Dodoma FC, Ihefu FC , Majimaji FC kila mtu ashinde mechi zake

Muktasari:
Hata hivyo, Mwanaspoti linaweka bayana michezo ambayo itakuwa ya kutolea macho kwa baadhi ya timu hizo ambazo alama tatu zitazinufaisha lakini ndio michezo inayoweza kuharibu malengo.
VITA inaendelea huko. Michezo mitano imesalia kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kufikia tamati, huku vikumbo vikiendelea kwa timu kusaka nafasi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
Katika michezo hiyo kazi kubwa ipo Kundi A ambalo timu nne zina nafasi ya kucheza Ligi Kuu na vita za hapa na pale zimeanza kuelekea michezo ya lala salama.
Kundi B, Gwambina FC kama vile amejihakikishia kutinga Ligi Kuu msimu ujao kutokana na pengo la alama 10 ililoliweka baina yake na timu zinazoifuata.
Hata hivyo, Mwanaspoti linaweka bayana michezo ambayo itakuwa ya kutolea macho kwa baadhi ya timu hizo ambazo alama tatu zitazinufaisha lakini ndio michezo inayoweza kuharibu malengo.
DODOMA v NJOMBE MJI
Kipute hiki kitapigwa wiki hii katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ambacho kitakuwa na kazi ya ziada kwa timu zote mbili kwa maana bado zina nafasi, Njombe Mji ipo nafasi ya tano ikiwa na alama 26 huku Dodoma ikiwa kileleni na alama 36 sawa na Ihefu FC.
Sare ya aina yoyote itaharibu mipango ya timu hizo kwa maana Dodoma itaongeza presha kama Ihefu itashinda hivyo kuifanya kuacha kwa alama mbili jambo ambalo litaipa mwanya Mbeya Kwanza na Majimaji kumkuta.
IHEFU FC v BOMA FC
Hii ni dabi ya Mbeya ambayo itapigwa wiki hii katika Uwanja wa Sokoine, baada ya kuishuhudia dabi ya wiki iliyopita Mbeya Kwanza ilikukubali kichapo cha bao 1-0 mbele ya Ihefu katika Dimba la Highland Estates.
Ihefu inahitaji alama tatu ili kupata nafasi ya kucheza hatua ya mtoano au kumtoa Dodoma kileleni huku Boma FC ikikwepa rungu la kushuka daraja hasa kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Bodi ya Ligi (TPLB).
MAJIMAJI v DODOMA FC
Mchezo huu unapigwa kwenye Uwanja wa Majimaji FC, Aprili 11 kama ratiba haitabadilika ukiwa wa 20 kwa timu hizo ambazo zina nafasi ya kwenda Ligi Kuu. Dodoma ipo chini ya Mbwana Makata ambaye msimu uliopita aliipandisha Polisi Tanzania na ndiye kocha aliyeipandisha Alliance FC 2018/19 na sasa anasaka rekodi ya kuzipandisha timu tatu mfululizo na Majimaji FC iko chini ya beki wake wa zamani, Peter Mhina.
DODOMA v MBEYA KWANZA
Vijana hao kutoka makao makuu ya nchi wanaonekana kuwa na ratiba ngumu kufikia malengo, kwani mzunguko wa 21 itapambana na Mbeya Kwanza ambayo hadi sasa zimeachana alama mbili, hivyo lolote linaweza kutokea.
Mbeya Kwanza msimu wake wa pili sasa inasaka nafasi ya kucheza Ligi Kuu katika dirisha dogo la usajili liliwachukua wakongwe, Danny Mrwanda, Uhuru Selemana na David Naftali kuongeza nguvu na ndio timu yenye washambuliaji hatari katika kufumania nyavu ikiwa imeweka kambani mabao 29.
NJOMBE v MBEYA KWANZA
Baada ya kushuka Ligi Kuu msimu wa 2017/18 sasa inahitaji kurudi kwenye Ligi hiyo kwa kurejesha matumani na heshima kwa watu wa Mkoa wa Njombe baada ya kukosa kwa msimu miwili.
Timu hizo zimetofautiana alama tano huku kazi ikiwa kusaka nafasi ya kucheza hatua ya mtoano kama ataendelea kupata matokeo mazuri kwenye michezo yake ya hivi karibuni.
TRANSIT v PAMBA FC
Timu hizo zimelingana alama na zipo kwenye hali ambayo inaziweka kwenye presha kubwa ya kushuka daraja, lakini pia kama zikifanya vyema zitapata nafasi ya kucheza hatua ya mtoano.
