa na maarifa mengi, itafikia wakati utaweza, lakini siyo rahisi hivyo na ndio maana timu zote zilizokuja kuwahi kushindana zikapotea hii ligi."
Anasema: "Hii ligi tunayocheza saa hizi ilianza 1965, kuna mtu aliwahi kushindana na Cosmopolitan hayupo sasa hivi timu ipo ila haipo katika ushindani tena... inahangaika katika madaraja ya chini...ilishashidwa muda mrefu sana na ilichukua ubingwa mara moja tu 1967, wakapotea kuanzia 1970 hawachezi Ligi Kuu hadi Leo.
"Mwaka 1975 (ubingwa) walichukua Mseto sasa haipo tena, wakaja Pan African 1982 hawapo sijui wapo daraja la ngapi... nadhani wapo Championship, nadhani kubaki na ubara wao ni kwa kununua jina la timu nyingine. Wananunua leseni wanahangaika, lakini Pan kachukua ubingwa 1982, 1983, 1984 sijui baada ya hapo wakapotea hakukaa hata miaka mitano kudumu katika kupambana.
"Walikuja Mtibwa wakachukua ubingwa, lakini niambie mara ya mwisho kumaliza nafasi tano za juu lini. Sasa hivi
kashuka daraja (daraja), hivyo ni ngumu kwetu... tunaangalia na kujiona kwamba - fikiria tumecheza ligi (kuu) huu
msimu wa 16 huku mitatu tu ndio hatujakaa katika nafasi tatu za juu.
"Msimu wa kwanza wa ligi tulimaliza nafasi ya nane, wa pili tulimaliza ya tano, msimu wa 2016/17 tulimaliza nafasi ya nne misimu hiyo tu ndio ambayo hatujakaa kwenye nafasi za juu. Tunaenda kidogo kidogo na muda siyo rahisi hivyo kama ambavyo watu wangeweza kudhania.
"Unakuja kuona hiyo ukiwa kwenye hiyo hali yenyewe... ukianza kuyaogelea haya maji ndiyo utaona, ukiwa nje utasema rahisi ila ukiwa ndani na ukaona mkondo wa maji unavyovutwa hapa katikati ndiyo utagundua kwamba sio rahisi hivyo."
MAANA YA NENO AZAM
Ukubwa wa klabu hiyo uko katika maeneo mengi na siyo uwanjani tu, kwani jina lenyewe ukilitaja kila mtu lazima ashtuke na hapa Zaka anazungumzia maana yake, "unajua neno lenyewe Azam ni kubwa. Tunajitahidi sana kwenda na jina tunapambana sana kuwekeza kwenye kikosi chetu na kuiandalia timu mazingira mazuri ya kambi, ya safari na kila kitu (kuhusu) maisha ya wachezaji.
"Tunajitahidi sana kuwekeza tukiamini kwamba haya mengine yote yakiwa sawa... kinachobakia ni kupambania medali na ndio tunachokifanya sasa kuboresha matokeo yetu uwanjani. Hata kwenye ligi ukiangalia msimamo wa misimu minne iliyopita ukiwemo huu hasa kuanzia imekuwa na timu 16 tulikwenda hadi timu 20 hivi karibuni nadhani kuanzia 2017/18 ilikuwa, zikashuka hadi timu 18 mpaka 16 zilianza 2021/22.
"Tangu msimu huo hadi sasa tumekuwa tukiboresha matokeo yetu uwanjani. Tulimaliza msimu huo wa kwanza wa 2021/22 tukiwa na alama 49 zilikuwa chache sana ukilinganisha na bingwa kwa sababu alikuwa yupo juu akiwa na alama 75, tofauti kubwa, tukasema hatuwezi kupiga hatua kuchukua ubingwa kama tunatengeneza pengo kubwa namna hii na katika hali ya kawaida huwezi kushinda mkipishana kwa tofauti ya alama zinakaribia 30.
"Msimu uliofuata 2022/23 tulimaliza na alama 59 tukasema tunakwenda sawasawa, msimu uliofuata ambao ni 2023/24 tulimaliza na alama 69 alama 10 juu ulikua mwenendo mzuri sana."
Una maoni gani kuhusu mwenendo wa Azam FC? Tupe kupitia namba: 0658-376417
ITAENDELEA KESHO