Kwa Lwanga mtaomba po!

KIUNGO mpya wa Simba, Taddeo Lwanga amefanya mazoezi na kikosi hicho kwa muda wa siku mbili; Jumatatu na Jumanne na kila awamu moja walikuwa wanatumia sio chini ya saa 1:30 katika Uwanja wa Mo Simba Arena, huku jamaa akionyesha kweli ni ‘mtu’.

Mwanaspoti liliweka kambi maalumu kwa siku zote ambazo Lwanga alifanya mazoezi na kikosi hicho kwa zaidi ya saa tatu na kubaini mambo manane ambayo aliyaonyesha mbele ya kocha Sven Vandenbroeck pamoja na mashabiki waliofuatilia mazoezi hayo.
Jambo la kwanza ambalo Lwanga alilionyesha ni mtaalamu wa kupiga pasi fupifupi - zile ambazo unagusa na kuachia na alikuwa akifanya hivyo mara kwa mara akiwa na Francis Kahata, Hassan Dilunga na Ibrahim Ajibu. Pia anapiga pasi ndefu kama zile ambazo amekuwa akipiga kiungo mwenzake, Said Ndemla.
Lwanga anayeonekana mwili wake kujengeka kimazoezi kutokana na misuli ambayo imejitokeza katika miguu yake, umbo kubwa kama la Chriss Mugalu ambalo alikuwa akitumia nguvu kwenda kupora mipira kwa wachezaji wenzake.
Eneo lingine ambalo ameonyesha katika mazoezi hayo ya siku mbili licha ya kucheza katika sehemu ya kiungo mkabaji, lakini anaweza kukimbia kwa mwendo kasi kwenda kupora mipira au kumkabia mchezaji mwenzake ambaye atakuwa amepanda mbele kushambulia na eneo lake kubaki wazi.
Ubora mwingine ambao Lwanga aliouonyesha ni mzuri katika kugombania mipira ile ambayo wanakutana wachezaji wawili wa timu tofauti na muda wote kutumia nguvu kufanikiwa kuchukua kama ambavyo alifanya katika mazoezi ya siku ya kwanza dhidi ya Ajibu, Kahata, Mugalu na Charles Ilanfya.
Lwanga na Morrison katika siku zote mbili za mazoezi walikuwa kivutio kwani muda wote walipokuwa wanakutana kwenye kugombania mipira au mmoja kumkaba mwenzake kunakuwa na ushindani wa kweli kana kwamba kuna ugomvi kati yao, na kuna wakati mpaka walionekana kana kwamba wanachezeana rafu.
Katika ushindani huo kuna muda Lwanga alifanikiwa kumzuia Morrison, lakini wakati mwingine alionekana kuzidiwa na winga huyo mwenye uwezo wa kuchezea mpira unapokuwa miguuni kwake.
Jambo lingine ambalo Lwanga ameonyesha kuwa mzuri sio kutumia nguvu tu, bali akili za mpira anazo sana, kwani katika mazoezi ya siku ya pili kuna wakati alizungukwa na viungo wa ‘timu pinzani’ katika mazoezi yao - Jonas Mkude na Mzamiru Yassin, lakini aliweza kupiga pasi iliyofika kwa mlengwa.
Lwanga katika mazoezi hayo ya siku mbili alionyesha udhaifu wa aina mbili, kwani si mzuri sana kwenye kupiga pasi za mwisho. Katika mazoezi ya siku ya kwanza alipoteza mbili ambazo alikuwa akimpigia Meddie Kagere na Ibrahim Ame, jambo lingine
sio mzuri kupi-
ga ma-shu
ti mara kwa mara kwani katika mazoezi ya siku ya pili alipiga mawili moja lilizuiliwa na Joash Onyango na lingine lilidakwa na kipa Ali Salim.
Lwanga aliliambia Mwanaspoti lilifichua kuhitajiwa kwake na hata aliposaini mkataba wa miaka miwili kuwa kabla ya kuja hapa nchini kuanza kazi katika kikosi hicho alikuwa akiifutialia timu hiyo vya kutosha na kubaini kuwa kuna wachezaji bora katika kila nafasi.
Alisema ukiangalia kikosi cha Simba sio nafasi ya kiungo mkabaji ambayo anacheza kuna wachezaji bora, bali katika maeneo yote kila mchezaji ana uwezo wa kufanya kazi iliyo bora kulingana na majukumu ya eneo husika.
“Nimeona Simba kuna viungo wengi wazuri na mpaka unapata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza au kuingia kuna kazi kubwa ambayo mchezaji unatakiwa kuifanya katika mazoezi ili kupewa mechi ambayo nayo unatakiwa kutimiza majukumu yako kwa hali ya juu.”
NA THOBIAS SEBASTIAN NA RAMADHAN ELIAS