Hadi sasa zina alama 22 katika michezo 17 ilizocheza, lakini hali ya msimamo wa kundi lao linaziweka katika hali ngumu ya kuendelea kupambana na kuondoka katika nafasi walizokuwa nazo sasa.
MASHUJAA v ARUSHA FC
Kipute hicho kitapigwa Lake Tanganyika, Arusha FC imekusanya alama 25 ikiwa nyuma kwa alama mbili za alizokusanya Arusha FC inayokamata nafasi ya tatu.
Katika mzunguko wa kwanza timu hizo zilipokutana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, mwenyeji aliibuka na ushindi wa mabao 2-1 ya James Mwashinga pamoja na Gasper Mwaipasi huku bao la kufutia machozi kwa Mashujaa FC likifungwa na Ben Rahael.
GWAMBINA KUSHINEYI
Hadi sasa tunaweza kusema Gwambina imemaliza kazi yake na kilichobaki katika michezo mitano ilioyosalia ni kuzisaka alama sita na kujihakikishia kucheza Ligi Kuu.
Kwa maana nyingine Gwambina anaziachia msala timu zilizosalia nafasi ya pili hadi ile saba kuwania nafasi ya kucheza hatua ya mtoano kwa kuwa kila mmoja anaweza kupata nafasi ya kucheza hatua ya mtoano.
Gwambina imekusanya alama 37 na kuiacha Geita nafasi ya pili kwa alama 10 ambazo sio rahisi kukutwa hasa kwa kuangalia mwenendo wa timu zote mbili katika michezo ya karibuni.
WASIKIE MAKOCHA
Kocha wa Gwambina Fulgence Novatus ameeleza bado watapambana kwenye michezo iliyosalia kwa maana kwenye soka lolote linaweza kutokea na sasa wanaona bado kazi ndio inaanza.
Kocha wa Ihefu FC, Maka Malwisi alisema watahakikisha wanapambana na kuvuna alama tatu katika michezo iliyobaki na kumuombea adui wao ateleze kwenye michezo yake.
“Kila mchezo kwetu ni vita, wachezaji na viongozi wanalitambua hilo, hivyo kila mchezaji anajua kitu anachotakiwa kukifanya kwaajili ya timu yake na maisha yake kupitia soka kazi ambayo aliichagua,” alisema Malwisi.
Kocha Peter Mhina wa Majimaji FC alisema wanahitaji kurejesha heshima katika Mkoa wa Ruvuma kwa wapenzi wa soka ambao kwa misimu miwili wamekosa kusuhudia Ligi Kuu nyumbani.
‘Tunayo nafasi ya kupanda Ligi Kuu na uwezo tunao wa kuhakikisha kila mchezo tunapata alama tatu ambazo ndio silaha pekee ya kutufanya kuwa na matumaini ya kurejea Ligi Kuu,” alisema Mhina.
HOFU YATANDA
Kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Bodi ya Ligi (TPLB) ya kupunguza timu TPL, FDL na SDL Msimu wa (2020/21) FDL zitashiriki timu 20 ikiwa timu 12 zilizobaki FDL (6 kila kundi).
Msimu huu (2019/20) zitashuka timu nane moja kwa moja ikiwa timu nne kila kundi timu ambazo zimeshika nafasi ya 9, 10, 11 na 12 kwenye kundi itashuka moja kwa moja kwenda Ligi Daraja la Pili (SDL) huku aliyeshika nafasi ya 7/8 atacheza ‘play off’ na timu za SDL.
-Timu itakayoshika nafasi ya kwanza kwenye kundi itapanda Ligi Kuu moja kwa moja huku timu ambayo imeshika nafasi ya 2/3 kwenye Kundi A itacheza ‘play off’ na timu iliyoshika nafasi ya 3/2 kwenye Kundi B.
Mshindi wa jumla hapo atacheza ‘play Off’ ya kupanda Ligi Kuu au kubaki Ligi Daraja la Kwanza na timu zilizoshika nafasi ya 15/16 kwenye Ligi Kuu.
Timu zilizoshika nafasi ya 7/8 kwenye Kundi A zitacheza play off na timu zilizoshika nafasi ya 8/7 kwenye Kundi B na aliyefungwa atacheza ‘play off’ ya kubaki FDL au kushuka SDL na timu ambazo zimefika hatua ya nusu fainali ya sita bora ya SDL.
Timu nne ambazo zimeshuka daraja kutoka VPL, timu mbili ambazo zimepanda daraja kutoka SDL na timu mbili ambazo zitashinda michezo ya ‘play Off’ kwa timu zilizoshika nafasi ya 7 na 8 na zile mbili kutoka SDL.