Azam na dakika 90 za kwenda makundi CAFCC
Muktasari:
- Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Misri, Oktoba 16, matokeo yanayoacha kila upande ukiwa na nafasi ya kufuzu. Hata hivyo, Azam ambayo ina faida kubwa itahitaji kuwa makini katika safu zote, kwa sababu sare nyingine ya mabao zaidi ya moja itawatupa nje Azam.
AZAM FC leo Jumamosi Oktoba 24, 2026, inaingia kwenye mtihani wa kuamua hatma ya safari yake ya Afrika, ikiwakaribisha ZED FC ya Misri katika mchezo wa marudiano wa raundi ya pili ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikihitaji kutumia vizuri uwanja wa nyumbani kupata tiketi ya hatua ya makundi.
Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Misri, Oktoba 16, matokeo yanayoacha kila upande ukiwa na nafasi ya kufuzu. Hata hivyo, Azam ambayo ina faida kubwa itahitaji kuwa makini katika safu zote, kwa sababu sare nyingine ya mabao zaidi ya moja itawatupa nje Azam.
Hii ni mara ya pili mfululuzo Azam inatafuta tiketi ya kwenda hatua ya makundi baada ya msimu uliopita kufuzu kwa mara ya kwanza na kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi ikiwa na pointi tisa.
IBENGE AITAKA AZAM IMALIZE KAZI
Katika mchezo wa kwanza, ZED ilitangulia kupata bao dakika ya 45 kabla ya Azam kusawazisha dakika ya 59. Azam ilionyesha uwezo wa kurejea mchezoni baada ya kuwa nyuma, lakini sasa itahitaji kutumia vizuri nafasi za kufunga na kuzuia makosa ya kiulinzi ili isijiweke kwenye mazingira magumu mbele ya mashabiki wake ambao tajiri ameshawalipia tiketi zote.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Ibenge amesema: “Bado tuna kazi kubwa ya kufanya mbele yetu. Ninashukuru kwa matokeo tuliyopata katika mchezo wa kwanza, lakini tuna kazi ya kujiandaa kwa ajili ya mchezo wa marudiano kwa sababu tunatakiwa kushinda. Hilo ndilo jambo muhimu zaidi kwetu.”
REKODI ZA AZAM KIMATAIFA
Azam inaingia katika mchezo huo ikiwa na uzoefu wa mashindano ya Afrika baada ya kufanikiwa kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita wa 2025/26.
Katika hatua za awali za msimu huo, Azam iliiondoa El Merriekh ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 4-0, ikishinda mabao 2-0 nyumbani na ugenini. Baadaye iliifunga KMKM ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 9-0, baada ya kushinda 2-0 katika mchezo wa kwanza na 7-0 katika marudiano.
Katika hatua ya makundi, Azam ilikutana na Wydad AC ya Morocco, AS Maniema Union ya Congo na Nairobi United ya Kenya. Iliambulia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Maniema nyumbani na ugenini dhidi ya ikaipiga Chamazi Nairobi United 1-0 na ikapigwa Kigali 2-0.
ZED FC SI YA KUIDHARAU
ZED ilifika raundi hii baada ya kuiondoa ASAS Djibouti Telecom ya Djibouti kwa jumla ya mabao 5-1, ikishinda 4-0 nyumbani kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini. Rekodi hiyo inaonyesha kuwa wapinzani hao wana uwezo wa kufunga mabao na wanaweza kuwa hatari Azam itakapowapa nafasi.
Mambo matatu yanaweza kuamua hatma ya mchezo huo uwezo wa Azam kutumia nafasi za kufunga, nidhamu ya safu ya ulinzi na namna timu zote zitakavyokabiliana na presha ya mchezo. Azam inahitaji kuanza kwa utulivu bila kuruhusu wapinzani kupata bao la mapema, pia haitakiwi kucheza kwa kujilinda pekee kwa sababu matokeo ya sare ya mchezo wa kwanza hayajahakikisha kufuzu.