Amunike amshangaa Farid kurudi Bongo

ALIYEKUWA kocha wa timu ya Taifa la Tanzania ‘Taifa Stars’, Emmanuel Amunike amesikitishwa na kitendo cha nyota wake wa zamani, Farid Mussa, kwa umri wake kurejea nyumbani badala ya kuendelea kupigania ndoto zake barani Ulaya.
Akiwa nchini kwao Nigeria, Amunike alisema siku zote hakuna njia ya mkato kwenye utafutaji wa maisha bora ya soka, na kwamba hata kama kulikuwa na changamoto kadhaa ambazo alikuwa akikumbana nazo Farid huko Hispania alipaswa kuendelea kupambana.
Farid alikuwa CD Tenerife, ambapo Amunike anadai kusikia kwamba nyota huyo alikataa ofa ya kuendelea kuichezea na kufanya uamuzi wa kurejea nyumbani.
“Siku zote nimekuwa nikipenda kuwaambia wachezaji chipukizi kwamba ni vyema kupambana hata kama watu watashindwa kuona mchango wako,” alisema.
“Naelewa kwa sababu nilicheza kwa miaka mingi soka kwenye mataifa ya watu, kuna muda unaweza kucheza kwa kujituma halafu watu wakashindwa kuthamini mchango wako, wanaweza kupuuzia lakini utafika muda ambao kila mmoja atakubali.”
Wakati akicheza soka la kulipwa barani Ulaya, Amunike ambaye aliiongoza Taifa Stars kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika msimu uliopita nchini Misri aliwahi kutamba akiwa na miamba ya soka la Hispania, FC Barcelona pamoja na Sporting CP ya Ureno.
Baada ya kujiunga na Yanga, Farid alisema sababu ya kurejea kwake nyumbani ni kutoona mwanga wa kupiga hatua akiwa na CD Tenerife. “Ni kweli walitaka kuniongeza mkataba, lakini walitaka niendelee kucheza kikosi B jambo ambalo sikukubaliana nalo,” alisema.
“Walitaka nikisaidie kikosi B kupanda daraja kwa sababu kilikuwa kikishiriki Ligi Daraja la Tatu achana na kikosi cha kwanza ambacho kipo Segunda.
“Huwa wanauza hisa nadhani walishindwa kuangalia nini ndoto zangu zinataka, ningecheza madaraja ya chini hadi lini? Ni bora kurudi nyumbani na kujipanga tena.” Nyota huyo aliongeza kuwa wakati akirudi nchini alikuwa na ofa kadhaa za nje ya nchini, lakini kuyumba kwa klabu nyingi kiuchumi ndiyo sababu iliyomfanya akakubali kujiunga na Yanga kwa mkataba mfupi.
“Nina msimu mmoja wa kucheza Yanga. Najua watu wanaongea mengi, lakini najua nachofanya,” alisema winga huyo.
Farid aliondoka nchini mwaka 2016 baada ya kupata ofa ya kujiunga na CD Tenerife akitokea Azam FC , lakini aliishia kucheza kikosi B kwa takribani miaka minne aliyocheza soka la kulipwa nchini humo. Mchezaji huyo ni mmoja wa washambuliaji wa timu ya Taifa, Taifa Stars.